204 – Rabaah bin ´Abdir-Rahmaan bin Abiy Sufyaan bin Huwaytwib amesimulia kutoka kwa bibi yake ambaye amesimulia kutoka kwa baba yake aliyeeleza kuwa amemsikia Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akisema:

لا وضوءَ لِمَنْ لَمْ يَذكرِ اسمَ الله عليه

“Hana wudhuu´ ambaye hakutaja jina la Allaah kabla yake.”[1]

Ameipokea at-Tirmidhiy na tamko ni lake, Ibn Maajah na al-Bayhaqiy. at-Tirmidhiy amesema:

“Muhammad bin Ismaa´iyl – bi maana al-Bukhaariy – amesema: “Kitu bora kilichopokelewa katika maudhui haya ni Hadiyth aliyoisimulia Rabaah bin ´Abdir-Rahmaan bin Abiy Sufyaan bin Huwaytwib, kutoka kwa bibi yake, kutoka kwa baba yake.” Baba yake alikuwa anaitwa Sa´iyd bin Zayd bin ´Amr bin Nufayl.”

Zipo Hadiyth nyingi juu ya maudhui haya na hakuna yoyote inayosalimika na kasoro. al-Hasan, Ishaaq bin Raahuuyah na Dhwaahiriyyah wanaona kuwa ni lazima kutaja jina la Allaah kabla ya kutawadha kiasi cha kwamba mtu akiacha kutaja jina la Allaah kwa makusudi basi analazimika kutawadha upya. Haya ni moja katika maoni ya Imaam Ahmad. Ingawa hakuna Hadiyth yoyote juu ya mada hiyo inayosalimika kutokana na kasoro, hakika zinatiana nguvu kutokana na wingi wa njia zake na hivyo zinakuwa na nguvu – na Allaah ndiye mjuzi zaidi.

[1] Nzuri.

  • Mhusika: Imaam ´Abdul-´Adhwiym bin ´Abdil-Qawiy al-Mundhiriy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Swahiyh-ut-Targhiyb wat-Tarhiyb (1/201)
  • Imechapishwa: 04/01/2024
  • taaliki: Imaam Muhammad Naaswir-ud-Diyn al-Albaaniy