Yanayopelekea duniani na Aakhirah kwa kuacha swalah

Asiyeswali kabisa ni kafiri. Huyu ni kafiri aliyetoka katika Uislamu. Ahesabiki kuwa katika idadi ya waislamu duniani. Aakhirah atakuwa katika idadi ya makafiri. Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) ameeleza kuwa atafufuliwa na kina Fir´awn, Haamaan, Qaaruun na ´Ubayy bin Khalf. Hawa ndio viongozi wa makafiri. Atafufuliwa pamoja nao – na tunaomba kinga kwa Allaah.

Ama kuhusu duniani, ni kafiri aliyeritadi. Ni wajibu kwa mtawala amwite kuswali. Akiswali, ni sawa, la sivyo, amuue hali ya kuritadi. Akiuawa kifo cha kuritadi, atabebwa kwenye gari mbali na mji, achimbiwe shimo na kutupwa ndani yake ili nyamafu yake isiwaudhi watu kwa harufu yake na familia yake isiudhike kwa kumuona. Hastahiki heshima yoyote lau angelibaki juu ya ardhi. Kwa ajili hii ndio maana [waislamu hatutakiwi] kumvika sanda, kumswalia, hatumwingizi kwenye misikiti ya waislamu aswaliwe baada ya kufa kwake. Kwa sababu ni kafiri. Ameritadi.

Pengine mtu akasema “mapya haya jameni! Huu ni unyanyasaji au ni kutumia hisia?” [Hapana] haya ndio malipo yake. Sio unyanyasaji wala kutumia hisia. Tunasema kutokana na jinsi dalili zilivo kwa mujibu wa maneno ya Allaah (Ta´ala), maneno ya Mtume Wake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) na maneno ya Maswahabah wa Mtume Wake (Radhiya Allaahu ´anhum):

1 – Maneno ya Allaah. Allaah (Ta´ala) amesema katika Suurah “at-Tawbah” kuhusu washirikina:

فَإِن تَابُوا وَأَقَامُوا الصَّلَاةَ وَآتَوُا الزَّكَاةَ فَإِخْوَانُكُمْ فِي الدِّينِ

“Wakitubu na wakasimamisha swalah na wakatoa zakaah, basi ni ndugu zenu katika dini.” (09:11)

Kwa msemo mwingine ni kwamba ikiwa hawakufanya haya ina maana sio ndugu zetu katika dini. Ikiwa sio ndugu zetu katika dini ina maana ni makafiri. Kwa sababu upande mwingine kila muumini, hata kama atakuwa ni mtenda madhambi makubwa yasiyomtoa nje ya Uislamu, ni ndugu yako. Makundi mawili ya waislamu wakipigana vita ni jambo lenye kujulikana kumpiga vita muislamu ni kufuru. Lakini hata hivyo ni kufuru [ndogo] isiyomtoa mtu katika Uislamu. Kwa kuwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Kumtukana muislamu ni utenda dhambi mkubwa na kumpiga vita muislamu ni kufuru.”[1]

Pamoja na hivyo huyu anayempiga vita ndugu yake ni ndugu yetu. Hatoki katika Uislamu. Dalili ya hilo ni maneno ya Allaah (Ta´ala):

وَإِن طَائِفَتَانِ مِنَ الْمُؤْمِنِينَ اقْتَتَلُوا فَأَصْلِحُوا بَيْنَهُمَا ۖ فَإِن بَغَتْ إِحْدَاهُمَا عَلَى الْأُخْرَىٰ فَقَاتِلُوا الَّتِي تَبْغِي حَتَّىٰ تَفِيءَ إِلَىٰ أَمْرِ اللَّـهِ ۚفَإِن فَاءَتْ فَأَصْلِحُوا بَيْنَهُمَا بِالْعَدْلِ وَأَقْسِطُوا ۖ إِنَّ اللَّـهَ يُحِبُّ الْمُقْسِطِينَ إِنَّمَا الْمُؤْمِنُونَ إِخْوَةٌ فَأَصْلِحُوا بَيْنَ أَخَوَيْكُمْ

