Shaytwaan alivyowapendezeshea makhurafi misikiti ya makaburi

Ibn Taymiyyah (Rahimahu Allaah) amesema:

“Bali baadhi yao wanachukulia kufanya I´tikaaf humo [yaani kwenye misikiti ya makaburi au makaburi yaliyojengewa misikiti] imependekezwa zaidi kuliko kufanya I´tikaaf katika Masjid-ul-Haraam.”

Kwa kuwa shaytwaan hakati tamaa. Anampeleka binaadamu mpaka anahakikisha amemtoa katika ´ibaadah ya Allaah (´Azza wa Jall). Baadhi yao wamefikia mpaka kuonelea kuwa kufaya I´tikaaf kwenye misikiti ambayo ina makaburi ni bora kuliko kufanya I´tikaaf kwenye Masjid-ul-Haraam ambao Allaah ameufanya kuwa ni mahala pa kukusanyikia watu na pa amani. Msikiti ambao Allaah (Jalla wa ´Alaa) amesema juu yake kumwambia Ibraahiym:

أَن طَهِّرَا بَيْتِيَ لِلطَّائِفِينَ وَالْعَاكِفِينَ وَالرُّكَّعِ السُّجُودِ

“… Itakaseni Nyumba Yangu kwa wanaotufu na wanaokaa i’tikaaf, na wanaorukuu na kusujudu.” (02:125)

Swalah, I´tikaad, du´aa na ´ibaadah inakuwa kwenye misikiti na khaswa Masjid-ul-Haraam na Masjid-un-Nabawiy. Ama misikiti iliojengwa kwenye makaburi, hizi ni nyumba za shirki na ni nyumba za kumfanyia ´ibaadah asiyekuwa Allaah (´Azza wa Jall). Haijuzu kufanya I´tikaaf ndani yake, bali haijuzu kuswali ndani yake hata kama mwenye kuswali anaswali kwa ajili ya Allaah. Kwa kuwa amekatazwa kuswali kwenye makaburi na kuomba du´aa kwenye makaburi.

Anaendelea kusema (Rahimahu Allaah):

“Bali heshima ya msikiti huo uliojengwa kwenye kaburi – jambo ambalo limeharamisha Allaah na Mtume Wake – ni kubwa kwa waabudia makaburi kuliko Nyumba ya Allaah ambayo Allaah ameamrisha itukuzwe na litajwe humo jina Lake na umejengwa juu ya msingi wa kumcha Allaah tangu siku ya mwanzo.”

Waabudia makaburi wanaiheshimu Misikiti iliojengwa kwenye makaburi zaidi kuliko wanavyouheshimu Masjid-ul-Haraam na misikiti iliojengwa juu ya Tawhiyd. Kwa ajili hiyo utaona kuwa Misikiti isiokuwa na kaburi ndani haina hadhi yoyote kwao na haiswalii. Nyoyo zao zimefungamana na Misikiti iliojengwa kwenye makaburi, wanaitegemea na kuiadhimisha.

  • Mhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Sharh Iqtidhwaa’-is-Swiraat al-Mustaqiym (03) http://www.alfawzan.af.org.sa/node/2247
  • Imechapishwa: 05/05/2015