05. Sababu ya nne ya maisha mazuri: Kutilia bidii hali ya leo

4- Miongoni mwa mambo yanayoondosha ule msongo wa mawazo na misononeko ni kuzikusanya fikira zote juu ya kutilia bidii kubwa ya hali ya sasa na kutotilia umuhimu wakati unaokuja huko mbele na huzuni ya wakati uliopita. Ndio maana Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) aliomba kinga dhidi ya msongo wa mawazo na kuhuzunika[1]. Huzuni unakuwa juu ya yale mambo yaliyopita ambayo mtu hawezi kuyarudisha wala kuyarekebisha. Msongo wa mawazo unazuka kwa sababu ya kuwa na khofu juu ya siku zinazokua huko mbele. Kwa hiyo mtu anatakiwa awe mtwana wa ile siku aliyomo kwa njia ya yeye kukusanya nguvu na bidii yake katika kuitengeneza hiyo siku na wakati wake wa sasa. Hakika kuukusanya moyo juu ya jambo hilo kunapelekea kuyakamilisha matendo na pia mja atajiliwaza kuepukana na msongo wa mawazo na huzuni.

Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) anapoomba du´aa au akauelekeza Ummah wake katika du´aa, basi yeye hujihimiza – licha ya kumtaka msaada Allaah na kuwa na matumaini katika fadhilah Zake – katika bidii na jitihada ya kuhakikisha amefikia kile alichoomba kukifikia na kujiepusha na kile alichoomba kimwepuke. Kwa sababu du´aa ni yenye kwenda sambamba na kitendo. Mja anajitahidi katika yale yanayomnufaisha katika dini na dunia yake na sambamba na hilo anamuomba Mola Wake yaweze kufanikiwa yale malengo yake na kwamba amsaidie juu ya jambo hilo. Amesema (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

“Pupia yale yanayokunufaisha na mtake msaada Allaah na usivunjika moyo. Ukipatwa na kitu usiseme ´lau ningefanya kadhaa ingelikuwa kadhaa na kadha`. Badala yake sema:

قَدَّرَ اللهُ وَما شـاءَ فَعَـلَ

“Allaah amekadiria na akitakacho hufanya.”

Kwani hakika neno ´lau´ linafungua matendo ya shaytwaan.”[2]

Kwa hiyo (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akakusanya kati ya amri ya kupupia yale mambo yenye kunufaisha katika kila hali na kumtaka msaada Allaah na kutonyenyekea kushindwa ambako ni ule uvivu unaodhuru na kati ya kujisalimisha na yale mambo yaliyopita ambayo yamekwishatendeka na kushuhudia makadirio na mipango ya Allaah. Ameyafanya mambo ni sampuli mbili:

1- Fungu la kwanza ni lile ambalo mja anaweza kufanya bidii kuipata, kupatikana kwake ni jambo lenye kuwezekana, kuliondosha au kulififiza. Hapa mja ataonyesha bidii yake na wakati huohuo atamtaka msaada mwabudiwa Wake wa haki.

2- Fungu ambalo hawezi kufanya hivo. Hapa mja atatakiwa kutulizana, aridhie na ajisalimishe. Hapana shaka kwamba kuchunga msingi huu ndio sababu ya kupata furaha na kuondosha msongo wa mawazo na huzuni.

[1] Katika Hadiyth iliyopokelewa na al-Bukhaariy na Muslim.

[2] Muslim.

  • Mhusika: ´Allaamah ´Abdur-Rahmaan bin Naaswir as-Sa´diy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: al-Wasaa-il-ul-Mufiydah lil-Hayaat-is-Sa´iydah, uk. 19-20
  • Imechapishwa: 10/06/2020