Swali 01: Tunaomba utufafanulie maana ya nguzo ya kwanza miongoni mwa nguzo za Uislamu, maana hiyo inapelekea katika nini, mtu ataihakikisha vipi na ni ipi hukumu kwa ambaye atajahili kitu katika nguzo hiyo?

Jibu: Kwa jina la Allaah, Mwingi wa rehema, Mwenye kurehemu. Himdi zote njema anastahiki Allaah. Swalah na amani zimwendee Mtume wa Allaah, kizazi chake, Maswahabah zake na wale watakaofuata mwongozo wake.

Amma baada ya hayo;

Hakika Allaah amemtuma Mtume wake Muhammad (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) kwa watu wote; waarabu na wasiokuwa waarabu, majini na watu, waume kwa wake, ili awalinganie kumpwekesha Allaah, kumtakasia Yeye nia, kumwamini yeye (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) na ujumbe wake, kuwaamini Mitume yote, Malaika wote, vitabu vilivyoteremshwa kutoka mbinguni na kuamini siku ya Mwisho kukiwemo kufufuliwa, kukusanywa, malipo, hesabu, Pepo, Moto na makadirio ya kheri na ya shari. Allaah ameyakadiria mambo, akayajua, akayadhibiti na akayaandika (Subhaanahu wa Ta´ala). Kila kitu kinatokea kwa mipango, makadirio na kwa matakwa Yake yanayotekelezeka. Aliwaamrisha watu washuhudie ya kwamba hapana mungu wa haki isipokuwa Allaah na kwamba Muhammad ni Mtume wa Allaah. Hili ndio jambo la kwanza ambalo Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alilingania. Pia ndio nguzo ya kwanza ya Uislamu: kushuhudia ya kwamba hapana mungu wa haki isipokuwa Allaah na kwamba Muhammad ni Mtume wa Allaah. Wakati alipowaambia watu watamke ya kwamba hapana mungu wa haki isipokuwa Allaah na akawaamrisha wamwamini kuwa yeye ni Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam), basi wengi wao walikataa na wakakemea ulinganizi huu. Allaah amesimulia kuwa Quraysh walimwambia:

أَجَعَلَ الْآلِهَةَ إِلَـٰهًا وَاحِدًا ۖ إِنَّ هَـٰذَا لَشَيْءٌ عُجَابٌ

“Amewafanya waungu kuwa ni mungu Mmoja?  Hakika hili ni jambo la ajabu mno!”[1]

Amesema (Subhaanah) juu yao:

إِنَّهُمْ كَانُوا إِذَا قِيلَ لَهُمْ لَا إِلَـٰهَ إِلَّا اللَّـهُ يَسْتَكْبِرُونَ وَيَقُولُونَ أَئِنَّا لَتَارِكُو آلِهَتِنَا لِشَاعِرٍ مَّجْنُونٍ

“Hakika wao walipokuwa wakiambiwa “hapana mungu wa haki isipokuwa Allaah” wanafanya kiburi na wanasema: “Je, sisi kweli tuache waabudiwa wetu kwa ajili ya mshairi mwendawazimu?”[2]

Wakakemea ulinganizi huu kwa sababu walikuwa wamezowea kuishi kwa kuabudu mizimu, masanamu na waungu hawa pamoja na Allaah (´Azza wa Jall). Kwa ajili hiyo wakakataa ulinganizi wa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) katika kumpwekesha Allaah na kumtakasia nia Yeye. Hili ambalo Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alilingania kwalo ndilo ambalo walilingania kwalo Mitume wote. Amesema (Subhaanahu wa Ta´ala):

وَلَقَدْ بَعَثْنَا فِي كُلِّ أُمَّةٍ رَّسُولًا أَنِ اعْبُدُوا اللَّـهَ وَاجْتَنِبُوا الطَّاغُوتَ

“Hakika Tulituma katika kila ummah Mtume [awaamrishe watu wake] kwamba: “Mwabuduni Allaah na jiepusheni na Twaaghuut.””[3]

وَمَا أَرْسَلْنَا مِن قَبْلِكَ مِن رَّسُولٍ إِلَّا نُوحِي إِلَيْهِ أَنَّهُ لَا إِلَـٰهَ إِلَّا أَنَا فَاعْبُدُونِ

