04. Msingi wa kwanza: Kutilia umuhimu suala la kuisoma dini

1- Kutilia umuhimu kujifunza elimu ya dini na kuielewa dini

Kutokana kwamba makundi mengi ya Kiislamu hii leo wamejitenga mbali na elimu ya dini na kutokana pia na kwamba wafuasi wengi wa makundi hayo wamejitenga mbali na elimu ya dini, basi itambulike kwamba Da´wah ya Salafiyyah inaipa suala la kujifunza elimu umuhimu mkubwa. Kwani jambo hilo ndio msingi ambao maisha yanasimama juu yake. Kumtengeneza mtu mmojammoja na jamii nzima hakusimami na wala hakutengemai isipokuwa kwa kujifunza elimu ya dini. Kwa ajili hiyo ndio maana Allaah (Siubhaanahu wa Ta´ala) akamwamrisha Mtume Wake Muhammad (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) elimu kabla ya kutamka na kutenda. Amesema (´Azza wa Jall):

فَاعْلَمْ أَنَّهُ لَا إِلَـٰهَ إِلَّا اللَّـهُ وَاسْتَغْفِرْ لِذَنبِكَ وَلِلْمُؤْمِنِينَ وَالْمُؤْمِنَاتِ

“Basi tambua kwamba hapana mungu wa haki isipokuwa Allaah na omba msamaha kwa dhambi zako na kwa ajili ya waumini wa kiume na waumini wa kike.”[1]

Tumefanya elimu kuwa ndio msingi wa mwanzo kwa sababu njia ziko nyingi na zote ni njia za upotofu isipokuwa tu ile njia ya Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Allaah (Ta´ala) amesema:

وَأَنَّ هَـٰذَا صِرَاطِي مُسْتَقِيمًا فَاتَّبِعُوهُ ۖ وَلَا تَتَّبِعُوا السُّبُلَ فَتَفَرَّقَ بِكُمْ عَن سَبِيلِهِ

“Kwamba hii ni njia Yangu iliyonyooka, hivyo basi ifuateni na wala msifuate njia za vichochoro nyinginezo zitakufarikisheni na njia Yake.”[2]

Hakuna namna nyingine ya kumfanya mtu kupita njia ya Sunnah isipokuwa kwa kujifunza elimu ambayo itamfichulia ukweli wa mambo na kumwangazia njia. Kwa ajili hiyo ndio maana Allaah akasema kumwambia Mtume Wake Muhammad aseme (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

قُلْ هَـٰذِهِ سَبِيلِي أَدْعُو إِلَى اللَّـهِ ۚ عَلَىٰ بَصِيرَةٍ أَنَا وَمَنِ اتَّبَعَنِي

“Sema: “Hii ndio njia yangu: nalingania kwa Allaah, juu ya ujuzi na umaizi – mimi na anayenifuata.”[3]

Maneno Yake:

عَلَىٰ بَصِيرَةٍ

“.. juu ya ujuzi na umaizi… “

Bi maana juu ya dalili na hoja ambavyo ni elimu yenye manufaa.

Imaam Ahmad (Rahimahu Allaah) amesema:

“Watu wako na haja kubwa ya kujifunza elimu kuliko wanavohitajia chakula na kinywaji. Kwa sababu mtu anahitajia kula na kunywa mara moja au mara mbili kwa siku. Lakini kuhitajia kwake elimu ni kwa muda wote ambapo yeye anapumua.”[4]

[1] 47:19

[2] 06:153

[3] 12:108

[4] ”Madaarij-us-Saalikiyn” (02/470) ya Ibn-ul-Qayyim.

  • Mhusika: Shaykh ´Abdus-Salaam bin Barjas
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Usuwl-ud-Da´wah as-Salafiyyah, uk. 26-27
  • Imechapishwa: 15/07/2020