04. Kuendelea kuwa na msimamo baada ya Ramadhaan

02 – Sufyaan bin ´Abdillaah ath-Thaqafiy (Radhiya Allaahu ´anh) amesema:

“Nilisema: “Ee Mtume wa Allaah! Nambie katika Uislamu kitu ambacho sintomuuliza yeyote baada yako.” Akasema: “Sema: “Nimemwamini Allaah” kisha kuwa na msimamo.”[1]

Ameipokea Muslim.

Hadiyth inafahamisha kwamba mja, baada ya kumwamini Allaah (Ta´ala), ameamrishwa kuwa na msimamo katika utiifu; kwa kufanya yaliyoamrishwa na kujiepusha na yaliyokatazwa. Hilo linakuwa kwa kulazimiana na kufuata njia ilionyooka ambayo ndio dini ilionyooka pasi na kupindapinda kuliani na kushotoni.

Ikiwa muislamu ameishi Ramadhaan na akaipamba michana yake kwa kufunga na nyusiku zake kwa kusimama usiku kuswali na akaizoweza nafsi yake kufanya mambo ya kheri, basi analazimika kulazimiana na kumtii Allaah daima. Ingawa Ramadhaan ina sifa za kipekee kuliko miezi mingine kwa njia ya kwamba mtu anatakiwa kuzidisha utiifu na kuzidisha ´ibaadah zinazopendeza, hiyo haina maana kwamba muislamu anapaswa kuendelea katika hali hiyo. Hakika hapana vyengine kinachompasa ni yeye kuwa na shauku ya kufanya mambo ya kheri na kutahadhari na maasi ili awe amefaidika na mwezi wake.

Hakika muislamu kuendelea kuwa na msimamo baada ya Ramadhaan na kutengemaa kwa maneno na vitendo vyake ni alama kubwa ya kufaidika kwake na Ramadhaan na shauku yake katika utiifu. Ni anwani ya kukubaliwa na alama ya kufuzu. Matendo ya muumini hayamaliziki kwa kumalizika kwa mwezi na kuingia mwezi mwingine. Bali matendo yanaendelea mpaka wakati wa kifo.  Amesema (Ta´a):

وَاعْبُدْ رَبَّكَ حَتَّىٰ يَأْتِيَكَ الْيَقِينُ

“… na mwabudu Mola wako mpaka ikufikie yakini.”[2]

Hata kama funga ya Ramadhaan imemalizika funga za kujitolea zimesuniwa mwaka mzima. Hata kama kusimama usiku mwezi wa Ramadhaan kutamalizika mwaka mzima ni kielezi cha kusimama kuswali. Hata kama utamalizika muda wa kutoa Zakaat-ul-Fitwr, nyakati za kutoa zakaah ya faradhi na swadaqah ya kujitolea ni yenye kutanda miaka yote. Aidha kusoma Qur-aan, kuizingatia na kila tendo jema linatakikana katika kila zama.

Miongoni mwa fadhilah za Allaah kwa waja Wake ni kuwepo wingi wa milango ya matendo mema na kuwepo aina mbalimbali ya mambo ya kheri ili uchangamfu wa muislamu uweze kudumu na abaki hali ya kuwa ni mwenye kulazimiana kumtumikia Mola wake.

[1] Muslim (38).

[2] 15:99

  • Mhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Mukhtaswar Ahaadiyth-is-Swiyaam, uk. 87
  • Imechapishwa: 10/03/2023