Swali: Ni ipi hukumu akilazimika kuswali ambaye hakuvaa Hijaab au hakujisitiri kwa mujibu wa Shari´ah ya kiislamu kama kwa mfano kuonekana baadhi ya nywele za kichwani mwake au baadhi ya sehemu yake ya mguu kutokana na sababu miongoni mwa sababu?

Jibu: Mosi inapasa itambulike kwamba Hijaab ni lazima kwa mwanamke. Hivyo haijuzu kuiacha au kuichukulia wepesi. Ukifika wakati wa swalah na mwanamke wa kiislamu akawa si mwenye kuvaa Hijaab iliyokamilika au hakujisiti, jambo hili linahitajia upambanuzi:

1 – Ikiwa kutovaa Hijaab au kutojisitiri kunatokana na sababu za kutenzwa nguvu, basi hapo atatakiwa kuswali kutegemea na vile ilivyo hali yake. Swalah yake ni sahihi na hapati dhambi. Allaah (Ta´ala) amesema:

لَا يُكَلِّفُ اللَّـهُ نَفْسًا إِلَّا وُسْعَهَا

”Allaah hakalifishi nafsi yoyote isipokuwa kwa kadiri ya uwezo wake.”[1]

فَاتَّقُوا اللَّـهَ مَا اسْتَطَعْتُمْ

”Mcheni Allaah muwezavyo.”[2]

2 – Ikiwa kutovaa Hijaab au kutojisitiri kunatokana na mambo ya kikhiyari, kama vile kufata desturi, mila na mfano wa mambo hayo, ikiwa kutovaa Hijaab kumefupika juu ya uso na viganja vya mikono, basi swalah yake ni sahihi licha ya kuwa anapata dhambi ikiwa amefanya hivo mbele ya wanamme wa kando.

Ikiwa kujifunua na kutofunika mguu, mkono, nywele za kichwani na mfano wake, bais haitofaa kwake kuswali katika hali hiyo. Akiswali katika hali hiyo basi swalah yake ni batili. Hapo atakuwa ni mwenye kupata dhambi kwa pande mbili:

1 – Kujifunua kabisa ikiwa mbele yake wapo wanamme ambao sio Mahaarim zake.

2 – Kuingia kwake ndani ya swalah katika hali hiyo.

Lakini ikiwa mbele yake hakuna wanamme ambao sio Mahaarim, basi imependekezwa kwake kuswali hali ya kuacha uso wazi. Ni mwenye khiyari inapokuja katika viganja vya mikono; akitaka, atavifunika, na akitaka, ataviacha wazi kwa mujibu wa maoni sahihi zaidi ya wanazuoni. Ingawa bora zaidi ni kuvifunika.

[1] 02:286

[2] 64:16

  • Mhusika: Imaam ´Abdul-´Aziyz bin ´Abdillaah bin Baaz
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Majmuu´-ul-Fataawaa (10/407)
  • Imechapishwa: 28/09/2021