“Hatukutuma kabla yako Mtume yeyote isipokuwa Tulimfunulia Wahy ya kwamba: “Hakika hapana mwabudiwa wa haki isipokuwa Mimi; hivyo basi niabuduni.”[4]

al-Bukhaariy na Muslim wamepokea kupitia kwa Ibn ´Umar (Radhiya Allaahu ´anhumaa) aliyesimulia kuwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Uislamu umejengwa juu ya mambo matano: kushuhudia ya kwamba hapana mungu wa kweli isipokuwa Allaah na kwamba Muhammad ni Mtume wa Allaah, kusimamisha swalah, kutoa zakaah, kufunga Ramadhaan na kuhiji Nyumba.”[5]

Katika “as-Swahiyh” tena imepokelewa kupitia kwa ´Umar bin al-Khatwaab (Radhiya Allaahu ´anh) kwamba Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alijiliwa na muulizaji mmoja akimuuliza akiwa na umbile la bwana mmoja aliyevaa nguo nyeupe sana na nywele zake zikiwa nyeusi sana. Isitoshe hakuwa na alama yoyote ya safari na hakuna yeyote katika waliokuwepo pale ambaye alikuwa anamjua. Akasema:

“Ee Muhammad, nieleze kuhusu Uislamu!” Akasema (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akasema: “Uislamu ni kushuhudia kuwa hapana mungu wa haki isipokuwa Allaah na kwamba Muhammad ni Mtume wa Allaah, kusimamisha swalah, kutoa zakaah, kufunga Ramadhaan na kwenda kuhiji Nyumba kwa yule mwenye uwezo wa kuiendea.” Akasema: “Umesema kweli!” Maswahabah wakasema: “Tukashangazwa kuona anamuuliza kisha anamsadikisha.”Kisha akasema: “Nieleze kuhusu imani!” Akasema: “Imani ni kumuamini Allaah, Malaika Wake, Vitabu Vyake, Mitume Yake na siku ya Mwisho na kuamini Qadar; ya kheri na ya shari yake.” Akasema: “Umesema kweli!” Akasema: “Nielezee kuhusu Ihsaan!” Akasema: “Ni kumuabudu Allaah kama vile unamuona. Ikiwa wewe humuoni, basi Yeye anakuona…”[6]

Kisha Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akawaeleza kuwa muulizaji huyu ni Jibriyl na kwamba amewajia ili awafunze dini yao. Ilipokuwa hawamuulizi maswali, basi ndipo Jibriyl akawajia baada ya amri ya Allaah aulize kuhusu dini hii tukufu ili wajifunze na wapate kufaidika. Kwa hivyo dini ya Uislamu imejengeka juu ya nguzo hizi tano zinazoonekana:

1 – Kushuhudia ya kwamba hapana mungu wa haki isipokuwa Allaah na kwamba Muhammad ni Mtume wa Allaah.

2 – Kusimamisha vipindi vitano vya swalah.

3 – Kutoa zakaah.

4 – Kufunga Ramadhaan.

5 – Kuhiji Nyumba Tukufu ya Allaah kwa ambaye ataweza kuiendea.

Uislamu umejengeka pia juu ya nguzo zilizojificha za kimoyo; nazo ni kumuamini Allaah, Malaika Wake, Vitabu Vyake, Mitume Yake, siku ya Mwisho na Qadar; kheri na shari yake. Ni lazima kwa kila ambaye ´ibaadah ni yenye kumuwajibikia aamini misingi hii sita iliyojificha inayohusiana na moyo. Aamini kuwa Allaah ndiye Mola Wake, Mungu Wake Naye (Subhaanau wa Ta´ala) ndiye anastahiki kuabudiwa.

Awaamini Malaika wa Allaah, Vitabu vya Allaah ambavyo amewateremshia Mitume kukiwemo Tawraat, Injiyl, Zabuur na Qur-aan.

Awaamini pia Mitume wa Allaah ambao Allaah amewatumia waja Wake ambapo wa kwanza wao ni Nuuh na wa mwisho wao ni Muhammad (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Nao ni wengi Allaah amewabainisha ndani ya Qur-aan Tukufu.

