1 – Abu ´Abdir-Rahmaan Ahmad bin Shu´ayb bin ´Aliy an-Nasaa’iy ametukhabarisha kwa njia ya kumsomea: ´Amr bin ´Aliy ametukhabarisha: Wahb bin Jariyr ametukhabarisha: Baba yangu ametukhabarisha, kutoka kwa Ya´laa bin Hakiym, kutoka kwa ´Ikrimah, kutoka kwa Ibn ´Abbaas, ambaye amesimulia:

”Kwenye yale maradhi ambayo Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alikufa kwayo alitoka hali ya kuwa amefunga kichwa chake kwa kitambaa, akaketi juu ya mimbari na kumhimidi Allaah. Kisha akasema: ”Hakuna mtu yeyote ambaye alijitolea muhanga mkubwa nafsi na mali yake kwangu kama Abu Bakr bin Abiy Quhaafah. Kama ningechukulia kipenzi mwandani basi ningemchukua Abu Bakr awe kipenzi mwandani, lakini hata hivyo mapenzi ya Uislamu ndio bora. Nifungieni mianya yote msikitini isipokuwa mwanya wa Abu Bakr.”[1]

2 – ´Abdul-Malik bin ´Abdil-Hamiyd ametukhabarisha: al-Qa´nabiy ametukhabarisha, kutoka kwa Maalik, kutoka kwa Abun-Nadhwr, kutoka kwa ´Ubayd bin Hunayn, kutoka kwa Abu Sa´iyd al-Khudriy, ambaye ameeleza kuwa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

”Mtu ambaye alijitolea muhanga mkubwa kwangu katika matangamano yake na mali yake ni Abu Bakr. Kama ningechukulia kipenzi mwandani basi ningemchukua Abu Bakr awe kipenzi mwandani, lakini hata hivyo kubaki udugu wa Kiislamu. Wala kusibaki mwanya wowote msikitini isipokuwa mwanya wa Abu Bakr.”

3 – Azhar bin Jamiyl ametukhabarisha: Khaalid bin al-Haarith ametukhabarisha: Shu´ayb ametukhabarisha, kutoka kwa Ismaa´iyl bin Rajaa’, kutoka kwa ´Abdullaah bin Abiyl-Hudhayl, kutoka kwa Abul-Ahwasw, kutoka kwa ´Abdullaah, kutoka kwa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam), ambaye amesema:

”Kama ningechukulia kipenzi mwandani basi ningemchukua Abu Bakr awe kipenzi mwandani, lakini hata hivyo ni ndugu yangu na rafiki yangu. Allaah amemfanya rafiki yenu kuwa kipenzi mwandani.”[2]

4 – ´Amr bin ´Aliy ametukhabarisha, kutoka kwa ´Abdur-Rahmaan: Sufyaan ametuhadithia, kutoka kwa al-A´mash, kutoka kwa ´Abdullaah bin Murrah, kutoka kwa Abul-Ahwas, kutoka kwa ´Abdullaah, ambaye ameeleza kuwa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

”Hakika mimi najitenga mbali na kila kipenzi mwandani. Kama ningechukulia kipenzi mwandani basi ningemchukua mwana wa Abu Quhaafah kuwa kipenzi mwandani. Rafiki yenu ni kipenzi mwandani wa Allaah.”

5 – Muhammad bin ´Iysaa bin al-Mubaarak ametukhabarisha, kutoka kwa Ismaa´iyl, kutoka kwa Qays, kutoka kwa ´Amr bin al-´Aasw, ambaye amesimulia:

”Nilisema: ”Ee Mtume wa Allaah, ni mtu gani anayependeza zaidi kwako?” Akasema: ”´Aaishah.” Nikasema: ”Sikusudii katika wanawake.” Ndipo akasema: ”Baba yake.”[3]

6 – ´Abdur-Rahmaan bin Ibraahiym ametukhabarisha: Haaruun ametuhadithia: Yaziyd ametuhadithia: Abu Haazim ametuhadithia, kutoka kwa Abu Hurayrah, ambaye amesinulia kuwa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

