Shaka juu ya kupambazuka alfajiri

Swali: Ni ipi hukumu ya mwenye shaka ya kuchomoza kwa alfajiri? Je, inafaa kwake kula na kunywa au ajizuie mpaka awe na uhakika kuwa imechomoza au atendee kazi shaka?

Jibu: Allaah (Subhaanahu wa Ta´ala) amesema:

فَالْآنَ بَاشِرُوهُنَّ وَابْتَغُوا مَا كَتَبَ اللَّـهُ لَكُمْ ۚ وَكُلُوا وَاشْرَبُوا حَتَّىٰ يَتَبَيَّنَ لَكُمُ الْخَيْطُ الْأَبْيَضُ مِنَ الْخَيْطِ الْأَسْوَدِ مِنَ الْفَجْرِ

“Basi sasa changanyikeni nao [waingilieni] na tafuteni Aliyokuandikieni Allaah kwenu. Kuleni na kunyweni mpaka ubainike kwenu weupe wa alfajiri katika weusi wa usiku.”[1]

Akiwa na uhakika ya kuchomoza kwa alfajiri basi itaharamika kwake kula na kunywa na italazimika kwake kujizuilia. Asipokuwa na uhakika na kupambazuka alfajiri na akabaki juu ya shaka kama imeingia au haijaingia, basi tahadhari zaidi kwake ni yeye kujizuilia kula na kunywa. Atafanya hivo kwa minajili ya kuchukua tahadhari na kujiepusha na mambo yenye utata. Amesema (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

”Kiache kile chenye kukutia shaka na kiendee kile kisichokutia shaka.”

“Yeyote mwenye kuyaepuka mambo yenye utata basi ameitakasa dini na heshima yake.”

Bora ni yeye kujizuilia na kuacha kula na kunywa muda wa kuwa anakhofu kuwa alfajiri imekwishachomoza.

[1] 02:187

  • Mhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Majmuu´-ul-Fataawaa (02/394)
  • Imechapishwa: 15/03/2022