“Na mataifa [au makundi] mawili ya waumini yakipigana, basi suluhisheni baina yao. Lakini mojawapo likikandamiza jengine, basi lipigeni vitalile linalokandamiza mpaka lielemee kwenye amri ya Allaah. Likishaelemea, basi suluhisheni baina yao kwa uadilifu na fanyeni uadilifu. Hakika Allaah anapenda wafanyao uadilifu. Hakika si vyenginevyo waumini ni ndugu, hivyo basi suluhisheni baina ya ndugu zenu.” (49:09-10)

Hivyo, makundi mawili ya waislamu yenye kupigana vita ni ndugu zetu pamoja na kwamba haya ni maasi makubwa. Ikiwa Allaah (Ta´ala) amesema:

فَإِن تَابُوا وَأَقَامُوا الصَّلَاةَ وَآتَوُا الزَّكَاةَ فَإِخْوَانُكُمْ فِي الدِّينِ

“Wakitubu, wakasimamisha swalah na wakatoa zakaah, basi ni ndugu zenu katika dini.” (09:11) 

ina maana ya kwamba si ndugu yetu lau hatosimama kwa matendo haya. Hii ni dalili kutoka katika Qur-aan.

2 – Katika Sunnah. Sikiliza aliyopokea Muslim katika “as-Swahiyh” yake kupitia kwa Jaabir bin ´Abdillaah (Radhiya Allaahu ´anhumaa) ya kwamba Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Kati ya mtu na kati ya shirki na kufuru ni kuacha swalah.”[2]

Ukati unapelekea katika kupambanua na kutenganisha. Hii ina maana huyu si huyu.

“Kati ya mtu na kati ya shirki na kufuru ni kuacha swalah.”

Pale anapoiacha tu anakuwa mshirikina au kafiri.

Watunzi wa Sunan wamepekea kupitia kwa Buraydah bin al-Huswayn (Radhiya Allaahu ´anh) ya kwamba Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Ahadi iliyopo kati yetu sisi na wao ni swalah. Hivyo basi, yule mwenye kuiacha amekufuru.”[3]

Ahadi iliyopo kati yetu sisi na makafiri. Kitu chenye kupambanua kati yetu sisi na wao ni swalah. Hivyo mwenye kuiacha amekufuru. Amekuwa ni mmoja katika wao na si katika sisi. Maandiko haya yako mahala pake.

3 – Ama kuhusu waliyosema Maswahabah (Radhiya Allaah ´anhum), hebu sikiliza aliyosema ´Abdullaah bin Shaqiyq. Huyu ni mwanafunzi wa Maswahabah anayejulikana. Amesema (Rahimahu Allaah):

“Maswahabah wa Muhammad (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) hakuna kitu katika matendo walikuwa wakionelea kukiacha ni kufuru isipokuwa swalah.”[4]

Ishaaq bin Raahuuyah amepokea maafikiano ya Maswahabah juu ya ukafiri wa mwenye kuacha swalah. Huyu ni Imaam anayejulikana (Rahimahu Allaah). Vilevile baadhi ya wanachuoni wengine wamepokea hilo.Lau tutakadiria kuwa katika wao wako wenye kuona kinyume, wengi wao – wale wenye upeo wa kutoa hukumu za Kishari´ah katika wao – wanaonelea kuwa ni kafiri.

Hizi ni dalili kutoka katika Maneno ya Allaah, Mtume Wake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) na Maswahabah (Radhiya Allaahu ´anhum). Vilevile ´Umar bin al-Khattwaab (Radhiya Allaahu ´anh) amesema:

“Hana fungu katika Uislamu yule mwenye kuacha swalah.”

Ukanushaji huu ni wa aina. Hana dogo wala kubwa. Hana fungu katika Uislamu, si kubwa wala lidogo, yule mwenye kuacha swalah. Asiyekuwa na fungu lolote katika Uislamu, si kubwa wala lidogo, ina maana ya kuwa ni kafiri. Kuacha swalah kunapelekea katika mambo mengi, ya kidunia na Aakhirah.

