Swali: Kuna mtu anayedai elimu amejitokeza kwa watu ambaye anakanusha kutokeza kwa ad-Dajjaal na anasema lau ingelikuwa ni kweli…

Jibu: Enyi ndugu! Kuna watu wanaodai elimu wanaopinga alama za Qiyaamah. Wanapinga alama za Qiyaamah kwa sababu hawana elimu sahihi wala imani sahihi. Wamedanganyika na nafsi zao. Wanapinga mambo haya. Wanasema kuwa al-Masiyh ad-Dajjaal ni ibara inayotumiwa kuhusu kutokea kwa shari katika zama za mwisho. Ukweli wa mambo ni kwamba hakuna al-Masiyh ad-Dajjaal. Wanawaambia watu hivi.

Vilevile wanapinga kutokeza kwa Nabii ´Iysaa. Wanasema maana yake ni kutokeza kwa kheri na haki katika zama za mwisho. Ukweli wa mambo si kwamba Mtume ´Iysaa (´alayhis-Salaam) ndio atashuka. Wanawaambia watu namna hii. Wao wamejengea [´Aqiydah yao] juu ya akili zao. Watu hawa wanaitwa wanafalsafa. Hawaamini isipokuwa yale yanayokubaliana na akili zao. Yale yasiyokubaliana na akili zao wanayapinga. Watu hawa ni vijukuu vya Mu´tazilah. Mu´tazilah wao ndio watu wanaotegemea akili zao. Hategemei dalili za Qur-aan na Sunnah. Wanasema kuwa dalili za kiakili zinafidisha yakini wakati dalili za Qur-aan na Sunnah zinafidisha dhana. Wanaziita kuwa ni dalili zinazotia dhana. Wanaamini kuwa zinatia dhana kwa mujibu wao. Haya ndio madhehebu ya wapotevu. Wanapinga miujiza na karama za mawalii. Wanapinga kila kisichoingia katika akili zao.

Swali: Lau ingelikuwa ni kweli Allaah Angelitueleza naye katika Kitabu Chake…

Jibu: Haya ni maneno batili. Allaah Anaeleza katika Kitabu Chake na Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) anaeleza katika Sunnah zake. Allaah Amesema kuhusu Mtume:

وَمَا يَنطِقُ عَنِ الْهَوَىٰ

”Na wala hatamki kwa matamanio yake.” (53:03)

Watu hawa wanapinga Sunnah kama nilivyowaambia. Wanasema kuwa ni dalili zinazotia dhana na sio za yakini. Wanapinga Sunnah. Haya ni kutokana na madhehebu yao.

Wamefuata madhehebu haya wale wanaojiita kuwa ni ´wafikiriaji` wa leo. Watu hawa hawana elimu. Wanategemea fikira na akili zao. Watu hawa wapuuzwe kwa sababu wanapinga Sunnah. Wanasema kuwa wao wanaamini Qur-aan tu. Wanaitwa “Qur-aaniyyuun”. Hili ni kundi linalojulikana. Ni kundi potevu linalopinga Sunnah za Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Allaah (Jalla wa ´Allaa) amesema:

وَمَا آتَاكُمُ الرَّسُولُ فَخُذُوهُ وَمَا نَهَاكُمْ عَنْهُ فَانتَهُوا

“Na lolote lile analokupeni Mtume, basi lichukueni; na lolote lile analokukatazeni, basi acheni.” (59:07)

وَمَا يَنطِقُ عَنِ الْهَوَىٰ إِنْ هُوَ إِلَّا وَحْيٌ يُوحَىٰ

”Na wala hatamki kwa matamanio yake.” Hayo [ayasemayo] si chochote isipokuwa ni Wahy unaofunuliwa kwake.” (53:03-04)

Nyinyi mnasema kuwa mnaamini Qur-aan tu na hamwamini Sunnah. Allaah Ameamrisha Swalah ndani ya Qur-aan. Twambieni ni idadi ngapi za Swalah? Ni idadi ngapi za Rakaa? Ni sifa ipi ya Swalah? Tuwekeeni wazi haya. Mkikanusha Sunnah hamtoweza kufafanua kwa uwazi Ahkaam za Kishari´ah.

Vilevile kuhusu Zakaah Allaah Ameiamrisha katika Qur-aan. Ni nani aliyetubainishia nayo, kiasi chake na kiwango chake cha wajibu na masharti ya kuwajibika kwa Zakaah? Ni Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Yeye ndiye alitubainishia na kutufafanulia. Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) anafafanua yaliyokuja katika Qur-aan na anabainisha yaliyokuja katika Qur-aan:

وَأَنزَلْنَا إِلَيْكَ الذِّكْرَ لِتُبَيِّنَ لِلنَّاسِ مَا نُزِّلَ إِلَيْهِمْ

”Na Tumekuteremshia Ukumbusho [Qur-aan] ili uwabainishie watu [kwa Sunnah] yaliyoteremshwa kwao.” (16:44)

Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) ndiye mwenye kuibainisha Sunnah na kuifasiri Qur-aan na kuiweka wazi.

Watu hawa ni wapotevu, wapenda mjadala na washupavu. Kunapokuja majadiliano hoja zao zinaanguka na himdi zote ni za Allaah.

  • Mhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Sharh Kitaab Ahaadiyth-il-Fitnah http://www.alfawzan.af.org.sa/sites/default/files/hadist%20fitan-17-08-1435-01.mp3
  • Imechapishwa: 21/04/2015