Ni ipi hukumu ya swawm ya mwenye hedhi akioga baada ya alfajiri kuingia?

Swali: Mwenye hedhi amesafika kabla ya alfajiri lakini akaoga baada ya alfajiri. Ni ipi hukumu ya swawm yake?

Jibu: Mwenye hedhi akitwaharika kabla ya alfajiri kuingia hata kama itakuwa ni kwa dakika moja – midhali ana uhakika kuwa amesafika – ikiwa ni katika Ramadhaan ni lazima kwake kufunga. Swawm ya siku yake hiyo ni sahihi kwa kuwa amefunga akiwa msafi. Haijalishi kitu kama hakuoga isipokuwa baada ya alfajiri kuingia. Hakuna neno. Ni kama mfano wa mwanaume ambaye ameamka akiwa na janaba ima ya jimaa au ya kuota usiku, akala daku lakini hata hivyo akaoga baada ya alfajiri kuingia, swawm yake ni sahihi.

Kwa mnasaba huu napenda kuzindua jambo jengine kwa wanawake. Jambo lenyewe ni kwamba baadhi ya wanawake wanadhani wakijiwa na hedhi baada ya juwa kuzama kabla ya kuswali ´ishaa, basi swawm zao siku hiyo zimeharibika. Hili halina msingi. Bali hedhi ikimjia mwanamke baada ya juwa kuzama, hata kama itakuwa kwa muda mfupi, swawm yake ni sahihi na timilifu.

  • Mhusika: Imaam Muhammad bin Swaalih bin ´Uthaymiyn
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Majmuu´-ul-Fataawaa (19/105-106)
  • Imechapishwa: 03/06/2017