104- Baada ya kumaliza kumzika kumesuniwa mambo yafuatayo:

1- Kaburi linyanyuliwa kidogo juu ya ardhi kiasi cha shibiri moja na wala lisisawazishwe na ardhi. Lengo ni ili lipambanuke na hivyo lihifadhike na lisitwezwe Hilo ni kutokana na Hadiyth ya Jaabir (Radhiya Allaahu ´anh) isemayo:

“Kwamba Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alifanyiwa mwanandani na kukazibiwa juu yake matofali. Kaburi lake likanyanyuliwa juu ya ardhi kiasi cha shibiri moja.”

Ameipokea Ibn Hibbaan katika “as-Swahiyh” yake (2160) na al-Bayhaqiy (03/410) kwa cheni ya wapokezi nzuri.

Inayo Hadiyth nyingine ambayo kwenye cheni ya wapokezi wake yupo Swahabah anayekosekana kutoka kwa Swaalih bin Abiy al-Akhdhwar ambaye amesema:

“Nililiona kaburi la Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) lilikuwa shibiri moja au takriban shibiri moja.”

Ameipokea Abu Daawuud katika “al-Maraasiyl” (421). Swaalih huyu amedhoofishwa na Yahyaa bin al-Qattwaan na wengineo.

Isitoshe haya yanatiliwa nguvu na yale makatazo yatayokuja ya kuzidisha juu ya ule mchanga uliotoka katika kaburi. Ni jambo linalojulikana kwamba baada ya kuzika kunabaki juu ya kaburi ule mchanga uliotoka kwenye mwanandani ambamo umewekwa mwili wa maiti. Kiwango hicho kinalingana takriban na ule mchanga uliotajwa katika Hadiyth.

ash-Shaafi´iy amesema katika “al-Umm” (01/245-246) yale ambayo ufupisho wake ni kama ifuatavyo:

“Napendelea kusizidishwe ndani ya kaburi mchanga mwingine usiotoka humo. Kukizidishwa basi litanyanyuka sana. Napendelea linyanyuliwe kiasi cha shibiri moja au mfano wake.”

an-Nawawiy katika “al-Majmuu´” (05/296) amenakili kuafikiana kwa wafuasi wa madhehebu ya ash-Shaafi´iy juu ya kupendekeza kunyanyuliwa kwa kiwango kilichotajwa.

2- Linyanyuliwe katika mfumo wa tuta. Hilo ni kutokana na Hadiyth ya Sufyaan at-Tammaar ambaye amesema:

“Nililiona kaburi la Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) [na kaburi la Abu Bakr na ´Umar] limefanywa kwa mfumo wa tuta.”

Ameipokea al-Bukhaariy (03/198-199), al-Bayhaqiy (04/03) na ameipokea Ibn Abiy Shaybah na Abu Nu´aym katika “al-Mustakhraj” kama ilivyo katika “at-Talkhiysw” na ziada ni za wawili hao.

Hayo hayapingani na yale yaliyopokelewa kutoka kwa al-Qaasim ambaye amesema:

“Niliingia kwa ´Aaishah ambapo nikasema: “Ee mamangu! Nifungulie kaburi la Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) na marafiki zake wawili (Radhiya Allaahu ´anhumaa). Akaniwekea wazi makaburi hayo matatu ambapo hayakuwa yameinuka wala hayakuambatana na ardhi. Yalikuwa yamenyanyuliwa kidogo kwa mchanga wa changarawe nyekundu na pasi na kujengewa.”

Ameipokea Abu Daawuud (02/70), al-Haakim (01/369), al-Bayhaqiy (04/03) na Ibn Hazm (05/134) wamepokea kutoka kwake kupitia kwa njia ya ´Amr bin ´Uthmaan bin Haaniy´ kutoka kwa al-Qaasim.

al-Haakim amesema:

“Ni yenye cheni ya wapokezi Swahiyh.”

na adh-Dhahabiy ameafikiana naye. Lakini al-Bayhaqiy amesema:

“Ni Swahiyh zaidi kuliko Hadiyth ya Sufyaan at-Tammaar. Ibn-ut-Turkumaaniy amemraddi na kusema:

“Hilo ni kinyume na istilahi ya watu wenye fani hii. Bali Hadiyth ya at-Tammaar ni Swahiyh zaidi kwa sababu imesumuliwa katika “Swahiyh-ul-Bukhaariy” na Hadiyth ya al-Qaasim haijasimuliwa popote kutoka katika vitabu ambavyo ni Swahiyh.”