Aamini pia siku ya Mwisho ambapo ni kufufuliwa baada ya kufa, kufanyiwa hesabu, malipo na mambo mengine yanayohusiana na Aakhirah. Waumini watapata furaha na Pepo. Makafiri watapata khasara, majuto na Moto.

Ni lazima pia kuamini makadirio ya kheri na ya shari na kwamba amekadiria mambo, akayajua, akayaandika na kuyadhibiti. Aliyoyataka Allaah kuwa yanakuwa, na yale asiyoyataka yawepo hayawepo. Kila kilichopo katika mambo ya kheri, mambo ya shari, utifiu na maasi yamekwishatangulia katika ujuzi wa Allaah, kuyaandika na kuyakadiria (Subhaanahu wa Ta´ala).

Msingi wa kwanza mkuu ambao wamekuja nao Mitume ni kuamini ya kwamba Allaah (Subhaanahu wa Ta´ala) ndiye Mungu wa haki. Hii ndio maana ya kushuhudia ya kwamba hapana mungu isipokuwa Allaah. Msingi huu wa misingi ni jambo ambalo Mitume wote (Swalla Allaahu ´alayhim wa sallam) wameafikiana juu yake. Wote walilingania katiak msingi huu wa misingi: nao ni watu waamini ya kuwa Allaah ndiye mungu wa haki na kwamba hapana mwabudiwa mwingine wa haki isipokuwa Yeye. Hii ndio maana ya hapana mungu isipokuwa Allaah. Bi maana hakuna mwabudiwa wa haki isipokuwa Allaah. Vile vinavyoabudiwa na watu katika masanamu, miti, mawe, Mitume, mawalii na Malaika vyote ni batili. ´Ibaada ya haki inakuwa kwa Allaah (Subhaanahu wa Ta´ala). Amesema (Subhaanah):

وَإِلَـٰهُكُمْ إِلَـٰهٌ وَاحِدٌ ۖ لَّا إِلَـٰهَ إِلَّا هُوَ الرَّحْمَـٰنُ الرَّحِيمُ

“Mungu wenu ni Mungu mmoja pekee; hapana mwabudiwa wa haki isipokuwa Yeye, Mwingi wa huruma, Mwenye kurehemu.”[7]

وَقَضَىٰ رَبُّكَ أَلَّا تَعْبُدُوا إِلَّا إِيَّاهُ

“Mola wako ameamuru kwamba: “Msiabudu isipokuwa Yeye pekee.”[8]

إِيَّاكَ نَعْبُدُ وَإِيَّاكَ نَسْتَعِينُ

”Wewe Pekee tunakuabudu na Wewe Pekee tunakuomba msaada.”[9]

وَمَا أُمِرُوا إِلَّا لِيَعْبُدُوا اللَّـهَ مُخْلِصِينَ لَهُ الدِّينَ حُنَفَاءَ

“Hawakuamrishwa jengine isipokuwa wamuabudu Allaah pekee hali ya kumtakasia yeye dini, wenye kupondoka kwenye haki na kuiacha batili.”[10]

ذَٰلِكَ بِأَنَّ اللَّـهَ هُوَ الْحَقُّ وَأَنَّ مَا يَدْعُونَ مِن دُونِهِ هُوَ الْبَاطِلُ

“Hivyo ni kwa kuwa Allaah ndiye wa haki na kwamba vile wanavyoomba badala Yake ndiyo batili.”[11]

