04. Pozo ya kiungu na ya kinabii kwa wale wenye kupatwa na misiba

Pozo ya kiungu yanapatikana katika maneno ya Allaah (Ta´ala):

وَبَشِّرِ الصَّابِرِينَ الَّذِينَ إِذَا أَصَابَتْهُم مُّصِيبَةٌ قَالُوا إِنَّا لِلَّـهِ وَإِنَّا إِلَيْهِ رَاجِعُونَ أُولَـٰئِكَ عَلَيْهِمْ صَلَوَاتٌ مِّن رَّبِّهِمْ وَرَحْمَةٌ ۖ وَأُولَـٰئِكَ هُمُ الْمُهْتَدُونَ

“Wabashirie wenye kusubiri – wale ambao unapowafika msiba husema: “Hakika sisi ni wa Allaah na hakika sisi Kwake ni wenye kurejea.” – [wafikishie ya kwamba] hao zitakuwa juu yao barakah kutoka kwa Mola wao na rahmah; na hao ndio wenye kuongoka.” 02:155-157

Kuna Aayah nyingi kweli kuhusiana na subira.

Pozo ya kinabii inapatikana katika maneno ya Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

“Hakuna muislamu yoyote anayesibiwa na msiba na akasema “Sisi ni wa Allaah na Kwake ndiko tutarejea. Ee Allaah! Nilipe kwa msiba wangu na unipe kilicho bora kuliko hicho” isipokuwa Allaah humlipa kwa msiba wake na humpa kilicho bora kuliko hicho baadaye.” Muslim, Ahmad na Ibn Maajah.

Neno “Sisi ni wa Allaah na Kwake ndiko tutarejea” lina dawa kutoka kwa Allaah na Mtume Wake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) kwa wale wenye misiba. Dawa hii ni miongoni mwa dawa bora kabisa na dawa zenye manufaa anayoweza kupata yule aliyefikwa na msiba duniani na Aakhirah. Ni neno lililo la misingi miwili mikubwa ikiwa mja kweli ataitambua na kujiliwaza nayo:

Msingi wa kwanza ni mja anahakikisha kuwa yeye mwenyewe, familia yake, mali yake na watoto wake ni miliki kihakika ya Allaah (´Azza wa Jalla) ambayo alijiazima kutoka Kwake. Pale Allaah anapochukua kilichoazimwa ni kama kwamba yule muazimaji anakichukua tena kitu chake.

Msingi wa pili ni kuwa mta atarejea kwa Allaah ambaye ndiye mola Wake wa haki na aone kuwa ni lazima aiache dunia hii nyuma ya mgongo wake na amwendee Mola Wake siku ya Qiyaamah akiwa peke yake kama Alivyomuumba mara ya kwanza. Hapo alikuwa hana familia, mali wala matangamano. Badala yake anakuja kwa matendo mema na matendo maovu. Ikiwa huu ndio mwanzo na mwisho wa mja, mtu anaweza kujiuliza ni vipi anaweza kuhisi furaha kwa wana wake, mali yake au kitu kingine katika vitu vya dunia au ni vipi anaweza kuhisi huzuni kwa kitu alichokipoteza. Kule mja kufikiria juu ya mwanzo na mwisho wake ni miogoni mwa dawa kubwa kabisa yenye kutibu matatizo.

Miongoni mwa dawa vilevile ni yeye atambue kwa yakini kwamba kile kilichompata kusingelikuwa na namna yoyote kukikwepa na kile kisichompata hakuna na namna yoyote kimpate. Allaah (Ta´ala) amesema:

مَا أَصَابَ مِن مُّصِيبَةٍ فِي الْأَرْضِ وَلَا فِي أَنفُسِكُمْ إِلَّا فِي كِتَابٍ مِّن قَبْلِ أَن نَّبْرَأَهَا ۚ إِنَّ ذَٰلِكَ عَلَى اللَّـهِ يَسِيرٌ لِّكَيْلَا تَأْسَوْا عَلَىٰ مَا فَاتَكُمْ وَلَا تَفْرَحُوا بِمَا آتَاكُمْ ۗ وَاللَّـهُ لَا يُحِبُّ كُلَّ مُخْتَالٍ فَخُورٍ

“Hausibu msiba wowote katika ardhi au katika nafsi zenu isipokuwa umo katika Kitabu [Chetu] kabla Hatujamuumba. Hakika hayo kwa Allaah ni mepesi. [Mambo ni hivyo] ili msisononeke juu ya yale yaliyokuondokeeni na wala msifurahie kwa yale Aliyokupeni. Allaah Hapendi kila mwenye kujinata, anayejifakharisha.” 57:22-23

Yule mwenye kutafakari Aayah hii tukufu basi atapata dawa dhidi ya ugonjwa wa misiba. Yale yote tutayoyataja katika mlango huu yana mafungamano na Aayah hii – hivyo basi izingatie.

  • Mhusika: Imaam Muhammad bin Muhammad al-Hanbaliy al-Manbajiy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Tasliyatu Ahl-il-Maswaa-ib, uk. 13-14
  • Imechapishwa: 09/10/2016