Kuhusu mambo ya kidunia:

1 – Aitwe kuswali. Akiswali, sawa, la sivyo, auawe. Ni wajibu kwa mtawala afanye hivi. Wakipuuzilia mbali hili wataulizwa na Allaah (Ta´ala) pale wataposimama mbele Yake. Kila muislamu akiritadi kutoka katika Uislamu inatakiwa kumwita arejee. Akirudi ni sawa, la sivyo ni lazima auawe. Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Yule mwenye kubadilisha dini yake muueni”[5]

2 – Akichumbia asiozeshwe. Lau ataozeshwa basi ndoa hiyo ni batili. Mwanamke huyu si halali kwake. Anajamiana na mwanamke asiyekuwa halali kwake kwa kuwa ndoa si sahihi. Allaah (Ta´ala) amesema:

فَإِنْ عَلِمْتُمُوهُنَّ مُؤْمِنَاتٍ فَلَا تَرْجِعُوهُنَّ إِلَى الْكُفَّارِ ۖ لَا هُنَّ حِلٌّ لَّهُمْ وَلَا هُمْ يَحِلُّونَ لَهُنَّ

“Na mkiwatambua kuwa ni waumini basi msiwarejeshe [Makkah] kwa makafiri – wao si [wake]halali kwao [hao makafiri] na wala wao si [waume]halali kwao.” (60:10)

3 – Hana usimamizi wowote; si kwa watoto wake, dada zake wala muislamu yeyote. Kafiri hawezi kuwa msimamizi juu ya muislamu hata siku moja. Haijuzu hata akamuozesha msichana wake. Kwa mfano kuna mtu baada ya kuoa amepata wasichana. Kisha akaacha swalah. Haijuzu kwake kumuozesha msichana wake. Lau mtu atasema hapa kuna uzito kwa sababu kuko watu ambao wana wasichana na hawaswali. Tufanye nini? Jibu tunasema ikiwa haiwezekani kwa mtu akajiepusha kumuoa msichana huyu, amwendee kaka yake na msichana huyo au ami yake au Mahram yake mwingine – kwa kutegemea na mpangilio wa uwalii – amuozeshe kwa siri ili awe amemuoa msichana huyu kwa ndoa ilio sahihi. Ama baba yake kumuozesha ilihali ni kafiri aliyeritadi, ndoa haisihi. Lau atamuozesha mara elfu moja haikubaliwi.

4 – Lau ataacha swalah katikati ya ndoa, ndoa inavunjika. Kwa mfano mtu amemuoa mwanamke na wote wanaswali. Kisha baada ya hapo akaacha swalah. Tunasema ni wajibu kumtenganisha yeye na huyo mwanamke mpaka ataposwali. Tukiwatenganisha na akakaa eda [na ikaisha], haiwezekani akamrejea.  Lakini kabla ya eda kumalizika, akisilimu upya na akarudi katika Uislamu na kuanza kuswali tena, ataendelea kuwa mke wake. Ama eda ikimalizika, mwanamke huyo ametengana naye. Mwanamke huyo si halali kwake isipokuwa kwa kufunga tena ndoa nyingine mpya. Haya ndio maoni ya wanachuoni wengi.

Kuna wanachuoni wengine wanasema lau eda yake itaisha atabaki ni mwenye kuimiliki nafsi yake. Lakini hata hivyo lau atasilimu na kumtaka tena, atarejea kwake bila ya kufunga ndoa upya na ni sawa. Haya ndio maoni yenye nguvu kwa sababu yanasapotiwa na Sunnah. Faida ya eda ni kuwa mwanaume akisilimu basi mwanamke hana khiyari [ni lazima arudi kwake]. Lakini akisilimu baada ya eda, mwanamke ana khiyari; akitaka atarudi kwa mwanamme huyo na kama hataki hatorudi.

