Ubora wa kuchelewesha Tarawiyh mpaka mwisho wa usiku, kuirefusha na kuiswali Rak´ah 11

Swali: Tuna misikiti mingi ambayo baadhi inaswali Rak´ah nne, mingine inaswali Rak´ah ishirini, mingine inarefusha na mingine inafupisha. Ni msikiti upi ulio juu ya haki kwa mujibu wa alivokuwa akifanya Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam)?

Jibu: Mkiweza kuswali msikitini na mkaamka baada ya nusu ya usiku au theluthi ya mwisho ya usiku na mkaswali Rak´ah kumi na moja au Rak´ah kumi na tatu ni vyema, kama ilivyopokelewa katika Hadiyth ya ´Aaishah:

“Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alikuwa hazidishi, si katika Ramadhaan wala nyingine, juu ya Rak´ah kumi na moja.”

Kuna upokezi mwingine pia unaotaja Rak´ah kumi na tatu.

Napendekeza kuchelewesha swalah ya Tarawiyh mpaka nusu ya usiku au theluthi ya mwisho ya usiku. Kwani hakika Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Anayechelea kulala mwishoni mwa usiku basi aswali Witr mwanzoni mwake, na ambaye ana matumaini ya kuamka mwishoni mwa usiku basi aswali Witr mwishoni mwake. Kwani swalah ya mwishoni mwa usiku ni yenye kushuhudiwa.”

Ameipokea Muslim.

Imepokelewa pia kwamba wakati ´Umar alipomkuta Ka´b akiwaswalisha watu alisema:

“Uzuri wa uzushi uliyoje! Ingawa ile ambayo wanalala ikawapita ndio bora zaidi.”

Ikiwa wanaweza waende katika misikiti ambayo inatekeleza Sunnah na wanaamka nusu ya usiku au baada yake na wanawaswalisha watu Rak´ah kumi na moja na wanarefusha kwa kiasi wanavoweza, kwa sababu swalah ya usiku inapendeza na sio faradhi. Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Mimi huingia ndani ya swalah na nikakusudia kurefusha lakini nikafupisha kutokana na kilio ninachosikia cha mtoto kwa mama yake kwa kumuonea huruma.”

Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema kumwambia Mu´aadh:

“Hivi wewe ni mfitini, ee Mu´aadh?”

Bi maana kwa sababu ya kurefusha kwake katika swalah.

Vilevile amesema (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

“Anaposwali mmoja wenu peke yake, basi arefushe anavyotaka. Na anapowaswalisha watu basi akhafifishe. Kwani kati yao kuna mnyonge, mgonjwa na mwenye haja.”

Hili linahusu swalah ya faradhi. Kuhusu swalah ya kujitolea sio faradhi. Bali mtu anaswali anavyoweza na inafaa kwake kupumzika kwa Rak´ah za baada yake au kwenda nyumbani kwake. Akiweza kuswali nyumbani kwake ndio bora zaidi. Kwa sababu Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema baada ya kuwaswalisha watu Ramadhaan nyusiku mbili au tatu:

“Swalah bora ya mtu ni nyumbani kwake isipokuwa ya faradhi.”

Ingawa baadhi yao wanasema kuwa [msikitini] imekuwa ni Sunnah iliosisitizwa kwa sababu ya kwenda kinyume na Shiy´ah, kwa sababu wao wanaona kuwa swalah ya Tarawiyh ni Bid´ah. Hatukubaliani na Shiy´ah. Bali tunachotaka ni kwenda sambamba na Hadiyth ya Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Ikiwa mtu anachelea kulala au kushughulishwa nyumbani kwake na watoto wake au kitu kingine, basi tunamshauri kwenda kuswali msikitini.

  • Mhusika: ´Allaamah Muqbil bin Haadiy al-Waadi´iy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Fadhwaaih wa Naswaaih, uk. 85-86
  • Imechapishwa: 20/03/2024