05. Aliyepewa msiba anatakiwa kuwaangalia wengine waliopewa misiba

Katika pozo kwa wale wenye misiba ni kuwa wanatakiwa wasome Qur-aan na Sunnah. Humo ataona namna ambavyo Allaah anawapa wale wenye kusubiri na kuridhia yaliyo zaidi kabisa na makubwa kuliko lau msiba huo usingelitokea na lau Angelitaka basi angeliufanya ukawa mkubwa zaidi.

Miongoni mwa mambo yenye manufaa zaidi kwa yule aliyepata msiba ambaye anazima moto wa msiba wake ni kuwa anatakiwa kujiliwaza kwa kuwaangalia wale wenye misiba. Anatakiwa atambue kuwa kila kijiji, mji bali hata nyumba kuna mtu ambaye yuko na msiba. Kuna wanaosibiwa mara moja na wengine wakasibiwa mara nyingi. Msiba hautosita mpaka uwapate wanafamilia wote ikiwa ni pamoja na yule msibiwa. Naye anasibiwa kama wahenga wake. Akitazama kuliani basi hakuna anachoona zaidi ya mitihani. Akitazama kushotoni hakuna anachoona isipokuwa tu huzuni.

Ibn Mas´uud (Radhiya Allaahu ´anh) amesema:

“Kila mwenye furaha ana msiba. Hakuna nyumba yoyote iliyojaa furaha isipokuwa kulijaa huzuni.”

Ibn Siriyn amesema:

“Kamwe hapakuchekwa isipokuwa baada ya hapo kuliliwa.”

Kwa ajili hiyo ndio maana mja anatakiwa kutambua kuwa makimbilio ya subira na kujisalimisha ndio baraka, rehema na uongofu katika maneno ya Allaah (Ta´ala):

الَّذِينَ إِذَا أَصَابَتْهُم مُّصِيبَةٌ قَالُوا إِنَّا لِلَّـهِ وَإِنَّا إِلَيْهِ رَاجِعُونَ أُولَـٰئِكَ عَلَيْهِمْ صَلَوَاتٌ مِّن رَّبِّهِمْ وَرَحْمَةٌ ۖ وَأُولَـٰئِكَ هُمُ الْمُهْتَدُونَ

“Wale ambao unapowafika msiba husema: “Hakika sisi ni wa Allaah na hakika sisi Kwake ni wenye kurejea.” – [wafikishie ya kwamba] hao zitakuwa juu yao barakah kutoka kwa Mola wao na rahmah; na hao ndio wenye kuongoka.” 02:156-157

  • Mhusika: Imaam Muhammad bin Muhammad al-Hanbaliy al-Manbajiy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Tasliyatu Ahl-il-Maswaa-ib, uk. 14-15
  • Imechapishwa: 09/10/2016