02. Madhambi khaswa yale makubwa yanaiathiri Tawhiyd 

Swali 02: Nilifanya maasi na khaswa makubwa. Je, kitendo hicho kinaathiri nguzo miongoni mwa nguzo za Uislamu?

Jibu: Kufanya madhambi makubwa, kama vile uzinzi, kunywa pombe, kuua nafsi pasi na haki, kula ribaa, usengenyi, umbea na mengineyo katika madhambi makubwa, ni jambo linaiathiri Tawhiyd na katika kumwamini Allaah, kunainyongesha na mtenda huyo anakuwa mwenye imani dhaifu. Lakini hata hivyo hakufuru kwa mambo hayo tofauti na wanavoamini Khawaarij. Khawaarij wanamuona kuwa ni kafiri na kumfanya ni mwenye kudumishwa Motoni milele akifa katika hali hiyo pasi na kutubia. Mwenye kuiba, kuwaasi wazazi wawili au kula ribaa wanamfanya kuwa ni kafiri hata kama mtu huyo hakuona kuwa mambo hayo ni halali. Hili ni kosa kubwa la Khawaarij. Ahl-us-Sunnah wal-Jamaa´ah wanaamini kuwa sio kafiri. Bali ni mtenda dhambi na mwenye imani pungufu. Hakufuru ukafiri mkubwa. Bali imani yake inakuwa nyonge na dhaifu. Kwa ajili hiyo Allaah ameweka Shari´ah kwa mwenye kuzini kupewa adhabu ya kupigwa bakora mia moja ikiwa mzinzi huyo ni bikira na kutolewa nje ya mji mwaka mzima. Ingelikuwa kuzini kunamritadisha mtu basi ingelilazimika kumuua. Ikafahamisha kuwa hakumritadishi mtu. Mwizi pia hauliwi. Bali anakatwa mkono wake. Hilo likajulisha kuwa maasi haya hayamfanyi mtu kuritadi wala kukufuru. Lakini kunadhoofisha na kuinyongesha imani. Kwa ajili hiyo Allaah ameweka Shari´ah ya kuwatia adabu na kuwaadhibu kwa adhabu hizi za kidini ili watubu na warejee kwa Mola wao na waache yale madhambi wanayofanya. Mu´tazilah wanaona kuwa mtenda dhambi huyo anakuwa katika daraja kati ya madaraja mawili; lakini hata hivyo wanaona kuwa atadumishwa Motoni milele akifa juu ya hali hiyo. Wameenda kinyume na Ahl-us-Sunnah ambapo wanaona kuwa watenda madhambi watadumishwa Motoni milele na hivyo wakaafikiana na Khawaarij. Khawaarij wameona kuwa anakufuru na kudumishwa Motoni milele. Hawa wengine wameona kuwa atadumishwa Motoni milele lakini hata hivyo hawamwiti kuwa ni kafiri na kwamba ana ukafiri mkubwa. Makundi yote mawili hayo yamepotea kutokana na njia.

Maoni sahihi ni ´Aqiydah ya Ahl-us-Sunnah wal-Jamaa´ah ambao wanaona kuwa hakufuru kwa maana nyingine ukafiri mkubwa. Hata hivyo anakuwa mtenda dhambi na anakuwa mwenye imani dhaifu ambapo anakuwa katika khatari kubwa ya ukafiri. Lakini sio kafiri muda wa kuwa haoni kuwa maasi hayo ni halali. Bali imemtokea ameyafanya na huku akitambua kuwa ni maasi. Kilichompelekea huko ni shaytwaan, matamanio na nafsi yenye kuamrisha sana maovu. Hii ndio ´Aqiydah ya watu wa haki. Mtu huyu anakuwa chini ya matakwa ya Allaah anapokufa katika hali hiyo; akitaka kumsamehe atamsamehe na akitaka atamuadhibu kwa kiwango cha maasi yake. Allaah (Ta´ala) amesema:

إِنَّ اللَّـهَ لَا يَغْفِرُ أَن يُشْرَكَ بِهِ وَيَغْفِرُ مَا دُونَ ذَٰلِكَ لِمَن يَشَاءُ

“Hakika Allaah hasamehi kushirikishwa lakini anasamehe yaliyo chini ya hayo kwa amtakae.”[1]

Kisha baada ya Allaah kupitisha hukumu ya mtenda madhambi kuingia Motoni atamtoa na kumwingiza Peponi. Hii ndio ´Aqiydah ya watu wa haki na ndio ´Aqiydah inayoafikiana na mapokezi kutoka kwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Kinyume na wanavoamini Khawaarij na Mu´tazilah kama tulivyotangulia.