Radd hii haitoshelezi. Pengine cheni ya wapokezi wa Hadiyth inayotafautiana na Hadiyth ya al-Bukhaariy ikawa ni Swahiyh na yenye nguvu zaidi kuliko cheni ya wapokezi wa al-Bukhaariy. Kwa hivyo hakutimii kuitilia nguvu Haidyth ya at-Tammaar isipokuwa mpaka kwa kubainisha kasoro ya Hadiyth ya al-Qaasim au angalau kwa uchache kubainisha kuwa kiusahihi iko chini zaidi, jambo ambalo ndio uhalisia wa mambo hapa. Kasoro yake ni ´Amr bin ´Uthmaan bin Haaniy´, ambaye amesitiriwa. Hayo yamesemwa na al-Haafidhw katika “at-Taqriyb”. Hakuna yeyote aliyemfanya kuwa mwaminifu. Kwa hiyo kule al-Haakim kufanya Hadiyth yake kuwa Swahiyh ni katika kuchukulia kwake mambo wepesi kama inavotambulika. Aidha kule adh-Dhahabiy kumwigiliza ni katika yale makosa yake mengi yanayotambulika kwa yule mwenye kufuatilia maneno yake katika “Talkhiysw-ul-Mustadrak”.

Isitoshe endapo itasihi basi si yenye kupingana na Hadiyth ya at-Tammaar. Kwa sababu maneno yake (مّبْطوح) hayana maana ya (مُسَطّحٌ). Bali ule mchanga uliotoka ndani asili yake ulikuwa changarawe. Hayo yanapatikana katika “an-Nihaayah”. Hilo liko wazi katika maelezo yenyewe:

“Yalikuwa yamenyanyuliwa kidogo kwa mchanga wa changarawe nyekundu na pasi na kujengewa.”

Haya hayapingani na kufanywa kama tuta. Kwa ajili hiyo Ibn-ul-Qayyim amekusanya kati ya Hadiyth hizo mbili na akasema katika “az-Zaad”:

“Kaburi lake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) lilifanywa kama tuta na kutandazwa kwa mchanga ambao ni changarawe nyekundu. Halikujengewa wala halikufanywa udongo. Vivyo hivyo ndivo yalivokuwa makaburi ya marafiki zake wawili.”

3- Kuweka alama ya jiwe au mfano wake ili azikwe maeneo hayo wataokufa katika watu wake. Hilo ni kutokana na Hadiyth ya al-Muttwalib, ambaye ni ´Abdullaah bin al-Muttwalib bin Hantwab[1] (Radhiya Allaahu ´anh), ambaye amesema:

“Wakati alipokufa ´Uthmaan bin Madh´uun lilitolewa jeneza lake na akazikwa. Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alimwamrisha bwana mmoja amletee jiwe ambapo hakuweza kulibeba. Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akamwendea na akakunja dhiraa zake. at-Twalib amesema:

“Amesema yule ambaye amenipa khabari kutoka kwa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam): “Ni kama vile naona ule weupe wa dhiraa za Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) pale alipozikunja.” Kisha akalibeba na akaliweka karibu na kichwa chake na akasema: “Naweka alama kuweza kujua kaburi la ndugu yangu na kuwazika katika maeneo hayo wale jamaa zangu wataokufa.”

