112. Wabora katika wakeze Mtume (صلى الله عليه وسلم)

Wakeze Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) ambao ni wabora ni Khadiyjah na ´Aaishah (Radhiya Allaahu ´anhumaa). Kila mmoja katika hao wawili ana sifa za kipekee juu ya mwingine[1]. Khadiyjah ameyafanya mambo mwanzoni mwa Uislamu ambayo hayakufanywa na ´Aaishah katika kutangulia, usaidizi na unusuraji. Vilevile ´Aaishah mwishoni mwa jambo lenyewe ameyafanya mambo ambayo hayakufanywa na Khadiyjah katika kueneza elimu na kuunufaisha Ummah. Allaah amemtakasa kutokamana na yale aliyosingiziwa na wanafiki katika uzushi katika Suurah an-Nuur.

Kumchafua ´Aaishah kwa mambo ambayo Allaah amemtakasa ni ukafiri. Kwa sababu ni kuikadhibisha Qur-aan. Wanazuoni wana maoni mawili kuhusu kuwachafua mama wengine wa waumini. Maoni sahihi zaidi katika hayo mawili ni kwamba ni ukafiri. Kwa sababu ni kumchafua Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Kwani wanawake wachafu ni kwa ajili ya wanaume wachafu. 

[1] Haafidhw adh-Dhahabiy amesema alipokuwa anazungumzia wasifu wa mama wa waumini ´Aaishah:

”Alikuwa mwanamke mweupe na mrembo. Kwa ajili hiyo anaitwa al-Hamiyraa´. Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) hakumuoa mwanamke mwingine bikira zaidi yake na wala hakumpenda mwanamke yeyote kama alivyompenda. Sijui mwanamke yeyote katika Ummah wa Muhammad (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam), bali wanawake wote, mjuzi zaidi kuliko yeye. Baadhi ya wanazuoni wameona kuwa yeye ni bora kuliko baba yake, maoni ambayo ni yenye kurudishwa. Allaah amejaalia juu ya kila kitu kiwango chake. Bali tunashuhudia ya kwamba ni mke wa Mtume wetu duniani na Aakhirah. Je, kuna fakhari nyingine inayoshinda hiyo? Ijapokuwa rafiki yake Khadiyjah naye ana sifa za kipekee azisozkuwa nazo mwengine. Mimi sisemi chochote ni nani kati ya wawili hayo ni mbora zaidi. Nilisema kwa kukata kuwa Khadiyjah ndiye bora kutokana na mambo kadhaa ambayo hapa si mahali pake.” (Siyar A´laam-in-Nubalaa 02/140).  

  • Mhusika: Imaam Muhammad bin Swaalih bin ´Uthaymiyn
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Ta´aliyq mukhtaswar ´alaa Lum´at-il-I´tiqaad, uk. 155
  • Imechapishwa: 17/12/2022