Imaam an-Nawawiy (Rahimahu Allaah) amesema:

عَنْ أَبِي هُرَيْرَةَ (رضي الله عنه) عَنْ النَّبِيِّ صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ أَنَّهُ قَالَ: (إِنَّ اللَّهَ يَغَارُ وَغَيْرَةُ اللَّهِ أَنْ يَأْتِيَ الْمُؤْمِنُ مَا حَرَّمَ اللَّه) متفق عليه

64 – Abu Hurayrah (Radhiya Allaahu ´anh) amesimulia ya kwamba Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Allaah (Ta´ala) anaona wivu. Kuona Kwake wivu (Ta´ala) ni kule muumini kuyaendelea yale aliyomharamishia.”[1]

Wivu ni sifa ya kihakika iliyothibiti kwa Allaah (´Azza wa Jall). Lakini hata hivyo sio kama wivu wetu. Bali wivu wa Allaah ni mkubwa na ni mtukufu. Allaah kwa hekima Yake kuna mambo amewawajibishia viumbe, mengine akawaharamishia na mengine akawahalalishia. Yale ambayo amewahalalishia ni kherikatika dini na dunia yao na katika wakati wao wa sasa na wakati wao wa huko mbele.Aliyowaharamishia ni shari kwao katika dini na dunia yao na wakati wao wa sasa na wa huko mbele. Ikishakuwa Allaah amewaharamishia waja Wake mambo fulani, basi anaona haya (´Azza wa Jall) kwa mtu kuyaendea aliyoharamishia. Vipi basi mtu atayaendea yale aliyoharamisha Mola Wake na wakati Allaah (Subhaanahu wa Ta´ala) ameyaharamisha kwa ajili ya manufaa ya mja? Kwa upande wa Allaah (Subhaanahu wa Ta´ala) haimdhuru kitu kwa mwanadamu kumuasi. Lakini hata hivyo anaona haya. Binadamu anajua kuwa Allaah (Subhaanah) ni mwingi hekima na mwingi wa rehema. Allaah hamuharamishii mja Wake kitu kwa ajili ya kuwafanyia ubakhili. Bali ni kwa ajili ya maslahi yao. Kisha pamoja na yote hayo mtu anathubutu kumuasi Allaah (´Azza wa Jall). Hili ni khaswa kitu kinachoitwa uzinzi. Imethibiti kutoka kwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) ya kwamba amesema:

“Hakuna yeyote ana wivu kuliko Allaah kwa mja au mjakazi wake kuzini.”[2]

Kwa sababu uzinzi ni uchafu. Ndio maana Allaah akamharamishia mja Wake uzinzi na njia zote zinazopelekea katika uzinzi. Allaah (Ta´ala) amesema:

وَلَا تَقْرَبُوا الزِّنَىٰ ۖ إِنَّهُ كَانَ فَاحِشَةً وَسَاءَ سَبِيلًا

“Na wala msiikaribie zinaa. Hakika huo ni uchafu na ni njia mbaya kabisa.” (17:32)

Pale ambapo mja anafanya uzinzi, basi Allaah anaona wivu mkubwa kabisa kuliko Mahaarim zake wanavoona wivu.

Vilevile kitu ambacho ni kibaya zaidi ni liwati. Mwanaume kumwendea mwanaume mwenzake. Hili ni baya na baya zaidi. Ndio maana Allaah (Ta´ala) akalifanya kuwa ni uchafu zaidi kuliko hata uzinzi. Luutw aliwaambia watu wake:

أَتَأْتُونَ الْفَاحِشَةَ مَا سَبَقَكُم بِهَا مِنْ أَحَدٍ مِّنَ الْعَالَمِينَ 

“Je, mnafanya uchafu [wa liwati] ambao hajakutangulieni nao yeyote katika walimwengu?”(07:80)

Allaah amefanya liwati kuwa ni baya na kubwa zaidi kuliko uzinzi.

Vivyo hivyo kuiba, kunywa pombe na mambo mengine yote haya haramu Allaah anayaonea wivu. Lakini hata hivyo kuna ambayo ni khatari zaidi kuliko mengine kwa kiasi na jarima na madhara yalivo.

[1] al-Bukhaariy na Muslim

[2] al-Bukhaariy (5221) na Muslim (901).

  • Mhusika: Imaam Muhammad bin Swaalih bin ´Uthaymiyn
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Sharh Riyaadh-is-Swaalihiyn (01/496-498)
  • Imechapishwa: 21/06/2023