Kuuza bidhaa kwa pesa zaidi ya uliyoambiwa uuze na mwenye bidhaa yake

Swali: Ni ipi hukumu endapo mtu atanipa kazi ya kumuuazia bidhaa kwa mfano akanambia niiuze kwa pesa mia moja ambapo mimi nikaiuza kwa pesa mia moja na kumi na hiyo kumi nikaichukua mimi. Je, kitendo hichi kinajuzu?

Jibu: Hakijuzu. Iwapo mtu atakwambia umuulize bidhaa fulani kwa pesa mia moja ambapo wewe ukaiuza kwa pesa mia moja na kumi, kumi hiyo ni ya yule mwenye bidhaa yake na si yako wewe. Isipokuwa ikiwa kama atakwambia uichukue na uiuze kwa pesa mia moja na zenye kuzidi hapo ni zako, katika hali hiyo ni sawa ukaiuza kwa pesa mia moja na zenye kuzidi ni zako. Lakini kwa sharti yule aliyekupa kazi awe anajua thamani ya bidhaa hii. Kwa sababu inawezekana yule aliyekupa kazi hiyo ni mjinga juu ya bei na anadhani kuwa bidhaa yake hii haizidi pesa mia moja ndio maana akakwambia umuuzie kwa pesa mia moja na kwamba zenye kuzidi ni zako. Katika hali hii ni wajibu kwako kumwambia kwamba thamani ya bidhaa hiyo ni zaidi kama mia mbili. Kwa sababu usipofanya hivo basi utakuwa ni mwenye kumhadaa. Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Hatoamini mmoja wenu mpaka ampendelee nduguye kila anachojipendea mwenyewe.”

  • Mhusika: Imaam Muhammad bin Swaalih bin ´Uthaymiyn
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: al-Liqaa’ ash-Shahriy (57) http://binothaimeen.net/content/1296
  • Imechapishwa: 17/10/2019