Zayd bin al-Haarith bin Sharaahiyl au Sharhabiyl bin Ka´b bin ´Abdil-´Uzzaa bin Yaziyd bin ´Amriy al-Qays bin ´Aamir bin an-Nu´maan.

Zayd alikuwa ni shahidi na kamanda wa kinabii. Ametajwa kwa jina katika al-Ahzaab. Kun-yah yake ni Abu Usaamah al-Kalbiy, kisha Muhammadiy. Alikuwa bwana wa watumwa na miongoni mwa watu waliotangulia kuingia katika Uislamu. Yeye na mwanae walikuwa ni vipenzi wa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) – na hakuwa ni mwenye kupenda isipokuwa kilicho kizuri pekee.

Allaah hakumtaja swahabah yeyote kwa jina lake ndani ya Kitabu Chake isipokuwa yeye na ´Iysaa bin Maryam (´alayhis-Salaam) ambaye atateremka akiwa ni hakimu na mwadilifu. Atajiunga na Ummah huu wenye kurehemewa katika swalah zake, funga zake, hijjah zake, ndoa zake na hukumu zake zengine zote za kidini.

Imepokelewa ya kwamba alikuwa mweupe sana na mtoto wake Usaamah alikuwa mweusi. Ndio maana Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alishangazwa wakati alipowasikia watafiti wa koo pindi walisema:

“Miguu hii inaingiliana.”[1]

Sulaymaan bin Yasaar na wengine wamesema:

“Mtu wa kwanza kusilimu alikuwa Zayd bin al-Haarith.”

Ibn ´Umar amesema:

“Daima tulikuwa tunamwita Zayd bin al-Haarith kwamab ni Zayd bin Muhammad. Ndipo kukateremshwa:

ادْعُوهُمْ لِآبَائِهِمْ

“Waiteni kwa majina ya baba zao.”[2]

Jabalah bin al-Haarith amesema:

“Nilikwenda kwa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) na kusema: “Ee Mtume wa Allaah! Nirejeshee ndugu yangu Zayd.” Akasema: “Huyu hapa. Akiondoka sintomzuia.” Ndipo Zayd akasema: “Ee Mtume wa Allaah! Naapa kwa Allaah sintochagua mwingine badala yako.” Jabalah akasema: “Nikaona kuwa maoni ya ndugu yangu ni bora kuliko ya kwangu.”[3]

Ibn Ishaaq na wengineo wamemtaja kuwa mmoja katika wale walioshuhudia vita vya Badr.

Salamah bin al-Akwa´ amesema:

“Nilipigana vita bega kwa bega pamoja na Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) na nikapigana vita bega kwa bega pamoja na Zayd bin al-Haarith. Alikuwa akimfanya kuwa kamanda wetu.”[4]

´Abdullaah bin Diynaar amesema:

“Ibn ´Umar alimsikia namna ambavo Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akimteua Usaamah kuwa kamanda wa jeshi na jinsi baadhi ya watu wakiponda uongozi wa Usaamah. Ndipo akasema: “Mkiponda uongozi wake, mmekwishaponda vilevile uongozi wa baba yake. Naapa kwa Allaah kwamba alikuwa ni mtu stahiki juu ya uongozi na alikuwa ni mmoja katika watu wanaopendwa zaidi kwangu. Kadhalika mtoto wake huyu ni miongoni mwa watu wanaopendwa zaidi kwangu.”[5]

´Aaishah amesema:

“Lau Zayd angelikuwa hai, basi Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) angemfanya kuwa khaliyfah.”

´Aaishah amesema:

“Kila ambapo Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alikuwa akitumana jeshi basi alikuwa anamteua Zayd kuwa kamanda wake. Lau angelibaki baada yake, basi angemfanya kuwa khaliyfah.”[6]

Ibn ´Umar amesema:

“´Umar alimpa kiwango kikubwa cha pesa Usaamah bin Zayd kuliko alichonipa mimi. Nilipomuuliza juu ya hilo, akasema: “Alikuwa ni mwenye kupendwa zaidi kwa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) kuliko wewe na baba yake alikuwa ni mwenye kupendwa zaidi kwa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) kuliko baba yako.”

Alifariki Jumaadaa al-Uulaa mwaka wa 08. Aliishi miaka 55.

Ibn Buraydah amesimulia kutoka kwa baba yake ambaye amesema kuwa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Niiliingia Peponi na nikakutana na msichana. Nikamuuliza yeye ni wa nani ambapo akajibu: “Mimi ni wa Zayd bin al-Haarith.”

Cheni ya wapokezi wake ni nzuri.

[1] al-Bukhaariy (2555).

[2] 33:5

[3] at-Tirmidhiy (4067) aliyesema: ”Hadiyth ni nzuri na Swahiyh.”

[4] al-Bukhaariy (4272).

[5] al-Bukhaariy (6627).

[6] Ahmad (6/226).

  • Mhusika: Imaam Shams-ud-Diyn Muhammad bin Ahmad adh-Dhahabiy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Siyar A´laam-in-Nubalaa’ (1/220-230)
  • Imechapishwa: 12/01/2021