Swali 740: Ni ipi hukumu ya al-´Azl?

Jibu: Dogo liwezalo kusemwa juu yake ni kwamba al-´Azl imechukizwa. Machukizo ni kwa kuzingatia wale wanachuoni wanaosema kuwa inafaa. Inaweza kuwa ni jambo linalofaa lakini hata hivyo limechukizwa. Dalili ya kujuzu kwa al-´Azl ni Hadiyth ya Jaabir iliyopokelewa katika “as-Swahiyh” mbili ya al-Bukhaariy na Muslim ambaye amesema:

“Tulikuwa tukifanya al-´Azl na wakati huohuo Qur-aan inateremka.”

Maana ya maneno ya Jaabir ni kwamba midhali tulikuwa tukifanya al-´Azl na ndani ya Qur-aan hakukuteremka hukumu ya hilo, basi maana yake ni kwamba inajuzu. Lakini tumesema kuwa imechukizwa kwa kuegemeza juu ya kujuzu. Imetoka wapi basi hukumu ya machukizo? Hukumu hii imetoka katika maneno yake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

“Oeni wanawake wenye kuzaa sana na wenye mahaba. Hakika mimi nitajifakharisha juu yenu nyumati siku ya Qiyaamah.”

Imekuja katika upokezi mwingine:

“Hakika mimi nitajigamba juu yenu kwa nyumati siku ya Qiyaamah.”

Yule ambaye anamwaga nje ya tupu ya mke wake hakupatikani shauku hii ya Mtume wake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Baadhi ya nchi zimeweka msingi jambo hili kwa yale wanayoita “ukomo wa uzazi” au “upangaji wa uzazi”, hakika ni jambo linalokwenda kinyume na matakwa ya Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) kuhusu wingi na kujifakhari.

Jengine ni kwamba jambo hili ni kuwaiga magharibi ambao hawaamini thawabu zinazopelekea juu ya kuwalea watoto. Miongoni mwazo ni maneno yake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

“Atapofariki mwanadamu basi matendo yake yote hukatika isipokuwa mambo matatu; swadaqah yenye kuendelea, elimu ambayo watu wananufaika kwayo au mtoto mwema mwenye kumuombea.”

Vilevile maneno yake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) katika yale yaliyopokelewa na al-Bukhaariy katika “as-Swahiyh” yake kupitia kwa Abu Hurayrah (Radhiya Allaahu ´anh) aliyesimulia:

“Hakuna katika waislamu – bi maana wanandoa – wanaofiwa na watoto watatu wakaguswa na Moto isipokuwa ni kule kuhalalisha kiapo.”[1]

Je, makafiri wana fadhilah mfano wa fadhilah hizi tulizonazo?

Kwa kifupi ni kwamba inajuzu kwa mke kufanya ukomo wa uzazi kwa sababu ya dharurah atazozikadiria daktari mwaminifu ambaye ni muislamu.

[1] Imaam al-Baghawiy amesema:

”Anakusudia: isipokuwa  kwa yale makadirio ya Allaah kukitakasa kiapo chake. Nayo ni yale maneno Yake (´Azza wa Jall):

وَإِن مِّنكُمْ إِلَّا وَارِدُهَا

“Hakuna yeyote miongoni mwenu isipokuwa ni mwenye kuufikia [huo Moto]. (19:71)

Atapopita na kuuvuka [huo Moto] kiapo Chake kitakuwa kimetakasika.”  Sharh-us-Sunnah (05/451).

  • Mhusika: Imaam Muhammad Naaswir-ud-Diyn al-Albaaniy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Fataawaa al-Mar´ah al-Muslimah, uk. 289
  • Imechapishwa: 17/10/2019