103- Inapendekezwa kwa wale waliomo ndani ya kaburi kumimina mchanga mara tatu kwa mikono yake yote baada ya kumaliza kuuziba ule mwanandani. Hilo ni kutokana na Hadiyth ya Abu Hurayrah isemayo:

“Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) aliswalia jeneza kisha akaiendea ile maiti na akammiminia upande wa kichwa chake mara tatu.”

Ameipokea Ibn Maajah (01/474) kwa cheni ya wapokezi. an-Nawawiy amesema (05/292):

“Nzuri.”

Lakini al-Haafidhw amesema:

“Udhahiri wake ni usahihi.”

Kisha akataja kwamba ni yenye kasoro kutokana na kutotajwa baadhi ya wapokezi wake. Hilo nimelibainisha katika “at-Ta´aliyqaat al-Jiyaad”. Lakini Hadiyth ni yenye nguvu kutokana na zile shawahidi zake ambazo amezitaja al-Haafidhw katika “at-Talkhiysw al-Khabiyr” (05/222). Arejee huko yule anayetaka.

Kisha ikanibainikia kwamba kule kutiwa kasoro kulikoashiriwa hakutii dosari. Hilo nimelihakikisha katika “al-Irwaa´” (751).

Kuhusu mapendekezo ya baadhi ya wanazuoni waliokuja nyuma kusema wakati atapomimina mara ya kwanza:

مِنْهَا خَلَقْنَاكُمْ

“Kutoka humo [ardhini] Tumekuumbeni… “

Wakati atapomimina mara ya pili:

وَفِيهَا نُعِيدُكُمْ

“… na katika hiyo [ardhi] tutakurudisheni… “

Wakati atapomimina mara ya tatu:

وَمِنْهَا نُخْرِجُكُمْ تَارَةً أُخْرَىٰ

”… na kutoka humo tutakutoeni mara nyingine.”[1]

ni jambo lisilokuwa na msingi katika Hadiyth yoyote tuliyoiashiria hapo juu.

Kuhusu maneno ya an-Nawawiy (05/293-294):

“Pengine akatolea hoja kwa Hadiyth ya Abu Umaamah (Radhiya Allaahu ´anh) ambaye amesema:

“Wakati Umm Kulthuum msichana wa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alipowekwa ndani ya kaburi basi Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alisema:

مِنْهَا خَلَقْنَاكُمْ وَفِيهَا نُعِيدُكُمْ وَمِنْهَا نُخْرِجُكُمْ تَارَةً أُخْرَىٰ

“Kutoka humo [ardhini] Tumekuumbeni na katika hiyo [ardhi] tutakurudisheni na kutoka humo tutakutoeni mara nyingine.”

Ameipokea Imaam Ahmad kutoka katika upokezi wa ´Ubaydullaah bin Zahr kutoka kwa ´Aliy bin Zayd bin Jud´aan kutoka kwa Qaasim. Watatu wote hawa ni katika wanyonge. Ijapo ni Hadiyth yenye cheni ya wapokezi dhaifu inaweza kuliwazwa katika Hadiyth zinazozungumzia fadhilah za matendo. Aidha inafanyiwa kazi katika mlango wa kupendekeza na kukhofisha ambapo hii ni moja wapo. Allaah ndiye mjuzi zaidi.”

Haya yanajibiwa kwa njia zifuatazo:

1- Hadiyth haina upambanuzi uliyodaiwa kupendekezwa. Kwa hiyo hakuna hoja ndani yake kabisa iwapo cheni ya wapokezi wake itasihi.

2- Upambanuzi uliyotajwa haujathibiti katika Shari´ah kwamba ni katika ubora wa matendo mpaka mtu aseme kwamba Hadiyth hiyo inaweza kufanyiwa kazi kwa sababu inazungumzia fadhilah za matendo. Bali kujuzisha kuifanyia kazi ni kuthibitisha kuwekwa Shari´ah kwa kitendo kwa kutumia Hadiyth ambayo ni dhaifu. Kwa sababu uwekwaji Shari´ah, kiwango chake cha chini kabisa, ni mapendekezo. Mapendekezo ni hukumu miongoni mwa zile hukumu tano ambazo hazithibiti isipokuwa kwa dalili sahihi. Isitoshe dhaifu haileti manufaa kwa maafikiano ya wanazuoni.

3- Hadiyth ni dhaifu mno. Bali imezuliwa katika ukosoaji wa Ibn Hibbaan. Ipo katika “Musnad Ahmad” (05/254) kupitia njia ya ´Abdullaah ´Ubaydullaah bin Zahr kutoka kwa ´Aliy bin Yaziyd, ambaye ni al-Alhaaniy. Maneno ya an-Nawawiy:

“´Aliy bin Yaziyd Jud´aan”

ni kosa kwa sababu ya kwenda kinyume na yale yaliyomo katika “al-Musnad”. Ibn Hibbaan amesema:

“´Ubaydullaah bin Zahr anapokea Hadiyth zilizotungwa kutoka kwa watu madhubuti. Akisimulia kutoka kwa ´Aliy bin Yaziyd basi analeta majanga. Katika cheni ya wapokezi wake kutapokusanyika khabari ya ´Ubaydullaah, ´Aliy bin Yaziyd, al-Qaasim na ´Abdur-Rahmaan basi haitokuwa khabari hiyo isipokuwa ni katika zile zilizofanywa na mikono yao.

Hadiyth hii hali yake nzuri zaidi ni kwamba ni dhaifu mno. Hivyo haitojuzu kuifanyia kazi kwa kauli moja kama alivobainisha Ibn Hajar katika “Tabyiyn-ul-´Ajab fiymaa warada fiy Fadhwl Rajab”.

[1] 20:55

  • Mhusika: Imaam Muhammad Naaswir-ud-Diyn al-Albaaniy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Ahkaam-ul-Janaa-iz wa Bid´ahaa, uk. 193-195
  • Imechapishwa: 15/03/2022