Mbali na msingi huu, ni lazima kuwaamini Mitume (Swalla Allaahu ´alayhim wa sallam) kuanzia kwa Aadam na waliokuja baada yake. Katika zama za Aadam kwa kizazi chake walitakiwa kufuata yale ambayo Allaah alimteremshia, akamuwekea katika Shari´ah katika elimu, matendo ambapo msingi wake ni kumpwekesha Allaah, kumtakasia Yeye nia na kumwamini Mtume na Nabii Wake Aadam (Swalla Allaahu ´alayhim wa sallam). Katika zama za Nuuh na watu wake waliokuja baada yake ilikuwa kumuamini Nuuh na kufuata yale aliyokuja nayo pamoja na kumpwekesha Allaah na kumtakasia Yeye nia. Nuuh ndiye alikuwa Mtume wa kwanza kutumwa kwa watu wa ulimwenguni baada ya kuzuka shirki kati yao. Kabla ya hapo watu walikuwa juu ya Tawhiyd ambayo Allaah alimtumiliza nayo Aadam (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) na akawafunza kizazi chake. Kwa watu wa Nuuh ilikuwa kumuamini Huud, kufuata ujumbe wake pamoja na kumpwekesha Allaah (Subhaanahu wa Ta´ala). Katika zama za Swaalih na watu wake ilikuwa kumuamini Swaalih, kufuata ujumbe wake pamoja na kumpwekesha Allaah. Vivyo hivyo katika wakati wa kila Mtume ilikuwa ni lazima kumpwekesha Allaah na kumuamini ya kwamba hapana mungu wa haki isipokuwa Allaah. Ukiongezea ya kwamba ni lazima pia kuwaamini Mitume na kufuata nyujumbe zao mpaka zama za ´Iysaa mwana wa Maryam (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) ambaye ndiye Nabii wa mwisho wa wana wa israaiyl. Baada ya hapo Allaah akamtumiliza wa mwisho wao na mbora wao ambaye ni Mtume wetu Muhamamd (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). ´Iysaa ndiye Nabii wa mwisho wa wana wa israaiyl na Muhammad ndiye Nabii na Mtume wa mwisho kwa watu wote. Hakuna baada yake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) Nabii wala Mtume mwingine atakayekuja. Yeye ndiye Mtume bora, ndiye kiongozi wao na wa mwisho wao. Kwa hivyo ni lazima kwa ummah wote wa Muhammad (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam); kuanzia majini na watu, waarabu na wasiokuwa waarabu, waume kwa wake, matajiri kwa mafukara, watawala na wanaotawaliwa. Ni lazima kwa wote kumuamini Mtume huyu na wale Mitume na Manabii wengine (Swalla Allaahu ´alayhim wa sallam) waliokuwa kabla yake. Asiyemuamini hana Uislamu wala dini yoyote. Ni lazima kuamini ya kuwa Allaah ndiye Mungu wa haki na kwamba hakuna mungu wa haki mwingine isipokuwa Yeye. Ni lazima pia kumuamini Muhammad (Swalla Allaahu ´alayhim wa sallam) na kwamba ndiye Mtume wa Allaah wa haki kwa watu wote. Asiyeamini shahaadah hizi mbili sio muislamu. Ni lazima kuziamini, kuitakidi maana yake na kwamba ´hapana mungu isipokuwa Allaah` maana yake ni kwamba hapana mwabudiwa wa haki isipokuwa Allaah. Haijuzu kumwabudu Malaika, Nabii, mti, jiwe, jini, sanamu au vyenginevyo pamoja na Allaah. Mtu akimuomba Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amnusuru baada ya kufa kwake, akamuomba bwana al-Badawiy amnusuru, amponye mgonjwa wake, akamuomba bwana al-Husayn, bwana ´Abdul-Qaadir au akawaomba msaada na mfano wa hayo, yote haya ni kumshirikisha Allaah (´Azza wa Jall) na kunabatilisha maana ya shahaadah yake. kwa sababu hukumwabudu Allaah peke yake. Bali umemshirikisha Allaah pamoja na wengine na umemuomba Allaah pamoja na wengine ilihali Allaah anasema:

وَأَنَّ الْمَسَاجِدَ لِلَّـهِ فَلَا تَدْعُوا مَعَ اللَّـهِ أَحَدًا

“Sehemu zote za kuswalia ni kwa ajili ya Allaah, hivyo basi msiombe yeyote pamoja na Allaah.”[12]

وَلَا تَدْعُ مِن دُونِ اللَّـهِ مَا لَا يَنفَعُكَ وَلَا يَضُرُّكَ ۖ فَإِن فَعَلْتَ فَإِنَّكَ إِذًا مِّنَ الظَّالِمِينَ

“Wala usiombe badala ya Allaah asiyekufaa [ukimwabudu] na wala asiyekudhuru [usipomwabudu]. Na ukifanya hivyo, basi hakika utakuwa miongoni mwa madhalimu.”[13]

