08. Msiba mkubwa ni mtu kupata msiba katika dini

Moja katika misiba mikubwa kabisa ni kupata msiba katika dini. Kupata msiba katika dini ndio msiba mkubwa kabisa duniani na Aakhirah. Hiyo ndio khasara ya mwisho kabisa na timilifu. Ibn Abiy Dunyaa amepokea kutoka kwa Shurayh ambaye amesema:

“Mimi pindi ninapopatwa na msiba humhimidi na kumshukuru Allaah mara nne; mara ya kwanza ni kwa sababu msiba haukubwa mbaya zaidi, mara ya pili ni kwa sababu Amenifanya kuweza kuwa na subira, mara ya tatu ni kwa sababu Amenifanya kuweza kusema “Sisi ni wa Allaah na Kwake ndiko tutarejea” kwa kutarajia thawabu zake na mara ya nne kwa sababu hakuufanya msiba huo kuipata dini yangu.”

Moja katika misiba mikubwa ya dini ni kufa kwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Msiba wake ni msiba mkubwa kuliko misiba mingine yote yenye kumsibu muislamu. Kufa kwake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) ndipo Wahy uliposimama kushuka kutoka mbinguni na hali itaendelea kuwa hivyo mpaka siku ya Qiyaamah. Utume pia umesimama. Kufa kwake ndio ilikuwa chanzo cha kudhihiri shari na ufisadi pale waarabu waliporitadi katika dini. Kifo chake ndio ilikuwa chanzo cha fundo la dini kulegea na kufunguka. Kufariki kwake Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) kuna maliwazo makubwa kabisa kwa mja na kwa misiba yote inayomsibu na mambo mengine yote ya kidunia yasiyohesabika.

Misiba inatofautiana kama tulivyosema. Msiba mkubwa kabisa ni msiba katika dini. Tunamuomba Allaah atukinge nao. Msiba katika dini ndio msiba mkubwa kabisa kuliko misiba mingine yote inayoweza kumpata mtu.

  • Mhusika: Imaam Muhammad bin Muhammad al-Hanbaliy al-Manbajiy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Tasliyatu Ahl-il-Maswaa-ib, uk. 17-19
  • Imechapishwa: 09/10/2016