06. Machungu ya dunia hii ni matamu huko Aakhirah

Miongoni mwa mambo yenye kuwaliwaza wale wenye misiba ni mja kuangaia kwa uoni wake na kutambua kuwa uchungu wa dunia hii kwa hakika ni utamu huko Aakhirah ambao Allaah ataubadilisha na kwamba utamu wa dunia hii kwa hakika ni uchungu huko Aakhirah. Lililo bora zaidi ni kuhama kutoka katika utamu wa kipindi cha muda na kwenda katika utamu wenye kudumu. Ikiwa hukuyaona haya basi soma maneno ya Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

“Pepo imezingirwa na matatizo na Moto umezingirwa na matamanio.” Muslim na at-Tirmidhiy.

Fahamu za watu ni zenye kutofautiana katika suala hili. Watu wengi hii leo ni wenye kuyapa kipaumbele utamu wa muda juu ya utamu wenye kudumu. Hawawezi kustahamili uchungu wa muda kwa sababu ya starehe yenye milele. Hawawezi kustahamili utwevu wa muda kwa sababu ya utukufu wa milele. Hawawezi kustahamili mtihani wa muda kwa sababu ya furaha ya milele. Haya yanatokamana na mtu kutazama yaliyoko sasa ilihali yale yenye kusubiriwa si yenye kuwepo. Imani ni dhaifu na matamamio ndio yenye kuchukua nafasi. Yanazalisha kuipa kipaumbele maisha ya dunia haya na kuyatupilia mbali maisha ya Aakhirah. Huo ndio udhahiri wa watu wengi wa leo katika mambo yao ya msingi. Hayatokamani na jengine isipokuwa kuyapenda maisha ya dunia hii. Wahb bin Munabbih ameeleza kuwa ´Iysaa bin Maryam (´alayhis-Salaam) amesema:

“Wale katika nyinyi wenye kuipenda zaidi dunia hii ndio wenye kusononeka zaidi wakati wa msiba.”

Kuhusiana na mtu mwenye kuitazama kwa jicho la ukali lenye kutoboa tundu la mapazia ya dunia hii, hali yake ni tofauti kabisa. Jibidishe katika neema ya milele na nusura kubwa ambayo Allaah amewaadalia mawalii Wake wenye kumtii na madhalilisho makubwa, khasara na adhabu ya kudumu amewaandalia watenda madhambi. Baada ya hapo chagua chaguo lililo bora zaidi. Kila mwenye kutenda anatenda lenye kuendana na yeye. Kila mwenye kwenda anaenda kule kwenye kuendana na yeye. Hii ni nasaha ya ndugu yako kwa yale yaliyo mazuri kwako na yenye kukuliwaza.

  • Mhusika: Imaam Muhammad bin Muhammad al-Hanbaliy al-Manbajiy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Tasliyatu Ahl-il-Maswaa-ib, uk. 15-16
  • Imechapishwa: 09/10/2016