Imaam Ahmad bin Hanbal (Rahimahu Allaah) amesema:

“Imani ni maneno na matendo, inapanda na kushuka. Kama ilivyokuja katika mapokezi:

“Waumini walio na imani kamilifu zaidi ni wale walio na tabia bora zaidi.”[1]

MAELEZO

Hii ndio ´Aqiydah ya Ahl-us-Sunnah wal-Jamaa´ah juu ya imani. Imani ni kutamka kwa ulimi, kuamini kwa moyo na matendo ya viungo. Inapanda kwa utiifu na inashuka kwa maasi. Kuna ambao wana imani kamilifu na wengine wana imani pungufu.

Imani ya waumini ni yenye kutofautiana katika asili yake na ukamilifu wake, kama inavyofahamisha Qur-aan na Sunnah. Amesema (Ta´ala):

هُوَ الَّذِي أَنزَلَ السَّكِينَةَ فِي قُلُوبِ الْمُؤْمِنِينَ لِيَزْدَادُوا إِيمَانًا مَّعَ إِيمَانِهِمْ

“Yeye ndiye aliyeteremsha utulivu katika nyoyo za waumini ili awazidishie imani pamoja na imani zao.”[2]

Amesema kuhusu wale waumini wenye imani kamilifu:

وَإِذَا تُلِيَتْ عَلَيْهِمْ آيَاتُهُ زَادَتْهُمْ إِيمَانًا

“Wanaposomewa Aayah Zake huwazidishia imani.”[3]

Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) kuhusu mwenye imani pungufu:

“Hazini mwenye kuzini wakati anapozini hali ya kuwa ni muumini, haibi mwenye kuiba pindi anapoiba hali ya kuwa ni muumini, hanywi pombe mwenye kunywa pombe pindi anapokunywa pombe hali ya kuwa ni muumini, hapori mwenye kupora pindi anapopora, jambo linalofanya watu kumwangalia kwa ajili ya hilo, hali ya kuwa ni muumini.”[4]

Hadiyth inalenga imani kamilifu, jambo ambalo punde tumelitaja kutokana na Hadiyth kuhusu uombezi. Hivyo imani inazidi na inashuka. Hii ndio ´Aqiydah ya Ahl-us-Sunnah wal-Jamaa´ah ambao iliojengeka juu ya Qur-aan na Sunnah Swahiyh. Amesema (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

“Yule katika nyinyi mwenye kuona maovu, basi ayazuie kwa mkono wake. Asipoweza, afanye hivo kwa kuzungumza. Asipoweza, afanye hivo kwa mdomo wake. Asipoweza, afanye hivo kwa moyo wake na hiyo ni imani dhaifu kabisa.”[5]

Hadiyth hii ni dalili inayoonyesha kuwa imani inadhoofika. Hii ndio haki juu ya masuala haya na kwa ajili hiyo maoni ya Murji-ah (ambao ni Jahmiyyah, Karraamiyyah, Ashaa´irah na Murji-ah al-Fuqahaa´) yanatakiwa kupuuzwa. Wamepondoka kuiacha haki juu ya masuala haya na wameenda kinyume na dalili za wazi katika Qur-aan na Sunnah na ´Aqiydah na mfumo wenye busara. Hata hivo kupondoka kwao kunatofautiana kutegemea na upindaji wao na kuwa kwao mbali na usawa.

[1] Abu Daawuud (4682) na at-Tirmidhiy (1162). Nzuri na Swahiyh kwa mujibu wa al-Albaaniy.

[2] 48:04

[3] 08:02

[4] al-Bukhaariy (2475) na Muslim (57).

[5] Ahmad (3/10) na Muslim (49).

  • Mhusika: ´Allaamah Zayd bin Muhammad al-Madkhaliy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: at-Ta´liyqaat al-Latwiyfah ´alaa Usuwl-is-Sunnah al-Muniyfah, uk. 99-100
  • Imechapishwa: 17/10/2019