03. Wakati ambapo watu wa batili hupata uchangamfu

Watu wa batili hufanya mambo yao na kupata uchangamfu pindi elimu inapotea, kudhihiri kwa ujinga na jamii kukosa wale wanaonukuu yale yaliyosemwa na Allaah na Mtume Wake. Kipindi hicho ndio huwasumbua wengine na hupata uchangamfu katika batili yao kwa sababu ya kutokuweko wale wanaowaogopa katika watu wa haki, waumini na watambuzi.

Allaah katika baadhi ya maeneo ndani ya Kitabu Chake ametaja kila kitu kwa njia ya ujumla na katika baadhi ya maeneo mengine ametaja kwa upambanuzi. Amsema (´Azza wa Jall):

وَنَزَّلْنَا عَلَيْكَ الْكِتَابَ تِبْيَانًا لِّكُلِّ شَيْءٍ

“Na Tumekuteremshia Kitabu hali ya kuwa ni chenye kubainisha kila kitu.”[1]

Haya ni maneno ya Mwingi wa hekima ambaye hakuna mkweli zaidi kumliko:

وَمَنْ أَصْدَقُ مِنَ اللَّـهِ قِيلًا

“Na nani mkweli zaidi kwa kauli kuliko Allaah?”[2]

Ameweka wazi (Subhaanah) katika maneno Yake:

وَنَزَّلْنَا عَلَيْكَ الْكِتَابَ تِبْيَانًا لِّكُلِّ شَيْءٍ وَهُدًى وَرَحْمَةً وَبُشْرَىٰ لِلْمُسْلِمِينَ

“Tumekuteremshia Kitabu hali ya kuwa ni chenye kubainisha kila kitu na ni mwongozo na rehema na bishara kwa waislamu.”[3]

ya kwamba, licha ya kuwa ni chenye kubainisha kila kitu, ndani yake pia mna uongofu, rehema na bishara njema. Ni chenye kubainisha haki, kuweka wazi njia yake, mfumo wake na kulingania kwacho kwa ibara zilizo wazi na bainifu zaidi. Pamoja na hayo ni uongofu kwa walimwengu katika kila wanachokihitajia kuhusu utajo wa Mola wao, kuelekea yale yanayomridhisha na kujitenga mbali na yale yanayomkasirisha. Vilevile kinawabainisha njia ya uokozi na njia ya kufaulu ingawa pia ni rehema katika ubainifu na maelekezo yake, mwongozo, wema na bishara njema. Qur-aan inazihakikishia nyoyo kutokana na yale inayoweka wazi katika ukweli na kuelekeza kwayo katika utambuzi ambavyo hunyenyekewa na mioyo, nafsi kupata utulivu kwavyo na vifua hufunguka kwa kuwa kwake wazi. Amesema (Subhaanah):

يَا أَيُّهَا النَّاسُ قَدْ جَاءَتْكُم مَّوْعِظَةٌ مِّن رَّبِّكُمْ وَشِفَاءٌ لِّمَا فِي الصُّدُورِ وَهُدًى وَرَحْمَةٌ لِّلْمُؤْمِنِينَ

“Enyi watu! Hakika yamekujieni mawaidha kutoka kwa Mola wenu na shifaa ya yale yote yaliyomo vifuani, na mwongozo na Rahmah kwa waumini.”[4]

يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا أَطِيعُوا اللَّـهَ وَأَطِيعُوا الرَّسُولَ وَأُولِي الْأَمْرِ مِنكُمْ ۖ فَإِن تَنَازَعْتُمْ فِي شَيْءٍ فَرُدُّوهُ إِلَى اللَّـهِ وَالرَّسُولِ إِن كُنتُمْ تُؤْمِنُونَ بِاللَّـهِ وَالْيَوْمِ الْآخِرِ ۚ ذَٰلِكَ خَيْرٌ وَأَحْسَنُ تَأْوِيلًا

“Enyi walioamini! Mtiini Allaah na mtiini Mtume na wenye madaraka katika nyinyi; mkizozana juu ya jambo, basi lirudisheni kwa Allaah na Mtume mkiwa mnamuamini Allaah na siku ya Mwisho. Hivyo ni bora na matokeo mazuri kabisa.”[5]

وَمَا اخْتَلَفْتُمْ فِيهِ مِن شَيْءٍ فَحُكْمُهُ إِلَى اللَّـهِ ۚ ذَٰلِكُمُ اللَّـهُ رَبِّي عَلَيْهِ تَوَكَّلْتُ وَإِلَيْهِ أُنِيبُ

”Jambo lolote lile mlilokhitilafiana kwalo, basi hukumu yake ni kwa Allaah. Huyo ndiye Allaah, Mola wangu, Kwake nategemea na Kwake narejea kutubia.”[6]

[1] 16:89

[2] 04:122

[3] 16:89

[4] 10:57

[5] 04:59

[6] 42:10

  • Mhusika: Imaam ´Abdul-´Aziyz bin ´Abdillaah bin Baaz
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Ahamiyyat-ul-´Ilm https://binbaz.org.sa/discussions/33/اهمية-العلم-في-محاربة-الافكار-الهدامة
  • Imechapishwa: 15/03/2022