Wenye kufuata uongofu wa Allaah na wasiofuata

Allaah (Tabaarak wa Ta´ala) amesema:

قُلْنَا اهْبِطُوا مِنْهَا جَمِيعًا ۖ فَإِمَّا يَأْتِيَنَّكُم مِّنِّي هُدًى فَمَن تَبِعَ هُدَايَ فَلَا خَوْفٌ عَلَيْهِمْ وَلَا هُمْ يَحْزَنُونَ

”Tukasema: ”Teremkeni kutoka humo nyote. Utakapokufikieni kutoka Kwangu uongofu, basi yeyote atakayefuata uongofu Wangu hakutokuwa na khofu juu yao wala hawatohuzunika.”[1]

Enyi watu! Wakati na zama zozote ambapo mtajiliwa na uongofu kutoka Kwangu. Uongofu wenyewe inahusiana na Mtume na Kitabu vinavyokuongozeni na yale yatayokufanyeni kuwa karibu Nami na kuwawekeni karibu na radhi Zangu.

هُدًى فَمَن تَبِعَ هُدَايَ

”… basi yeyote atakayefuata uongofu Wangu.”

Miongoni mwenu kwa njia ya kwamba akawaamini Mitume na Vitabu Vyangu na akafuata miongozo yavyo. Hayo yanakuwa kwa kusadikisha maelezo yote ya Mitume na ya Vitabu na kutekeleza maamrisho na kujiepusha na makatazo. Basi watu aina hiyo:

فَلَا خَوْفٌ عَلَيْهِمْ وَلَا هُمْ يَحْزَنُونَ

“Hakutokuwa na khofu juu yao wala hawatohuzunika.”

Katika Aayah nyingine imetajwa:

فَمَنِ اتَّبَعَ هُدَايَ فَلَا يَضِلُّ وَلَا يَشْقَى

”Basi atakayefuata uongofu Wangu hatopotea na wala kutaabika.”[2]

Kufuata uongofu kunapelekea katika mambo manne:

1- Kuondoshewa khofu na huzuni. Tofauti kati ya hayo mawili ni kwamba mabaya ni mambo yaliyokwishapita, ndipo kunazuka huzuni. Ama ikiwa mambo mabaya yanasubiriwa, ndipo kunazuka khofu.

2- Mambo mawili hayo amekanushiwa yule mtu anayefuata uongofu. Yakikanushwa basi kunapatikana kinyume chake ambacho ni amani kamilifu.

3- Vivyo hivyo kukanushwa upotofu na kutaabika kwa yule anayefuata uongofu. Yakikanushwa mawili hayo basi kunathibiti kinyume chavyo, nayo ni uongofu na furaha.

4- Yule mwenye kufuata uongofu basi anapata amani na furaha ya kidunia na ya Aakhirah na kunaondoka kwake mambo yote yenye kuchukiza, khofu, huzuni, upotofu na kutaabika. Mambo haya ni kinyume na yule asiyefuata uongofu, akakanusha na akakadhibisha Aayah Zake:

وَالَّذِينَ كَفَرُوا وَكَذَّبُوا بِآيَاتِنَا أُولَـٰئِكَ أَصْحَابُ النَّارِ ۖ هُمْ فِيهَا خَالِدُونَ

“Na wale waliokufuru na wakakadhibisha Aayah Zetu, basi hao ni watu wa Motoni wao humo ni wenye kudumu.”[3]

Bi maana watalazimiana nao kama ambavo rafiki anamlazimu mwenzie.

هُمْ فِيهَا خَالِدُونَ

“Wao humo ni wenye kudumu.”

Hawatotoka ndani yake, adhabu haitositishwa kwao na wala hawatonusuriwa.

Katika Aayah hizi na mfano wake majini na watu wamegawanyika kati ya wenye furaha na wala khasara. Pia faida nyingine ni kwamba zimetajwa sifa za pande zote mbili, matendo yanayopekea huko na kwamba majini ni kama watu inapokuja katika kupewa thawabu na kupewa adhabu kama ambavo ni mfano wao katika maamrisho na makatazo.

[1] 02:38

[2] 20:123

[3] 02:39

  • Mhusika: ´Allaamah ´Abdur-Rahmaan bin Naaswir as-Sa´diy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Taysiyr-ul-Kariym, uk. 40
  • Imechapishwa: 23/06/2020