04. Sababu ya tatu ya maisha mazuri: Kujishughulisha na kazi na elimu

3- Miongoni mwa sababu zinazoondosha misononeko inayokuza kupata udhaifu katika viungo vya mwili na kuushughulisha moyo na baadhi ya vitu vinavyomteketeza mtu ni kujishughulisha na kazi miongoni mwa kazi au elimu miongoni mwa elimu zenye manufaa. Jambo hilo linaupumbaza moyo kutokamana na yale mambo yanayousononesha moyo wake. Sivyo tu, bali huenda jambo hilo likamfanya yeye kusahau sababu hiyo iliyompelekea kusononeka na kusikitika. Matokeo yake nafsi yake ikafurahi na uchangamfu wake ukaongezeka. Anashirikiana katika sababu hii muumini na asiyekuwa muumini pia. Lakini muumini anapambanuka kwa imani yake, kutakasika kwa nia yake na kutaraji malipo kutoka kwa Allaah kwa sababu ya kujishughulisha kwake na elimu hiyo ambayo anajifunza au anaifunza na pia kuifanya ile kheri anayoijua. Kheri hiyo ikiwa ni ´ibaadah basi inabaki kuwa ni ´ibaadah. Na ikiwa ni kazi ya kidunia au jambo la kimazowea la kidunia ambalo limeambatana na nia njema na pia akakusudia limsaidie katika kumtii Allaah, basi jambo hilo linakuwa na athari katika kumwondoshea misononeko, msongo wa mawazo na kuhuzunika.

Kuna watu wengi waliopewa mtihani wa misononeko, kuandamwa kwa shida na maradhi mbalimbali ambapo tiba yake iliyofaulu ikawa ni kusahau ile sababu iliyomsononesha na kumsitikisha na wakati huohuo akajishughulisha na kazi miongoni mwa makazi yake.

Kazi anayojishughulisha nayo inapaswa iwe miongoni mwa zile ambazo zinailiwaza na zinapendwa na nafsi. Kwani kufanya hivo kuna matarajio makubwa ya kufikia malengo haya yenye manufaa – na Allaah ndiye mjuzi zaidi.

  • Mhusika: ´Allaamah ´Abdur-Rahmaan bin Naaswir as-Sa´diy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: al-Wasaa-il-ul-Mufiydah lil-Hayaat-is-Sa´iydah, uk. 18
  • Imechapishwa: 10/06/2020