Watu hawawezi kukunufaisha wala kukudhuru

Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) anamwambia Ibn ´Abbaas (Radhiya Allaahu ´anh):

“Tambua kuwa lau Ummah mzima utakusanyika ili kukunufaisha kwa chochote, basi hawawezi kukunufaisha isipokuwa kwa kitu ambacho Allaah amekuandikia.”[1]

Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amebainisha katika kipande hichi ya kwamba lau Ummah wote utakusanyika ili kukunufaisha kwa kitu, basi hawawezi kukunufaisha isipokuwa kwa kitu ambacho Allaah amekuandikia. Wakikunufaisha kwa kitu, basi utambue kuwa kimetoka kwa Allaah. Kwa sababu yeye ndiye amekiandika. Mtume hakusema kuwa hawawezi kukunufaisha. Bali amesema:

“… hawawezi kukunufaisha isipokuwa kwa kitu ambacho Allaah amekuandikia.”

Ni jambo lisilokuwa na shaka kuwa watu wananufaishana wao kwa wao na wanasaidiana wao kwa wao. Lakini hata hivyo yote haya ni miongoni mwa yale ambayo Allaah amemuandikia binadamu. Fadhilah zinamwendelea kwanza Allaah (´Azza wa Jall). Yeye ndiye amekutunukia aliyekunufaisha, akakutendea wema na akakuondolea matatizo. Vilevile kinyume chake:

“Lau Ummah mzima utakusanyika ili kukudhuru kwa chochote, basi hawawezi kukudhuru isipokuwa kwa kitu ambacho Allaah amekuandikia.”

Kuamini hili kunalazimisha mtu awe ameufungamanisha moyo kwa Mola Wake na kumtegemea. Asimjali yeyote. Kwa sababu anajua lau viumbe wote watakusanyika ili kumdhuru kwa kitu, basi hawawezi kumdhuru isipokuwa kwa kitu ambacho Allaah amemwandikia. Hapo ndipo afungamanishe matarajio yake kwa Allaah. Hata kama viumbe wote watamkusanyikia asibabaishwe nao.

Kwa ajili hii ndio maana tunaona kuna watu waliotangulia katika Ummah huu pindi walipomtegemea Allaah hawakudhurika na vitimbi vya wafanya vitimbi na wala hasadi za wenye kufanya hasadi:

وَإِن تَصْبِرُوا وَتَتَّقُوا لَا يَضُرُّكُمْ كَيْدُهُمْ شَيْئًا ۗ إِنَّ اللَّـهَ بِمَا يَعْمَلُونَ مُحِيطٌ 

“… na mkisubiri na mkamcha Allaah, basi haitokudhuruni chochote katika vitimbi vyao. Hakika Allaah kwa wayatendayo ni Mwenye kuyazunguka.” (03:120)

[1] al-Bukhaariy (59).

  • Mhusika: Imaam Muhammad bin Swaalih bin ´Uthaymiyn
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Sharh Riyaadh-is-Swaalihiyn (01/491-492)