5 – Hana usimamizi kwa yeyote miongoni mwa wale waislamu anaowasimamia. Miongoni kwa masharti ya uongozi na usimamizini pamoja na uadilifu. Ukafiri sio uadilifu. Mwenye kuacha swalah hawi na usimamizi kwa yeyote miongoni mwa waja wa Allaah waislamu kwa hali yoyote. Hata ikiwa ni msichana wake haisihi kumfungisha ndoa kwa kuwa hana usimamizi wowote kwake.

6 – Haoshwi, havishwi sanda, haswaliwi na wala hazikwi pamoja na waislamu. Apelekwe nchi kavu na kuchimbiwa shimo na kutupwa ndani yake. Asichimbiwe kaburi kwa kuwa jitu hili halistahiki kupewa heshima yoyote.

Si halali kwa yeyote mwenye kufiwa na mtu na yeye anajua kuwa mtu huyo haswali, akamuosha, akamvisha sanda au kumpeleka kwa waislamu ili wamswalie. Akifanya hivo atakuwa amewafanyia ghushi waislamu. Allaah (Ta´ala) amemwambia Mtume Wake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) kuhusiana na wanafiki – hawa ni makafiri waliodhihirisha Uislamu:

وَلَا تُصَلِّ عَلَىٰ أَحَدٍ مِّنْهُم مَّاتَ أَبَدًا وَلَا تَقُمْ عَلَىٰ قَبْرِهِ ۖ إِنَّهُمْ كَفَرُوا بِاللَّـهِ

“Na wala usimswalie yeyote abadani miongoni mwao akifana wala usisimame kaburini kwake. Kwani hakika wao wamemkanusha Allaah.” (09:84)

Hii ni dalili yenye kuonyesha kuwa kufuru inapingana na kuswaliwa na kusimama mbele ya kaburi lake baada ya kuzikwa [ili kumuombea]. Allaah (Ta´ala) amesema tena:

مَا كَانَ لِلنَّبِيِّ وَالَّذِينَ آمَنُوا أَن يَسْتَغْفِرُوا لِلْمُشْرِكِينَ وَلَوْ كَانُوا أُولِي قُرْبَىٰ مِن بَعْدِ مَا تَبَيَّنَ لَهُمْ أَنَّهُمْ أَصْحَابُ الْجَحِيمِ

“Haimpasi Nabii na wale walioamini kuwaombea msamaha washirikina, japokuwa ni jamaa zao wa karibu, baada ya kuwabainikia kwamba wao ni watu wa Motoni.” (09:113)

Baadhi ya watu wanauliza kuhusiana na mtu anayetuhumiwa kuwa haswali na ameletwa ili aswaliwe baada ya kufa kwake na mtu huyo ana shaka kama amswalie au asimswalie. Jibu ni kuwa ikiwa shaka hii imejengwa juu ya msingi, basi utapotaka kumuombea du´aa sema: “Ee Allaah! Msamehe na umrehemu ikiwa kama alikuwa ni muumini.” Iseme namna hii. Kwa kusema hivo utakuwa ni mwenye kusalimika na shari yake.

Kuhusiana na mambo ya Aakhirah:

Baadhi ya mambo yanayopelekea katika kuacha swalah Aakhirah:

1 – Adhabu yenye kudumu ndani ya kaburi. Ataadhibiwa kama anavyoadhibiwa kafiri au zaidi yake.

2 – Siku ya Qiyaamah atafufuliwa na Fir´awn, Haamaan, Qaaruun, ´Ubayy bin Khalf.

3 – Ataingizwa Motoni na kudumishwa humo milele.

[1] al-Bukhaariy (48).

[2] Muslim (82).

[3] at-Tirmidhiy (2621).

[4] Imetangulia.

[5]al-Bukhaariy (6922).

  • Mhusika: Imaam Muhammad bin Swaalih bin ´Uthaymiyn
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Sharh Riyaadh-is-Swaalihiyn (01/402-408)
  • Imechapishwa: 04/06/2023