Miongoni mwa mambo yanayotakiwa kutambulika ni kwamba elimu imegawanyika mafungu mawili:

1- Elimu ambayo ni faradhi kwa kila mmoja.

2- Faradhi kwa baadhi ya watu.

Aina ya kwanza ni ile ambayo Shaykh-ul-Islaam Muhammad bin ´Abdil-Wahhaab (Rahimahu Allaah) amesema juu yake katika kitabu chake “Usuwl-uth-Thalaathah”:

“Tambua – Allaah akurehemu – ya kwamba ni wajibu kwetu kujifunza masuala mane; la kwanza ni elimu ambayo inahusiana na kumjua Allaah, kumjua Mtume Wake na kuijua dini ya Uislamu kwa dalili.”[1]

Pia Imaam Ahmad (Rahimahu Allaah) amebainisha yale ambayo ni lazima kwa muislamu kuyajua kwa kusema:

“Ni lazima kujifunza katika elimu yale ambayo yataifanya dini yake kusimama. Akaulizwa: “Kama mfano wa nini?” Akajibu: “Ambayo hakiwi kutoyajua; kama mfano wa swalah yake, swawm yake na mfano wa hayo.”[2]

Ambayo mtu analazimika kuyajua ni kama mfano wa misingi ya imani, nembo za Uislamu na yale ambayo ya haramu ambayo anapaswa kujiepusha nayo na yale anayoruhusiwa au anayohitajia katika mambo ya biashara na mfano wake. Ni lazima kwa mtu kuyajua mambo kama haya.

Kuwauliza wanachuoni ni katika elimu. Ambaye atawauliza wanachuoni basi ametafuta nuru katika dini yake na amefanya yale yanayomlazimu. Allaah (Ta´ala) amesema:

وَمَا أَرْسَلْنَا مِن قَبْلِكَ إِلَّا رِجَالًا نُّوحِي إِلَيْهِمْ ۚ فَاسْأَلُوا أَهْلَ الذِّكْرِ إِن كُنتُمْ لَا تَعْلَمُونَ بِالْبَيِّنَاتِ وَالزُّبُرِ

“Hatujatuma kabla yako isipokuwa ni wanamme Tunawafunulia Wahy. Hivyo basi waulizeni watu wenye ukumbusho ikiwa nyinyi hamjui; kwa hoja za wazi na vitabu.”[3]

Hii ndio aina ya elimu ambayo ni faradhi kwa kila mmoja.

Aina ya pili ambayo ni faradhi kwa baadhi ya watu ni yale yaliyo chini ya hayo. Kujishughulisha nayo ni bora kuliko mtu kujishughulisha na ´ibaadah zilizopendekezwa. Haya ndio maoni sahihi zaidi ya wanachuoni. Imepokelewa kutoka kwa Imaam Ahmad (Rahimahu Allaah) kwamba amesema:

“Kujifunza na kufunza elimu ni bora kuliko jihaad na mengineyo ambao yamependekezwa.”[4]

[1] Uk. 03.

[2] ”al-Mabda´ Sharh-il-Muqniy´” (03/233) ya Ibn-ul-Muflih.

[3] 16:43-44

[4] ”al-Furuu´ wa ma´ahu taswhiyh-il-Furuu´ lil-Mardaawiy” ya Ibn-ul-Muflih (02/339).

  • Mhusika: Shaykh ´Abdus-Salaam bin Barjas
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Usuwl-ud-Da´wah as-Salafiyyah, uk. 27-29
  • Imechapishwa: 15/07/2020