Wakati ni kitu chenye thamani sana kwa binaadamu

Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alikuwa hakosekani na Maswahabah zake au familia yake. Ima utamkuta nyumbani na akisaidia kazi za nyumbani (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Akikamua kondoo maziwa, akishona nguo na viatu. Au utamkuta msiktini pamoja na Maswahabah zake. Au anaenda kumtembelea mgonjwa. Au anaenda kuwatembelea ndugu au mengineyo katika mambo hakupiti muda hata kidogo isipokuwa yumo katika kumtii Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Alikuwa akiuhifadhi muda wake. Hakuwa kama sisi tunapoteza wakati wetu.

Linaloshangaza ni kwamba hakuna kitu chenye thamani zaidi kwa mtu kama wakati lakini binaadamu amekifanya ni kitu duni sana. Allaah amesema:

حَتَّىٰ إِذَا جَاءَ أَحَدَهُمُ الْمَوْتُ قَالَ رَبِّ ارْجِعُونِ لَعَلِّي أَعْمَلُ صَالِحًا فِيمَا تَرَكْتُ

“Mpaka itakapomfikia mmoja wao mauti, atasema: “Mola wangu! Nirejeshe ili nikatende mema katika yale niliyoyaacha.” (23:99-100)

Nirudishe ili wakati hata mmoja usinipite. Hatosema nirudishe ili niburudike kwa mali, mke, kipando na kadhalika. Bali anasema:

لَعَلِّي أَعْمَلُ صَالِحًا فِيمَا تَرَكْتُ

“… ili nikatende mema katika yale niliyoyaacha.”

Wakati ulinipita na haukuninufaisha chochote.

Wakati ni kitu chenye thamani sana lakini sisi leo tumekifanya ni kitu duni sana.  Tunapoteza wakati mwingi kwa mambo yasiyokuwa na faida. Bali wakati mwingine tunapoteza wakati mwingi katika mambo yenye kutudhuru. Simlengi mtu maalum bali nazungumzia hali ya waislamu wote leo. Kwa masikitiko makubwa wamo wamejisahau, kujipumbaza na wameghafilika. Waislamu sio watu wenye misimamo katika mambo ya dini yao. Waislamu wengi wameghafilika na wamo katika kujipumbaza.

  • Mhusika: Imaam Muhammad bin Swaalih bin ´Uthaymiyn
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Sharh Riyaadh-is-Swaalihiyn (01/344-345)
  • Imechapishwa: 07/05/2023