Imaam an-Nawawiy (Rahimahu Allaah) amesema:

108 – Abu Swafwaan ´Abdullaah bin Busr al-Aslamiy (Radhiya Allaahu ´anh) ameeleza kuwa Mtume wa Allaah (Swalla Allahu ´alayhi wa sallam) amesema:

خَيرُ النَّاسِ مَنْ طَالَ عُمُرهُ، وَحَسُنَ عَمَلُهُ

“Mbora katika watu ni yule ambaye umri wake unakuwa mrefu na matendo yake yanakuwa mazuri.”

at-Tirmidhiy na amesema ni Hadiyth nzuri.

Hili ni kwa sababu kila ambavyo umri wa mwanadamu unarefuka katika kumtii Allaah ndivyo anavozidi kumkurubia Allaah na ngazi yake inazidi kupanda Aakhirah. Kila kitendo anachokifanya na huku umri wake unazidi kusonga mbele, basi kitendo hicho kinamkurubisha kwa Allaah (´Azza wa Jall). Mbora katika watu ni yule anayejaaliwa mambo haya mawili.

Kufanya umri ukawa mrefu ni jambo linalomiliki Allaah. Binadamu hamiliki hilo. Umri ni kitu kilichoko kwenye mikono ya Allaah (´Azza wa Jall). Lakini kuhusu kufanya matendo yakawa mazuri, hili binadamu analimiliki. Binadamu anaweza kufanya matendo yake yakawa mazuri. Kwa sababu Allaah (Ta´ala) amemtunukia akili, akateremsha Vitabu, akatuma Mitume, akabainisha njia na akamsimamishia hoja. Kila mtu anaweza kufanya matendo mema.

  • Mhusika: Imaam Muhammad bin Swaalih bin ´Uthaymiyn
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Sharh Riyaadh-is-Swaalihiyn (02/106-107)
  • Imechapishwa: 16/01/2024