Ni ipi kafara ya msafiri kula ndani ya Ramadhaan?

Swali: Nilisafiri ndani ya Ramadhaan na nikafungua siku moja. Ni ipi kafara?

Jibu: Ikiwa ulikula safarini basi unalazimika kulipa peke yake na wala hakuna kafara. Na ikiwa ulisafiri kwa ajili ya safari basi hapana neno. Bali inapendeza. Allaah (´Azza wa Jall) amesema:

وَمَن كَانَ مَرِيضًا أَوْ عَلَىٰ سَفَرٍ فَعِدَّةٌ مِّنْ أَيَّامٍ أُخَرَ

”Na atakayekuwa mgonjwa au safarini basi [atimize] idadi katika siku nyinginezo.”[1]

Allaah (Subhaanahu wa Ta´ala) amefanya jambo hilo ni lenye wasaa na sahali. Amemruhusu msafiri na mgonjwa kula. Ukisafiri kwenda mahali fulani na ukala siku moja au zaidi, basi unalazimika kulipa na huhitaji kutoa kafara. Isipokuwa ukichelewesha kulipa deni lako mpaka ukaingiliwa na Ramadhaan ya pili kabla ya kulipa, basi unalazimika kulipa baada ya Ramadhaan pamoja na kumlisha chakula masikini juu ya kila siku iliyokupita nusu ya pishi ya tende, mchele au chakula kingine kinacholiwa katika mji kutokana na kuchelewesha. Hivo ndivo wamefutu kikosi cha Maswahabah (Radhiya Allaahu ´anhum) na ndio maoni sahihi zaidi ya wanazuoni. Kwa maana nyingine ni kwamba unatakiwa kulipa siku uliyokula na utoe fidia kwa kuwalisha masikini ikiwa ulichelewesha deni mpaka kukaingia Ramadhaan nyingine.

[1] 02:185

  • Mhusika: Imaam ´Abdul-´Aziyz bin ´Abdillaah bin Baaz
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: https://binbaz.org.sa/fatwas/4776/ما-كفارة-الافطار-في-رمضان-للسفر
  • Imechapishwa: 24/03/2023