16. Kushikamana barabara na Qur-aan

Allaah (Ta´ala) ameamrisha kushikamana na Qur-aan na akasema:

وَاعْتَصِمُوا بِحَبْلِ اللَّـهِ جَمِيعًا وَلَا تَفَرَّقُوا

”Na shikamaneni kwa kamba ya Allaah nyote pamoja wala msifarikiane.”

Kamba ya Allaah (Ta´ala) ni Kitabu Chake. Zayd bin Arqam amesimulia kwamba Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Zindukeni! Hakika mimi nimekuachieni vizito viwili ambapo kimoja wapo ni Kitabu cha Allaah,  nayo ndio kamba ya Allaah. Yule mwenye kukifuata ameongoka, na yule mwenye kukiacha amepotea.”[1]

Ibn Mas´uud (Radhiya Allaahu ´anh) amesema:

“Hakika njia hii ni yenye kuhudhuriwa na mashaytwaan waitao: “Ee mja wa Allaah, hii hapa njia!” Shikamaneni na njia ya Allaah. Kwani hakika njia ya Allaah ni Qur-aan.”[2]

Ibn Mas´uud (Radhiya Allaahu ´anh) amesema tena:

“Hakika Qur-aan hii ni ndio kamba ya Allaah, nuru, shifaa yenye kunufaisha, kinga kwa yule mwenye kushikamana nayo na uokozi kwa yule mwenye kuifuata.”[3]

al-Kirmaaniy amesema kuhusiana na maneno Yake Allaah (Ta´ala):

وَاعْتَصِمُوا بِحَبْلِ اللَّـهِ جَمِيعًا وَلَا تَفَرَّقُوا

”Na shikamaneni kwa kamba ya Allaah nyote pamoja wala msifarikiane.”[4]

 “Makusudio ya kamba ni Qur-aan na Sunnah… kwa sababu vyote viwili vinapelekea katika malengo, nazo ni thawabu, kama ambavo kamba inapelekea katika maji ndani ya kisima na mengineyo.”[5]

´Allaamah ´Aliyal-Qaariy amemkosea juu ya hilo na akasema:

“Kilichotangaa ni kwamba kamba inakusudiwa Qur-aan, kama ilivyopokelewa katika baadhi ya Hadiyth. Hata hivyo kushikamana na Qur-aan kunapelekea vilevile kushikamana na Sunnah kwa sababu Allaah (Ta´ala) amesema:

وَمَا آتَاكُمُ الرَّسُولُ فَخُذُوهُ وَمَا نَهَاكُمْ عَنْهُ فَانتَهُوا

”Kile alichokupeni Mtume basi kichukueni na kile alichokukatazeni basi kiacheni.”[6][7]

[1] Muslim (2408).

[2] ad-Daarimiy katika ”as-Sunan”.

[3] ad-Daarimiy katika ”as-Sunan”.

[4] 3:103

[5] al-Kawaakib ad-DaraariyfiySharhSwahiyh al-Bukhaariy (25/28).

[6] 59:7

[7]Mirqaat-ul-Mafaatiyh (1/365).

  • Mhusika: Shaykh ´Abdus-Salaam bin Barjas Aal ´Abdil-Kariym
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: al-Hujaj al-Qawiyyah ´alaa anna Wasaa-il-ad-Da´wah Tawqiyfiyyah, uk. 21-22
  • Imechapishwa: 08/05/2023