Swali: Masuala ya kutibu uchawi kwa kutumia uchawi mwingine ni masuala yaliyo na tofauti na kwamba wanachuoni wa Hanaabilah wamejuzisha hilo na yule mwenye kuharamisha ameharamisha tu kwa ajili ya kufunga njia [zinazopelekea katika Shirki] na kwa ajili ya maslahi.

Jibu: Enyi ndugu! Tofauti haikufungwa. Tofauti hutokea. Lakini kinachozingatiwa ni yale yaliyo na dalili. Wanachuoni wakitofautiana hatutazami ile tofauti tu na kusema mambo haya mtu ana khiyari ya kuchukua lile analopenda. Haya ni maneno ya wale wanaofuata matamanio ya nafsi zao. Wanachukua katika maoni yale yanayoafikiana na matamanio yao.

Lililo la wajibu pale wanapotofautiana wanachuoni ni kurudisha tofauti zao katika dalili, katika Qur-aan na Sunnah. Yale yanayoafikiana na Qur-aan na Sunnah ndio haki, na yale yanayoenda kinyume navyo ni makosa. Hatukizingatii na wala hatukifuati ilihali kinaenda kinyume na dalili. Allaah (Ta´ala) Amesema:

يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا أَطِيعُوا اللَّـهَ وَأَطِيعُوا الرَّسُولَ وَأُولِي الْأَمْرِ مِنكُمْ ۖ فَإِن تَنَازَعْتُمْ فِي شَيْءٍ فَرُدُّوهُ إِلَى اللَّـهِ وَالرَّسُولِ إِن كُنتُمْ تُؤْمِنُونَ بِاللَّـهِ وَالْيَوْمِ الْآخِرِ ۚ ذَٰلِكَ خَيْرٌ وَأَحْسَنُ تَأْوِيلًا

“Enyi mlioamini! Mtiini Allaah na mtiini Mtume na wenye madaraka katika nyinyi. Mkizozana katika jambo, basi lirudisheni kwa Allaah na Mtume mkiwa mnamwamini Allaah na siku ya Mwisho. Hivyo ni njia bora na matokeo mazuri zaidi!” (04:59)

Hatubaki kwenye tofauti zetu na kusema kila mtu afuate ile kauli anayopenda katika kauli za wanachuoni. Haya ni maneno ya watu wa batili na wanaofuata matamanio yao. Badala yake tunatakiwa kusema magomvi yarudishwe katika Kitabu cha Allaah na Sunnah za Mtume Wake. Yale yenye kutolewa dalili na Kitabu na Sunnah ni haki, na yanayoenda kinyume navyo ni makosa. Tunampa udhuru mwenye nayo na wala hatuchukui [kauli yake].

Miongoni mwa hayo ni suala la kutibu uchawi. Tukikadiria kuwa kuna mwanachuoni aliyeenda kinyume tofauti yake ni makosa kwa kuwa inaenda kinyume na dalili kutoka katika Qur-aan na Sunnah. Hivyo ni makosa.

  • Mhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: at-Tafsiyr al-Mufasswal (18) http://www.alfawzan.af.org.sa/sites/default/files/tf–1427-11-13.mp3
  • Imechapishwa: 19/08/2020