03. Inatosha kutamka shahaadah au ni lazima yafanyike mambo mengine?

Swali 03: Je, inatosha kutamka na kuitakidi nguzo hii miongoni mwa nguzo za Uislamu au ni lazima yapatikane mambo mengine ili ukamilike Uislamu na imani ya mtu?

Jibu: Nguzo hii ndio inayomwingiza kafiri ndani ya Uislamu. Hapo ni pale ambapo atashuhudia ya kwamba hapana mungu wa haki isipokuwa Allaah na kwamba Muhammad ni Mtume wa Allaah akiwa ni mkweli, mwenye yakini, mjuzi wa maana yake na akatendea kazi mambo hayo. Baada ya hapo atatakwa kuswali na nguzo na hukumu zingine za Uislamu zilizosalia. Kwa ajili hiyo wakati Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alipomtuma Mu´aadh kwenda Yemen alimwambia:

“Hakika wewe unawaendea watu katika watu wa Kitabu. Hivyo basi iwe kitu cha kwanza utakachowalingania kwacho iwe ni kushuhudia ya kwamba hapana mungu wa haki isipokuwa Allaah na kwamba Muhammad ni Mtume wa Allaah. Ikiwa watakutii kwa hilo, basi wafundishe ya kwamba Allaah amewafaradhishia swalah tano kila mchana na usiku. Ikiwa watakutii kwa hilo, wafundishe ya kwamba Allaah amewafaradhisha zakaah itayochukuliwa kutoka kwa matajiri wao na wapewe mafakiri wao. Ikiwa watakutii kwa hilo, tahadhari na kuwachukulia mali yao. Iogope du´aa ya mwenye kudhulumiwa, kwani hakika hakuna baina yake na baina ya Allaah kizuizi.”

Amewaamrisha swalah baada ya Tawhiyd na kumwamini Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Mosi makafiri wanatakiwa Tawhiyd na kumwamini Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Kafiri akikubali jambo hilo na akasilimu basi hukumu yake inakuwa kama ya waislamu. Kisha baada ya hapo anatakiwa kuswali na mambo mengine ya dini. Akikataa mambo hayo atakuwa na hukumu zingine. Mwenye kukataa kuswali basi anatakiwa kutakwa kutubia. Akitubia ni vyema na vinginevyo atauliwa hali ya kuwa kafiri. Haijalishi kitu hata kama hapingi uwajibu wake kwa mujibu wa maoni sahihi zaidi ya wanazuoni. Akikataa kutoa zakaah na akafanya kiburi kwayo atapigwa vita kama ambavyo Maswahabah walivyowapiga vita waliokataa kutoa zakaah wakiwa bega kwa bega pamoja na Abu Bakr (Radhiya Allaahu ´anh) na wakawahukumu kuritadi. Asipopigana juu yake basi kiongozi atamlazimisha kuitoa na kumuadhibu adhabu ya Kishari´ah itayowakhofisha watu mfano wake. Vivyo hivyo muislamu atatakiwa kufunga Ramadhaan, kuhiji Nyumba akiwa anaweza na mambo mengine ambayo Allaah amemuwajibishia. Atatakiwa pia kuacha yale mambo ambayo Allaah amemuharamishia. Kwa sababu kuingia kwake ndani ya Uislamu na kushikamana nao kunapelekea mambo hayo. Atakayetetelesha kitu miongoni mwa vile alivyowajibisha Allaah au akafanya kitu katika yale aliyoharamisha Allaah basi atataamiliwa kwa mujibu wa Shari´ah inavosema.

Ikiwa kafiri anatamka shahaadah katika hali ya ukafiri wake – kama wanavofanya makafiri wengi hivi sasa – basi atatakiwa kutubia kutokana na yale yaliyopelekea katika ukafiri wake na haitotosha kutamka kwake shahaadah. Kwa sababu bado anaitamka katika hali ya ukafiri wake lakini hajaifanyia kazi. Ikiwa ukafiri wake ni kuwaabudia wafu, majini, masanamu au viumbe wengine, kuwataka msaada na kadhalika, basi atalazimika kutubia kutokana na hayo na amtakasie ´ibaadah Allaah. Hivyo ndivo anaingia katika Uislamu. Ikiwa ukafiri wake ni kuacha swalah basi atalazimika kutubia kutokana na kitendo hicho na aitekeleze. Akiyafanya hayo ndipo anahesabika ameingia ndani ya Uislamu. Vivyo hivyo ikiwa ukafiri wake ni kwa kuhalalisha uzinzi au pombe, basi analazimika kutubu kutokana na jambo hilo. Akitubia kutokana na hayo ndipo anahesabika ameingia ndani ya Uislamu. Vivyo hivyo kafiri atatakiwa kuacha kitendo au imani iliyompelekea yeye kukufuru. Akifanya hivo ndipo anahesabika ameingia ndani ya Uislamu.

Haya ni mambo muhimu ambayo mwanafunzi anapaswa kuyatilia umuhimu na ayatambue. Wanazuoni wameyaweka wazi katika mlango unaozungumzia hukumu ya mwenye kuritadi. Ni mlango muhimu ambao mwanafunzi anapaswa kuupatiliza na ausome sana.

  • Mhusika: Imaam ´Abdul-´Aziyz bin ´Abdillaah bin Baaz
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Rukn-ul-Awwal min Arkaan-il-Islaam, uk. 20-22
  • Imechapishwa: 19/03/2023