´Allaamah ´Abdur-Rahmaan bin Naaswir as-Sa´diy (rahimahullaah) amesema:

Swali 6: Mnasemaje kuhusu maneno ya Allaah na Qur-aan?

Jibu: Qur-aan ni maneno ya Allaah, imeteremshwa na haikuumbwa. Imeanza Kwake na itarudi Kwake.

Allaah ndiye mwenye kutamka kwayo kikweli, matamshi yake na maana yake. Hakuacha na hatoacha kuwa mwenye kuzungumza siku zote kwa anayoyataka na pale anapotaka.

Maneno yake hayaishi na wala hayatoisha.

MAELEZO

Maneno ya Allaah ni sifa miongoni mwa sifa Zake ambayo ameiegemeza Kwake pale aliposema:

وَإِنْ أَحَدٌ مِّنَ الْمُشْرِكِينَ اسْتَجَارَكَ فَأَجِرْهُ حَتَّىٰ يَسْمَعَ كَلَامَ اللَّـهِ

“Endapo mmoja katika washirikina atakuomba umlinde, basi mlinde mpaka aweze kusikia maneno ya Allaah.”[1]

Allaah (´Azza wa Jall) amesema:

قُل لَّوْ كَانَ الْبَحْرُ مِدَادًا لِّكَلِمَاتِ رَبِّي لَنَفِدَ الْبَحْرُ قَبْلَ أَن تَنفَدَ كَلِمَاتُ رَبِّي وَلَوْ جِئْنَا بِمِثْلِهِ مَدَدًا

“Sema: “Endapo bahari ingelikuwa ni wino wa [kuandika] maneno ya Mola wangu, basi ingelimalizika bahari kabla ya kumalizika maneno ya Mola wangu ijapo tungelileta mfano wake kujaza tena.”[2]

وَلَوْ أَنَّمَا فِي الْأَرْضِ مِن شَجَرَةٍ أَقْلَامٌ وَالْبَحْرُ يَمُدُّهُ مِن بَعْدِهِ سَبْعَةُ أَبْحُرٍ مَّا نَفِدَتْ كَلِمَاتُ اللَّـهِ ۗ إِنَّ اللَّـهَ عَزِيزٌ حَكِيمٌ

”Na lau kama miti yote iliyomo ardhini ingekuwa ni kalamu na bahari [ikawa wino], na ikaongezewa juu yake bahari zengine saba, basi yasingelimalizika maneno ya Allaah. Hakika Allaah ni Mwenye nguvu kabisa asiyeshindika,  Mwenye hekima ya yote.”[3]

Katika Aayah hizi Allaah (´Azza wa Jall) ameyaegemeza maneno Kwake Mwenyewe.

Ahl-us-Sunnah wanaamini kuwa Allaah anazungumza kwa maneno ya milele ambayo anayazungumza kutokana na mahitajio ya viumbe. Anaumba viumbe na anawafanya wengine kuaga dunia. Anampa nguvu mnyonge na anamnyongesha aliye na nguvu. Anampa umaskini tajiri na anamtajirisha masikini. Anampa utawala na kumpokonya nao amtakaye na kadhalika. Maneno ya Allaah ni yenye kuenea.

Qur-aan ni katika maneno ya Allaah. Ameiteremsha kwa Mtume Wake Muhammad (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) ili amwongoze kwayo yule ambaye Allaah anamtakia uongofu.

Ahl-us-Sunnah wal-Jamaa´ah wameafikiana kwamba yule mwenye kusema kuwa Qur-aan imeumbwa ni kafiri. al-Laalakaa´iy ametaja katika kitabu chake “Sharh Usuul I´tiqaad Ahl-is-Sunnah wal-Jamaa´ah” maneno ya wanachuoni wa zamani zaidi ya 500 kutoka nchi mbalimbali. Hilo linafahamisha kwamba kuna maafikiano katika suala hili.

Ahl-us-Sunnah wal-Jamaa´ah wanaamini kuwa maneno ya Allaah ni sifa miongoni mwa sifa Zake. Anazungumza pale anapotaka, namna anavotaka. Yule mwenye kusema kinyume na hivo ni mtu wa Bid´ah mpotevu. Kutokuzungumza ni upungufu kwa viumbe, sembuse Muumba. Vivyo hivyo kuzungumza kwa kuendelea pasi na kusimama ni aibu pia. Kwa ajili hiyo ndio maana Ahl-us-Sunnah wanasema kuwa Allaah anazungumza akitaka na pindi anapotaka. Allaah (Ta´ala)  amesema:

مَا يَأْتِيهِم مِّن ذِكْرٍ مِّن رَّبِّهِم مُّحْدَثٍ إِلَّا اسْتَمَعُوهُ وَهُمْ يَلْعَبُونَ

“Hauwafikii Ukumbusho wowote ule mpya kutoka kwa Mola wao isipokuwa huusikiliza kwa makini na huku wao wanacheza.”[4]

Ndio maana wakasema kuwa Allaah anazungumza kwa maneno ya milele na  anazungumza kutokana na yale ambayo waja wanayahitajia. Allaah amezungumza kwa Tawraat, akamwandikia nayo Muusa kwa mkono Wake na akamzungumzisha kwenye mlima. Kwa ajili hiyo amesema:

تِلْكَ الرُّسُلُ فَضَّلْنَا بَعْضَهُمْ عَلَىٰ بَعْضٍ ۘ مِّنْهُم مَّن كَلَّمَ اللَّـهُ ۖ وَرَفَعَ بَعْضَهُمْ دَرَجَاتٍ

“Hao ni Mitume, Tumewafadhilisha baadhi yao juu ya wengine, miongoni mwao kuna aliyezugumzishwa na Allaah, na akawapandisha baadhi yao vyeo.”[5]

Maneno ya mtunzi wa kitabu (Rahimahu Allaah):

“Imeanza Kwake na itarudi Kwake.”

Kusema kwamba Qur-aan imeanza kwa Allaah ina maana kwamba imetoka Kwake kwa sababu Yeye ndiye kazungumza kwayo. Kwa ajili hiyo baadhi ya Salaf wamesema:

“Hakuna yeyote awezaye kujikurubisha zaidi kwa Allaah kwa kitu zaidi ya kile kilichotoka Kwake.”

Bi maana Qur-aan.

Maneno ya mtunzi wa kitabu (Rahimahu Allaah):

“Hakuacha na hatoacha kuwa mwenye kuzungumza siku zote kwa anayoyataka na pale anapotaka. Maneno yake hayaishi na wala hayatoisha.”

Hiyo ina maana kwamba ni lazima kwetu kuamini kuwa Qur-aan ni maneno ya Allaah na kwamba haikuumbwa, kwamba itaendelea kubaki kati ya watu mpaka kikaribie Qiyaamah ili baadaye inyanyuliwe Kwake pindi itapoachwa kutendewa kazi – ulinzi unaombwa kutoka kwa Allaah. Haya ndio ambayo muislamu anatakiwa kuamini.

[1] 09:06

[2] 18:109

[3] 31:27

[4] 21:2

[5] 2:253

  • Mhusika: ´Allaamah Ahmad bin Yahyaa an-Najmiy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Fath Rabb-il-Bariyyaat ´alaa Kitaab Ahamm-il-Muhimmaat, uk. 36-39
  • Imechapishwa: 28/09/2021