وَمَا أُمِرُوا إِلَّا لِيَعْبُدُوا اللَّـهَ مُخْلِصِينَ لَهُ الدِّينَ حُنَفَاءَ

“Hawakuamrishwa jengine isipokuwa wamuabudu Allaah pekee hali ya kumtakasia yeye dini, wenye kupondoka kwenye haki na kuiacha batili.”[14]

وَقَضَىٰ رَبُّكَ أَلَّا تَعْبُدُوا إِلَّا إِيَّاهُ

“Mola wako ameamuru kwamba: “Msiabudu isipokuwa Yeye pekee.”[15]

إِيَّاكَ نَعْبُدُ وَإِيَّاكَ نَسْتَعِينُ

”Wewe Pekee tunakuabudu na Wewe Pekee tunakuomba msaada.”[16]

Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Du´aa ndio ´ibaadah.”[17]

Amesema (´Azza wa Jall):

ادْعُونِي أَسْتَجِبْ لَكُمْ ۚ

“Niombeni, Nitakuitikieni.”[18]

Kwa hivyo ni lazima kumtakasia ´ibaadah Allaah pekee na miongoni mwa ´ibaadah ni pamoja na du´aa. Ukimuomba maiti, mti au sanamu akuokoe, akunusuru, amponye mgonjwa wako na kadhalika ni shirki kubwa na inachengua shahaadah yako. Vivyo hivyo mwenye kumkadhibisha Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) au wengineo katika Mitume na Manabii (Swalla Allaahu ´alayhim wa sallam), akatilia shaka ujumbe wake, akaona kuwa ametumwa kwa waarabu peke yao au akaona kuwa sio Mtume wa mwisho na kwamba baada yake kuna Mitume wengine, yote haya ni ukafiri mkubwa na upotofu na kunachengua Uislamu wake.

Hapo inapata kufahamika ukafiri wa Qaadiyaaniyyah kwa kuamini kwao utume wa Mirzaa Ghulaam Ahmad ambaye wanamuona kuwa Nabii wao baada ya Muhammad (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) baada ya karne nyingi. Kwa hiyo ni lazima kuamini ya kwamba Muhammad (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) ndiye Mtume wa Allaah wa haki kwa walimwengu wote majini na watu. Ni lazima pia kuamini kuwa yeye ndiye Nabii na Mtume wa mwisho na kwamba hakuna baada yake Nabii wala Mtume mwingine. Ni lazima pia kuamini kuwa yule atakayedai kuwa ni Mtume baada yake, kama alivofanya Musaylamah mwongo, basi ni kafiri na mwongo. Vivyo hivyo al-Aswad al-´Ansiy Yemen, Sajaah at-Tamiymiyyah, Mukhtaar bin Abiy ´Ubayd at-Thaqafiy na wengineo waliodai kuwa ni Manabii baada yake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Maswahabah (Radhiya Allaahu ´anhum) wameafikiana juu ya ukafiri wao na kuwapiga vita kwa sababu ya kukadhibisha maana ya maneno Yake (Subhaanah):

مَّا كَانَ مُحَمَّدٌ أَبَا أَحَدٍ مِّن رِّجَالِكُمْ وَلَـٰكِن رَّسُولَ اللَّـهِ وَخَاتَمَ النَّبِيِّينَ ۗ وَكَانَ اللَّـهُ بِكُلِّ شَيْءٍ عَلِيمًا

“Hakuwa Muhammad baba wa yeyote miongoni mwa wanaume wenu, lakini ni Mtume wa Allaah na ni mwisho wa Manabii. Na Allaah daima kwa kila kitu ni Mjuzi.”[19]

Kumepokelewa Hadiyth nyingi mno kutoka kwa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) kwamba amesema:

“Mimi ni Nabii wa mwisho na hakuna Nabii mwingine baada yangu.”[20]

Swalah na amani ziwe juu yake.

