Swali: Je, inafaa kuswali Tarawiyh kwa kuketi chini? Wakati imamu anapotaka kwenda katika Rukuu´, naleta Takbiyr kisha nasoma al-Faatihah na kurukuu pamoja na imamu. Nafanya hivo kwa sababu nashindwa kusimama Rak´ah yote na imamu kwa sababu nahisi kuchoka sana.

Jibu: Hapana vibaya kufanya hivo. Tarawiyh ni swalah ya kujitolea. Ni mamoja katika lile kumi la mwanzo au kumi la mwisho. Siku zote hizo ni zenye kupendeza. Kumi la mwisho watu wanaliita kuwa ni swalah ya kisimamo na ile swalah inayoswaliwa katika zile siku ishirini za mwanzo wanaita kuwa ni Tarawiyh. Zote huitwa kuwa ni kisimamo cha Ramadhaan na ni swalah ya kujitolea.

Hapana vibaya mtu akiswali kwa kuketi chini. Lakini anapata thawabu nusu. Akishindwa kwa sababu ya utuuzima au ni mnyonge na kusimama kunamtia uzito ambapo akakaa chini ni sawa. Akiketi chini mpaka kukapita sehemu ya kisomo kisha akasimama na kusoma hali ya kusimama halafu akarukuu pamoja na imamu ni sawa. Jambo ni lenye wasaa. Hata hivyo bora ni yeye kusimama mpaka asome kisomo [cha al-Faatihah] hali ya kusimama ikimsahilikia. Akikaa chini mpaka karibu na kurukuu na akasoma hali ya kuwa ameketi chini, kisha pindi imamu anapoleta Takbiyr na kutaka kurukuu, akasimama na kurukuu naye ni sawa pia.

  • Mhusika: Imaam ´Abdul-´Aziyz bin ´Abdillaah bin Baaz
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: https://binbaz.org.sa/fatwas/18506/حكم-ترك-القيام-في-صلاة-النافلة-كالتراويح-مثلا
  • Imechapishwa: 10/04/2023