Kuwazika watu wema misikitini

Ibn Taymiyyah (Rahimahu Allaah) amesema:

“Amebainisha (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) kwamba kule kujenga tu msikitini juu yake [kaburi] ni jambo limekatazwa kwa maafikiano ya Ummah na ni haramu kwa dalili za Sunnah, vipi mtu akiongezea juu ya kubaki hapo kwa muda mrefu utafikiri ni msikiti mtakatifu wa Makkah!”

Kule kujenga tu Msikiti kwenye kaburi, hata kama mtu hakufungamana na hilo kaburi, imekatazwa. Kwa kuwa hii ni njia inayopelekea katika shirki. Siku zitavyopita na ujinga kuzidi kuenea nyoyo za watu zitafungamana na kaburi hili ambalo limeingizwa msikitini au msikiti umejengwa juu yake na waseme lau mtu huyu angelikuwa hadhuru na kunufaisha na hana mambo maalum basi asingelijengewa Msikiti huu kwenye kaburi lake. Allaah (Jalla wa ´Alaa) Amesema:

وَأَنَّ الْمَسَاجِدَ لِلَّـهِ فَلَا تَدْعُوا مَعَ اللَّـهِ أَحَدًا

“Na kwamba misikiti ni [kwa ajili] ya Allaah, hivyo basi msiombe yeyote pamoja na Allaah.” (72:18)

Misikiti inatakiwa kuwa kwa ajili ya Allaah na kusiwe ndani yake kushirikishwa na wengine. Anasema (Ta´ala):

فِي بُيُوتٍ أَذِنَ اللَّـهُ أَن تُرْفَعَ وَيُذْكَرَ فِيهَا اسْمُهُ يُسَبِّحُ لَهُ فِيهَا بِالْغُدُوِّ وَالْآصَالِ رِجَالٌ لَّا تُلْهِيهِمْ تِجَارَةٌ وَلَا بَيْعٌ عَن ذِكْرِ اللَّـهِ وَإِقَامِ الصَّلَاةِ وَإِيتَاءِ الزَّكَاةِ

“Katika nyumba [misikiti] ameidhinisha Allaah zitukuzwe na litajwe humo jina Lake, humsabihi humo asubuhi na jioni. Wanaume haiwashughulishi biashara wala uuzaji na kumdhukuru Allaah na [hayawashughulishi pia na] kusimamisha swalah na [wala] kutoa zakaah.” (24:36-37)

إِنَّمَا يَعْمُرُ مَسَاجِدَ اللَّـهِ مَنْ آمَنَ بِاللَّـهِ وَالْيَوْمِ الْآخِرِ وَأَقَامَ الصَّلَاةَ وَآتَى الزَّكَاةَ وَلَمْ يَخْشَ إِلَّا اللَّـهَ ۖ فَعَسَىٰ أُولَـٰئِكَ أَن يَكُونُوا مِنَ الْمُهْتَدِينَ

“Hakika si venginevyo wanaoamirisha misikiti ya Allaah ni [wale] wanaomwamini Allaah na siku ya Mwisho na wakasimamisha swalah na wakatoa zakaah na hawamkhofu yeyote isipokuwa Allaah. Basi hakika hao wakawa miongoni mwa waliohidika.” (09:18)

Misikiti imejengwa kwa lengo hili, nalo ni kumpwekesha Allaah (Subhaanahu wa Ta´ala), kumuabudu ndani yake, kubaki humo kwa muda mrefu kwa kumtii Allaah na kuupenda. I´tikaaf ni ´ibaadah, nako ni kule kushikamana na msikiti kwa kumtii Allaah (Subhaanahu wa Ta´ala). Vivyo hivyo swalah, Dhikr, kusoma Qur-aan, kutafuta elimu na mambo mengineyo ambayo yanahusiana na msikiti. Msikiti ni nyumba ya ´ibaadah.Kumwabudu Allaah hali ya kuwa hana mshirika. Kusichanganywe ndani yake kuabudu asiyekuwa Yeye katika maiti, mawalii na watu wema. Kwa ajili hii ndio maana Amesema:

وَأَنَّ الْمَسَاجِدَ لِلَّـهِ فَلَا تَدْعُوا مَعَ اللَّـهِ أَحَدًا

“Na kwamba misikiti ni [kwa ajili] ya Allaah, hivyo basi msiombe yeyote pamoja na Allaah.”

Msikiti ukijengwa kwenye kaburi, ikiwa kaburi ndilo lililotangulia na msikiti ulikuja nyuma, basi msikiti ubomolewe na kubaki kaburi tu. Ama ikiwa ni kinyume chake, bi maana msikiti ndio ulitangulia na kaburi likaingizwa ndani yake baada ya hapo, ni wajibu kuliondosha hilo kaburi na kubakiza msikiti tu.

  • Mhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Sharh Iqtidhwaa’-is-Swiraat al-Mustaqiym (05) http://www.alfawzan.af.org.sa/node/2247
  • Imechapishwa: 05/05/2015