Tunaposema kabla ya Uislamu tunakusudia zama kabla ya kuja Uislamu ambazo waarabu walikuwa wakiishi kwa mtindo maalum na wengineo ulimwenguni wakiishi kwa mtindo wenye kuenea. Watu walikuwa wakiishi katika kipindi kisichokuwa na Mitume na kufutika kwa njia ya haki. Kama ilivyotajwa katika Hadiyth ya kwamba Allaah aliwatazama na akawachukia waarabu na wasiokuwa waarabu isipokuwa wachache katika Ahl-ul-Kitaab.

Mwanamke katika kipindi hichi sehemu kubwa alikuwa akiishi katika wakati mgumu na khaswa katika jamii ya kiarabu kwa vile walikuwa wakichukia kuzaliwa kwake. Miongoni mwao wako ambao walikuwa wakimzika hali ya kuwa hai mpaka anakufa chini ya udongo. Wengine walikuwa wakimwacha na huku akibaki katika maisha ya udhalili na utwevu. Kama alivosemaa Allaah (Ta´ala):

وَإِذَا بُشِّرَ أَحَدُهُم بِالْأُنثَىٰ ظَلَّ وَجْهُهُ مُسْوَدًّا وَهُوَ كَظِيمٌ يَتَوَارَىٰ مِنَ الْقَوْمِ مِن سُوءِ مَا بُشِّرَ بِهِ ۚ أَيُمْسِكُهُ عَلَىٰ هُونٍ أَمْ يَدُسُّهُ فِي التُّرَابِ ۗ أَلَا سَاءَ مَا يَحْكُمُونَ

“Anapobashiriwa mmoja wao mtoto wa kike, uso wake hupiga weusi naye huku akakaa sikitiko; anajificha kwa watu kwa ubaya aliobashiriwa: Je, amzuie kwa fedheha au amfukie ardhini. Tanabahi! Uovu ulioje wanayohukumu.”[1]

وَإِذَا الْمَوْءُودَةُ سُئِلَتْ بِأَيِّ ذَنبٍ قُتِلَتْ

”Mtoto wa kike aliyezikwa hali akiwa yuhai atakapoulizwa ”Kwa dhambi gani aliuliwa?”[2]

”al-Mauudah” ni msichana mchanga anayezikwa hai mpaka anakufa chini ya udongo. Akisalimika kuuawa na akaachwa aishi, basi anaishi maisha ya udhalili. Alikuwa hana fungu kutoka katika mirathi ya ndugu yake vovyote mali yake itavyokuwa nyingi na vovyote atavyosumbuliwa na ufakiri na haja. Kwa sababu walikuwa wakifanya mirathi kuwa maalum kwa wanaume pasi na wanawake. Bali mwanamke alikuwa akirithiwa yeye kwa mumewe ambaye amekufa kama zinavyorithiwa mali zake. Kundi kubwa la wanawake walikuwa wanaishi chini ya mume mmoja kwa vile hawakuwa wakitegemea idadi maalum ya wake bila ya kujali zile dhiki, uzito na dhuluma zinazowapata wanawake hao.

[1] 16:58-59

[2] 81:08-09

  • Mhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Tanbiyhaat ´alaa Ahkaam Takhtasswu bil-Mu´minaat, uk. 08-09
  • Imechapishwa: 17/10/2019