Ameipokea Abu Daawuud (02/69) na al-Bayhaqiy amepokea kutoka kwake (03/412) kwa cheni ya wapokezi nzuri. Hayo yamesemwa na al-Haafidhw (05/229). Abu Daawuud akaiwekea mlango “Mlango unaozungumzia kuwakusanya maiti ndani ya kaburi moja na kaburi likatiwa alama.” al-Bayhaqiy pia amefanya hivo “Mlango unaozungumzia kulijulisha kaburi kwa jiwe au alama kwa yale yaliyokuwa.”

Inayo shahidi mbili inazozitilia nguvu ambazo zimezitaja katika “at-Ta´liyqaat al-Jiyaad.”

4- Maiti asitamkishwe shahaadah kama inavotambulika hii leo. Kwa sababu Hadiyth iliyopokelewa juu yake haijasihi[2]. Bali asimame karibu na kaburi na amuombee du´aa ya uimara na msamaha. Awaamrishe wale waliohudhuria pale kufanya hivo. Hilo ni kutokana na Hadiyth ya ´Uthmaan bin ´Affaan (Radhiya Allaahu ´anh) ambaye amesema: “Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) anapomaliza kumzika maiti basi husimama karibu naye na akasema:

“Muombeeni msamaha ndugu yenu na mumtakie uthabiti. Kwani hakika hivi sasa anahojiwa.”

Ameipokea Abu Daawuud (02/70), al-Haakim (01/370), al-Bayhaqiy (04/56) na ´Abdullaah bin Ahmad katika “Zawaaid-uz-Zuhd”, uk. 129. al-Haakim amesema:

“Ni yenye cheni ya wapokezi Swahiyh.”

na adh-Dhahabiy akaafikiana naye. Mambo ni kama alivosema. an-Nawawiy amesema katika “ (05/292):

“Cheni ya wapokezi ni nzuri.”

[1] Asili ilikuwa ni al-Muttwalib bin Abiy Wadaa´ah. Nikasahihisha kama unavoona. Fadhilah zinarudi kwa yule aliyenizindua Dr. ´Abdul-´Aliym ´Abdul-´Adhwiym. Allaah amjaze kheri.

[2] Hivo pia ndivo alivosema Ibn-ul-Qayyim katika “Zaad-ul-Ma´aad” (01/206) na an-Nawawiy na wengineo wakaidhoofisha. Hayo nimeyataja katika “at-Ta´liyqaat al-Jiyaad”. Kisha nikahakikisha kauli katika “Silsilah al-Ahaadiyth adh-Dhwa´iyfah” (559). as-Swan´aaniy amesema katika “Subul-us-Salaam” (02/161):

“Kunafupizwa kutoka katika maneno ya wakaguzi kwamba ni Hadiyth dhaifu. Kuitendea kazi ni Bid´ah. Mtu asidanganyike na wingi wa wenye kuyafanya hayo.”

Katika aliyoyazungumza nimependezwa na maneno yake:

“Kuitendea kazi ni Bid´ah.”

Ukweli huu wanazuoni wengi wameghafilika nao. Wanawekea Shari´ah na kupendezesha mambo mengi kwa Hadiyth mfano wa hii kwa kutegemea baadhi yao juu ya kanuni isemayo “Hadiyth dhaifu inafanyiwa kazi katika kuzungumzia fadhilah za matendo.” Hawakuzindukana kwamba hilo ni kwa yale mambo ambayo yamethibiti katika Qur-aan na Sunnah juu ya kuwekwa kwake Shari´ah na si kuangalia Hadiyth dhaifu peke yake. Kumekwishatangulia juu ya jambo hilo mfano katika maelezo ya ukurasa wa 153. Halafu nikapambanua kauli juu ya masuala haya muhimu hali ya kuwa ni mwenye kunakili maneno kutoka kwa wanazuoni kadhaa ambao ni mabingwa katika utangulizi wangu wa “Swahiyh-ut-Targhiyb”. Tazama (01/34).

  • Mhusika: Imaam Muhammad Naaswir-ud-Diyn al-Albaaniy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Ahkaam-ul-Janaa-iz wa Bid´ahaa, uk. 195-198
  • Imechapishwa: 15/03/2022