Pia imesihi kutoka kwake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) kwamba alisema kumwambia ´Aliy (Radhiya Allaahu ´anh):

“Naapa kwa Allaah kule Allaah kumwongoza mtu mmoja kupitia kwako ni bora kwako kuliko ngamia wekundu.”[1]

Kuna maafikiano juu ya usahihi wake.

Hii pia inajulisha juu ya fadhilah ya kulingania kwa Allaah na ile kheri kubwa inayopatikana ndani yake na kwamba anayelingania katika dini ya Allaah (Jalla wa ´Alaa) hupewa mfano wa thawabu za wale ambao Allaah amewaongoza kupitia mikono yake, ingawa watakuwa maelefu ya mamilioni. Mlinganizi unapewa mfano wa ujira wao. Hongera wewe ambaye unalingania kwa Allaah kwa kheri hii kubwa.

Hapa tunapata kufahamu kuwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) anapewa mfano wa thawabu za wafuasi wake. Ni neema kubwa iliyoje Mtume wetu (Swalla Allaahu ´alayhim wa sallam) kupewa mfano wa thawabu za wafuasi wake mpaka siku ya Qiyaamah. Kwa sababu amewafikishia ujumbe wa Allaah na akawajulisha kheri (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam).

Vivyo hivyo Mitume wengine (Swalla Allaahu ´alayhim wa sallam) wanalipwa mfano wa thawabu za wafuasi wao. Wewe pia ambaye ni mlinganizi katika zama zote unapewa mfano wa thawabu wa wafuasi wako na wale wanaokubali ulinganizi wako. Kwa hivyo tumia fursa ya kheri hii kubwa na ifanyie haraka.

[1] al-Bukhaariy (3009) na Muslim (2406).

  • Mhusika: Imaam ´Abdul-´Aziyz bin ´Abdillaah bin Baaz
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: ad-Da´wah ilaa Allaah wa Akhlaaq-id-Du´aah, uk. 24
  • Imechapishwa: 05/06/2023