Shahaadah hii ndio msingi wa misingi na ndio nguzo ya kwanza ya Uislamu. Hakuna Uislamu isipokuwa kwa shahaadah hizi mbili ambapo mtu anatakiwa kuzitamka, kuzifanyia kazi na kuziamini. Endpo ataswali, akatoa zakaah, akafunga, akahiji, akamtaja Allaah kwa wingi, lakini hata hivyo asiamini kuwa Allaah ndiye anastahiki kuabudiwa, basi anakuwa kafiri kama wanafiki. Vivyo hivyo mwenye kuona kuwa hakuna vibaya kuabudu mizimu na masanamu na pia akaona ni sawa kumwabudu al-Badawiy, al-Husayn, Shaykh ´Abdul-Qaadir al-Jaylaaniy, ´Aliy bin Abiy Twaalib au wengineo katika Mitume, mawalii au majini, ambaye ataona kuwa inafaa kuwaabudu pamoja na Allaah na kwamba inafaa kuwataka msaada na kuwawekea nadhiri anakuwa amemshirikisha Allaah (´Azza wa Jall) na maneno na imani yake hiyo inachengua na kubatilisha shahaadah yake. Amesema (Subhaanah):

وَلَوْ أَشْرَكُوا لَحَبِطَ عَنْهُم مَّا كَانُوا يَعْمَلُونَ

“Lau wangemshirikisha bila shaka yangeporomoka yale waliyokuwa wakitenda.”[21]

وَلَقَدْ أُوحِيَ إِلَيْكَ وَإِلَى الَّذِينَ مِن قَبْلِكَ لَئِنْ أَشْرَكْتَ لَيَحْبَطَنَّ عَمَلُكَ وَلَتَكُونَنَّ مِنَ الْخَاسِرِينَ

“Hakika umefunuliwa Wahy na kwa wale walio kabla yako kwamba: “Ukifanya shirki bila shaka yataporomoka matendo yako na hakika utakuwa miongoni mwa waliokhasirika.”[22]

Vilevile endapo ataona kuwa Muhamamd (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) sio Mtume wa mwisho au kwamba hakutumwa kwa watu na majini, bali ametumwa kwa waarabu peke yao, anakuwa kafiri kwa andiko na maafikiano ya wanazuoni. Ni lazima kwa ambaye ´ibaadah ni yenye kumuwajibikia kuamini kuwa yeye ni Mtume wa Allaah kwa majini na watu wote na ni lazima pia kuamini kuwa yeye ndiye Mtume wa mwisho na hakuna baada yake Nabii wala Mtume mwingine. Huu ndio msingi wa misingi. Baada ya hili ndipo muislamu atatakiwa swalah, zakaah, kufunga, kuhiji Nyumba na yaliyosalia katika maamrisho na kuacha makatazo. Mbali na kuamini kuwa Muhammad ni Mtume wa Allaah, ni lazima vilevile kuwasadikisha Mitume wote waliotangulia na kwamba (Swalla Allaahu ´alayhim wa sallam) walitekeleza ujumbe na kuufikisha kwa watu. Sambamba na haya yote ni lazima pia kuyasadikisha yale yote ambayo Allaah na Mtume Wake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) wameeleza katika mambo yaliyokuwepo na yatakayokuwepo katika zama za mwisho na siku ya Qiyaamah.

[1] 38:05

[2] 37:35

[3] 16:36

[4] 21:25

[5] al-Bukhaariy (08), Muslim (16), at-Tirmidhiy (2609), an-Nasaa´iy (5001) na Ahmad (06/26).

[6] Muslim (08), at-Tirmidhiy (2610), an-Nasaa´iy (3990), Abu Daawuud (4690), Ibn Maajah (63) na Ahmad (01/56).

[7] 02:163

[8] 17:23

[9] 01:05

[10] 98:05

[11] 22:62

[12] 72:18

[13] 10:106

[14] 98:05

[15] 17:23

[16] 01:05

[17] at-Tirmidhiy (6969) na Ibn Maajah (3868).

[18] 40:60

[19] 33:40

[20] at-Tirmidhiy (2219) na Ahmad (05/278).

[21] 06:88

[22] 39:65

  • Mhusika: Imaam ´Abdul-´Aziyz bin ´Abdillaah bin Baaz
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Rukn-ul-Awwal min Arkaan-il-Islaam, uk. 05-16
  • Imechapishwa: 19/03/2023