Vichenguzi vya swawm ya Ramadhaan ndio vichenguzi vya swawm nyenginezo

Swali: Vile vichenguzi vya swawm ya Ramadhaan ndio vilevile vinavyotumika juu ya funga ya nadhiri au swawm inayopendeza? Je, anapata dhambi ambaye anakula katika swawm ya nadhiri au swawm ya kujitolea? Je, analazimika kutoa kafara?

Jibu: Ndio, vichenguzi vya funga ya Ramadhaan ndio vivyo hivyo vinavyochengua swawm ya nadhiri, swawm ya kafara na swawm inayopendeza. Isipokuwa tu jambo moja; swawm inayopendeza inafaa kwa mtu akaianza wakati wa mchana tofauti na swawm ya faradhi ambayo ni lazima mtu aianze kabla ya kuchomoza kwa jua. Ni lazima ajizuie kabla ya kupambazuka alfajiri. Kuhusu swawm inayopendeza inajuzu kwa mtu akanuia kuanzia kitambo kidogo baada ya alfajiri muda wa kuwa ameamka na bado hajafanya kichenguzi chochote kama vile kula wala kitu kingine. Katika hali hiyo inafaa kwake kuanza swawm inayopendeza kuanzia wakati wa mchana. Kwa sababu Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) siku moja aliingia nyumbani kwa ´Aaishah ambapo akauliza:

“Mna chochote?” Wakasema: “Hapana.” Ndipo akasema: “Basi mimi nimefunga.”

Bi maana swawm inayopendeza inatofautiana na swawm ya faradhi.

Kuhusu vichenguzi vyengine kukiwemo kula, kunywa na jimaa zinalingana na swawm inayopendeza, swawm ya nadhiri, swawm ya Ramadhaan na swawm ya kafara zote zinaharibika pindi mtu anapokula, anapokunywa au anapofanya tendo la ndoa kwa makusudi. Lakini msahaulifu swawm yake haiharibiki. Akila, akanywa, akajamii au akafanya chuku kwa kusahau swawm yake ni sahihi. Tunachotaka kusema ni kwamba vichenguzi vya swawm wakati wa kusahau haviharibu swawm. Ni mamoja funga hiyo ni ya kujitolea, swawm ya kafara, swawm ya nadhiri au swawm ya Ramadhaan.

  • Mhusika: Imaam ´Abdul-´Aziyz bin ´Abdillaah bin Baaz
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: https://binbaz.org.sa/fatwas/14657/هل-مفسدات-صوم-رمضان-تفسد-صوم-النذر-والتطوع
  • Imechapishwa: 19/03/2023