07. Misiba inatakiwa kukabiliwa kwa subira na swalah

Miongoni mwa mambo yenye kuwaliwaza wenye misiba ni wao kumtaka Allaah msaada, kumtegemea, kupokea pole Yake, kumtaka msaada kwa subira na swalah, kujua kuwa Allaah yuko pamoja na wale wenye kusubiri na kumuomba Ampe subira kwa yale Aliyowaahidi.

Ibn Abiy Dunyaa amepokea kwa mlolongo wa wapokezi wake kwamba Ibraahiym bin Daawuud amesimulia ya kwamba baadhi ya wenye hekima wamesema:

“Allaah ana waja wenye kuipokea misiba kwa furaha. Watu hawa hawana lolote kwenye mioyo yao kuhusiana na dunia hii. Wahb bin Munabbih amesema: “Nimesoma kwenye Zabuur ya Daawuud: “Allaah (Ta´ala) amesema: “Ee Daawuud! Hivi unawajua ni watu gani wataoipita haraka juu ya Njia? Ni wale wenye kuridhika na hukumu Yangu na ndimi zao ni zenye kulowa daima kwa kunidhukuru.”

Muumini aliyefanikiwa – tunamuomba Allaah mafanikio – ni yule mwenye kukubali msiba, akatambua kuwa umetoka kwa Allaah na haukutoka kwa viumbe Wake na akafanya kila aliwezalo ili kuufichika. ´Abdul-´Aziyz bin Rawwaad amesema:

“Mambo matatu ni katika mambo ya Peponi; kufichika msiba, kufichika maradhi na kuifichika swadaqah.”

Baadhi ya Salaf wamesema:

“Uelewa wa watu unajaribiwa kwa mambo matatu; utajiri, misiba na uongozi.”

´Abdullaah bin Muhammad al-Harawiy amesema:

“Katika mazuri ya uchamungu ni kufichika msiba kiasi cha mtu kufikiria kuwa hujapatapo kujaribiwa.”

´Awn bin ´Abdillaah amesema:

“Wema usiokuwa na usuhubiano na shari yoyote ni kushukuru pindi mtu yuko katika hali nzuri na kuvumilia pindi mtu anapopatwa na misiba.”

  • Mhusika: Imaam Muhammad bin Muhammad al-Hanbaliy al-Manbajiy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Tasliyatu Ahl-il-Maswaa-ib, uk. 16-17
  • Imechapishwa: 09/10/2016