Amechelewesha kulipa deni la Ramadhaan kwa miaka mingi

Swali: Umri wangu ni miaka 84. Miaka michache iliyopita nilikula Ramadhaan yote kwa amri ya daktari kwa sababu nilikuwa mgonjwa. Baada yake nikala Ramadhaan nyingine siku kumi na tano kutokana na sababu nyingine. Kumeshapita miaka mingi na sijalipa siku hizo. Nikafunga baada yake. Hivi sasa nataka kuzilipa. Nifanye nini?

Jibu: Ni lazima kwako kulipa pamoja na kutubu kwa Allaah (Jalla wa ´Alaa) kutokana na ucheleweshaji uliofanya. Ni lazima kwako kumuomba Allaah msamaha, utubie Kwake na ujutie uliyoyafanya. Ni lazima kwako kuzilipa siku hizo na utoe chakula kumpa masikini kwa kila siku moja iliyokupita. Utatoa nusu pishi ya kile chakula kinacholiwa sana katika mji. Kwa maana nyingine yanakulazimu mambo matatu:

1 – Kulipa na kuharakisha kufanya hivo.

2 – Kulisha masikini kwa kila siku moja iliyokupita ikiwa una uwezo wa hilo. Ukiwa ni fakiri na huwezi, basi huhitaji kulisha chakula. Lakini suala la kulipa litabaki palepale.

3 – Kutubu kwa Allaah kutokana na ucheleweshaji huu, kuomba msamaha na kujutia. Na yule mwenye kutubu basi Allaah humkubalia tawbah yake. Tunamuomba Allaah atuongoze sisi na wewe.

  • Mhusika: Imaam ´Abdul-´Aziyz bin ´Abdillaah bin Baaz
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: https://binbaz.org.sa/fatwas/10772/حكم-تاخير-قضاء-صوم-رمضان-لعدة-سنوات
  • Imechapishwa: 19/03/2023