Shari´ah ya Muhammad imefuta Shari´ah za Mitume wote waliokuwa kabla yake

Ibn Taymiyyah (Rahimahu Allaah) amesema:

““Ilipokuwa asli ya dini ya Kiislamu ni moja na Shari´ah yake ndio yenye kutofautiana, ndipo Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akasema katika Hadiyth Swahiyh:

“Sisi Mitume dini yetu ni moja.”

Allaah (Jalla wa ´Alaa) anasema:

إِنَّ الدِّينَ عِندَ اللَّـهِ الْإِسْلَامُ

“Hakika dini mbele ya Allaah ni Uislamu.” (03:19)

وَمَن يَبْتَغِ غَيْرَ الْإِسْلَامِ دِينًا فَلَن يُقْبَلَ مِنْهُ وَهُوَ فِي الْآخِرَةِ مِنَ الْخَاسِرِينَ

“Na yeyote anayetaka dini isiyokuwa ya Kiislamu basi haitokubaliwa kwake; naye katika Aakhirah atakuwa miongoni mwa waliokhasirika.” (03:85)

Uislamu – kama jinsi Shaykh alivyoufasiri mahali kwengine – maana yake ni kujisalimisha kwa Allaah kwa kumpwekesha, kunyenyekea kwake kwa utiifu na kujiweka mbali na shirki na washirikina.

Kwa maana hii Uislamu unakuwa ni dini ya Mitume wote. Anasema (Ta´ala):

وَمَا أَرْسَلْنَا مِن قَبْلِكَ مِن رَّسُولٍ إِلَّا نُوحِي إِلَيْهِ أَنَّهُ لَا إِلَـٰهَ إِلَّا أَنَا فَاعْبُدُونِ

“Hatukutuma kabla yako Mtume yeyote isipokuwa Tulimfunulia Wahy ya kwamba: “Hakika hakuna mola mwabudiwa wa haki isipokuwa Mimi, hivyo basi Niabuduni.” (21:25)

وَلَقَدْ بَعَثْنَا فِي كُلِّ أُمَّةٍ رَّسُولًا أَنِ اعْبُدُوا اللَّـهَ وَاجْتَنِبُوا الطَّاغُوتَ ۖفَمِنْهُم مَّنْ هَدَى اللَّـهُ وَمِنْهُم مَّنْ حَقَّتْ عَلَيْهِ الضَّلَالَةُ

“Na kwa hakika Tulituma katika kila ummah Mtume [awaamrishe watu wake] kwamba: “Mwabuduni Allaah na jiepusheni na  waungu wa batili.” (16:36)

Hii ndio dini ya Mitume, bi maana kumuabudu Allaah na kujiepushe na kumuabudu asiyekuwa Yeye.

Kumuabudu Allaah inakuwa kwa yale Aliyoyaweka katika Shari´ah, Aliyoyawekea waja Wake, kila wakati ´ibaadah yao maalum. Shari´ah ya Mitume ni kama Alivyosema (Jalla wa ´Alaa):

لِكُلٍّ جَعَلْنَا مِنكُمْ شِرْعَةً وَمِنْهَاجًا

“Kwa kila [ummah] katika nyinyi Tumeujaalia Shari´ah na mfumo [wao].” (05:48)

Shari´ah ya Mitume inatofautiana kutegemea na wakati wenyewe, kwa kiasi cha yale ambayo watu wanayahitajia katika wakati wao. Baada ya hapo Allaah Anafuta yale Anayoyataka na Analeta Shari´ah nyingine inayoendana na kizazi cha sasa. Hali iliendelea kuwa hivo mpaka wakati Alipomtuma Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam), Shari´ah yake ikawa imekhitimisha Shari´ah na nyujumbe nyingine zote zilizokuwepo hapo kabla, Uislamu ukawa mmoja kwa kumfuata yeye (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Shari´ah yake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) ndio yenye kubaki na yenye kurithi zingine. Shari´ah zilizotangulia zimeisha kwa kutumwa kwake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam), isipokuwa katika ´Aqiydah na Tawhiyd ni zenye kuendelea. Kwa ajili hii amesema (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

“Sisi Mitume dini yetu ni moja.”

yaani ´Aqiydah yetu ni moja. Ama Shari´ah zinazohusiana na utenda kazi unatofautiana kwa kiasi cha mahitajio na manufaa ya watu. Lakini hata hivyo baada ya kutumwa kwake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) Allaah Amewaamrisha viumbe wote kumfuata yeye. Kwa kuwa kila Mtume hapo kabla alikuwa akitumwa kwa watu maalum tofauti na Mtume huyu, yeye ametumwa kwa watu wote. Kwa hivyo Shari´ah yake ndio ikawa yenye kubaki pekee na inayotumika katika kila zama na mahala mpaka Qiyaamah itaposimama.

  • Mhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: http://www.alfawzan.af.org.sa/sites/default/files/ektda–1430-4-15.mp3
  • Imechapishwa: 05/05/2015