”Ni nani kati yenu ambaye ameamka leo amefunga?” Abu Bakr akasema: ”Mimi.” Akasema: ”Ni nani kati yenu ambaye amemlisha leo masikini?” Abu Bakr akasema: ”Mimi.” Akasema: ”Ni nani kati yenu ameshuhudia leo jeneza?” Abu Bakr akasema: ”Mimi.” Akasema: ”Ni nani kati yenu ambaye amemtembelea leo mgonjwa?” Abu Bakr akasema: ”Mimi.”[4]

7 – ´Amr bin ´Uthmaan bin Sa´iyd ametukhabarisha: Baba yangu ametuhadithia, kutoka kwa Shu´ayb, kutoka kwa az-Zuhriy: Humayd bin ´Abdir-Rahmaan amenikhabarisha kwamba Abu Hurayrah ameeleza kwamba amemsikia Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akisema:

”Yule mwenye kujitolea vitu viwili kama hivyo katika njia ya Allaah basi ataitwa kwenye milango ya Peponi: ”Hilo ni jema.” Pepo inayo milango. Yule ambaye ni katika waswaliji basi ataitwa kutoka kwenye mlango wa swalah. Yule ambaye ni katika wapambanaji jihaad basi ataitwa kutoka kwenye mlango wa jihaad. Yule ambaye ni katika watoa swadaqah basi ataitwa kutoka kwenye mlango wa swadaqah. Yule ambaye ni katika wafungaji basi ataitwa kutoka kwenye mlango unaoitwa ar-Rayyaan.” Abu Bakr akasema: ”Je, atadhurika yule atakayeitwa katika milango hiyo? Kuna yeyote atakayeitwa kwenye milango yote hiyo, ee Mtume wa Allaah?” Akasema: ”Ndio, na nataraji wewe utakuwa miongoni mwao.”[5]

8 – Qutaybah bin Sa´iyd ametukhabarisha: Humayd bin ´Abdir-Rahmaan ametukhabarisha, kutoka kwa Salamah bin Nubaytw, kutoka kwa Nu´aym, kutoka kwa Nubaytw, kutoka kwa Saalim bin ´Ubayd (ambaye alikuwa miongoni mwa wale Maswahabah mafukara), ambaye amesema:

”Answaar alisema: ”Hebu sisi tuwe na kiongozi nanyi muwe ni kiongozi.” ´Umar akasema: ”Kwa maana nyingine panga mbili kwenye ala moja. Haiwezekani.” Kisha akamshika Abu Bakr mkononi na kusema: ”Ni nani aliye na sifa hizi tatu?

إِذْ يَقُولُ لِصَاحِبِهِ

“…alipomwambia swahiba yake… ”

Ni nani aliyekuwa Swahabah wake?

ثَانِيَ اثْنَيْنِ

”Akiwa mmoja katika wawili… ”

Ni kina nani wawili hao?

لَا تَحْزَنْ إِنَّ اللَّـهَ مَعَنَا

”Usihuzunike, hakika Allaah yuamoja nasi!”[6]

Na nani? Kisha akasema: ”Toeni kiapo!” Hivyo watu wakatoa kiapo bora na kizuri kabisa.”

9 – Muhammad bin ´Abdil-´Aziyz bin Ghazwaan ametukhabarisha: Abu Mu´aawiyah ametuhadithia: al-A´mash ametuhadithia, kutoka kwa Abu Swaalih, kutoka kwa Abu Hurayrah, ambaye amesimulia kuwa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

”Hakuna mali ya yeyote iliyoninufaisha kama ilivyoninufaisha mali ya Abu Bakr.” Abu Bakr akaanza kuangua kilio na kusema: ” Je, mimi na mali yako ni vya mwengine kama si vyako?”

[1] al-Bukhaariy (467).

[2] Muslim (2383).

[3] al-Bukhaariy (3662) na Muslim (2384).

[4] Muslim (2388).

[5] al-Bukhaariy (1897) na Muslim (1027).

[6] 9:40

  • Muhusika: Imaam Ahmad bin Shu´ayb an-Nasaa’iy (afk. 303)
  • Tarjama: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Fadhwaa-il-us-Swahaabah, uk. 33-35
  • Imechapishwa: 03/09/2026