Amekula siku 6 Ramadhaan kwa sababu ya masomo

Swali: Mimi ni msichana ambaye mazingira yalinilazimisha kula makusudi siku sita za mwezi wa Ramadhaan kutokana na mitihani ya masomo iliyoanza katika mwezi wa Ramadhaan. Maudhui za masomo ni mgumu. Endapo nisingekula mwaka huu basi nisingeweza kusoma maudhui hizo kutokana na ugumu wake. Naomba ushauri nifanye nini ili Allaah aweze kunisaidia?

Jibu: Ni lazima kwako kutubu kwa Allaah kutokana na hilo. Kwa sababu haijuzu kwako kula katika hali kama hii na ulipe masiku uliyokula. Allaah anamsamehe mwenye kutubia. Hakika ya tawbah inayofuta makosa ni kujikwamua kutokana na dhambi hiyo na kuiacha kwa ajili ya kumtukuza Allaah (Subhaanah), kuogopa adhabu Yake, kujutia yale uliyoyafanya na kuazimia kikweli usirudie huko. Ikiwa dhambi inahusiana na kuwadhulumu watu basi katika utimilifu wa tawbah ni kuwarudishia haki zao. Allaah (Ta´ala) amesema:

وَتُوبُوا إِلَى اللَّـهِ جَمِيعًا أَيُّهَ الْمُؤْمِنُونَ لَعَلَّكُمْ تُفْلِحُونَ

“Tubuni kwa Allaah nyote, enyi waumini, mpate kufaulu.”[1]

يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا تُوبُوا إِلَى اللَّـهِ تَوْبَةً نَّصُوحًا

“Enyi walioamini! Tubieni kwa Allaah tawbah ya kwelikweli.”[2]

Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Tawbah inafuta yaliyo kabla yake.”

“Yule ambaye amemdhulumu ndugu yake katika heshima au kitu kingine, basi ajikwamue leo kabla haijakuwa dinari wala dirhamu. Akiwa na matendo mema, basi yatachukuliwa mema yake kwa kiwango cha alichodhulumu, na asipokuwa na mema, basi kutachukuliwa maovu ya mwenziwe na kubebeshwa yeye.”

Ameipokea al-Bukhaariy katika “as-Swahiyh” yake.

[1] 24:31

[2] 66:08

  • Mhusika: Imaam ´Abdul-´Aziyz bin ´Abdillaah bin Baaz
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: https://binbaz.org.sa/fatwas/11723/حكم-الافطار-من-اجل-الاختبارات
  • Imechapishwa: 24/03/2023