Kuhusu ambaye anakufa juu ya shirki kubwa, basi Allaah hatomsamehe kwa hali yoyote. Isitoshe Pepo ni haramu juu yake. Huyu ndiye ambaye atadumishwa Motoni milele kutokana na Aayah iliyotajwa punde na Aayah nyenginezo zinazofahamisha kuwa makafiri watadumishwa Motoni milele. Tunamuomba Allaah ulinzi kutokana na hali yao.

Kuhusu mtenda madhambi, endapo ataingia Motoni basi hatodumishwa ndani yake milele kwa milele. Bali atabaki ndani yake vile atakavyo Allaah. Huenda ukarefuka muda wake. Huku kunakuwa kudumishwa. Lakini ni kudumishwa kwa kipindi fulani na si kama watavyodumishwa milele makafiri. Allaah (Ta´ala) amesema:

وَالَّذِينَ لَا يَدْعُونَ مَعَ اللَّـهِ إِلَـٰهًا آخَرَ وَلَا يَقْتُلُونَ النَّفْسَ الَّتِي حَرَّمَ اللَّـهُ إِلَّا بِالْحَقِّ وَلَا يَزْنُونَ ۚ وَمَن يَفْعَلْ ذَٰلِكَ يَلْقَ أَثَامًا يُضَاعَفْ لَهُ الْعَذَابُ يَوْمَ الْقِيَامَةِ وَيَخْلُدْ فِيهِ مُهَانًا

“Wale ambao hawaombi pamoja na Allaah mungu mwengine na wala hawaui nafsi ambayo Allaah ameiharamisha isipokuwa kwa haki na wala hawazini; atakayefanya hivyo atakutana na adhabu – ataongezewa adhabu maradufu siku ya Qiyaamah na mwenye kudumu humo akiwa amedhalilika.”[2]

Kudumishwa huku ni kwa kipindi fulani ambapo kuna mwisho wake juu ya muuaji na mzinifu iwapo Allaah hatowasamehe na hatopokea tawbah zao. Tunamuomba Allaah usalama.

Kuhusu mshirikina, kudumishwa kwake ndani ya Motoni ni kwa milele. Allaah (Subhaanah) amesema kuhusu washirikina:

كَذَٰلِكَ يُرِيهِمُ اللَّـهُ أَعْمَالَهُمْ حَسَرَاتٍ عَلَيْهِمْ ۖ وَمَا هُم بِخَارِجِينَ مِنَ النَّارِ

“Hivyo ndivyo Allaah atakavyowaonyesha matendo yao kuwa ni majuto juu yao na wala hawatokuwa wenye kutoka Motoni.”[3]

يُرِيدُونَ أَن يَخْرُجُوا مِنَ النَّارِ وَمَا هُم بِخَارِجِينَ مِنْهَا ۖ وَلَهُمْ عَذَابٌ مُّقِيمٌ

“Watataka kutoka katika Moto lakini wao si wenye kutoka kamwe humo, na watapata adhabu ya kudumu.”[4]

لَا يُقْضَىٰ عَلَيْهِمْ فَيَمُوتُوا وَلَا يُخَفَّفُ عَنْهُم مِّنْ عَذَابِهَا ۚ كَذَٰلِكَ نَجْزِي كُلَّ كَفُورٍ

”Hawatahukumiwa [kifo] wakafa na wala hawatakhafifishiwa adhabu yake – hivyo ndivyo tunavyomlipa kila mwingi wa kukufuru.”[5]

Tunamuomba Allaah ulinzi kutokana na hali yao.

[1] 04:48

[2] 25:68-70

[3] 02:167

[4] 05:37

[5] 36:35

  • Mhusika: Imaam ´Abdul-´Aziyz bin ´Abdillaah bin Baaz
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Rukn-ul-Awwal min Arkaan-il-Islaam, uk. 16-20
  • Imechapishwa: 19/03/2023