Ni ipi hukumu ya kuyaangaza makaburi kwa mishumaa na mataa ya mafuta?

Swali: Katika nchi yetu ni jambo la kawaida kuweka nadhiri ya kuyaangaza makaburi kwa mishumaa. Wanaweka mishumaa kama mfano wa makaburi ya Mitume Swaalih na Muusa (Swalla Allaahu ´alayhimaa swalaatu wa sallam) na makaburi ya mawalii. Wanaweka pia nadhiri iwapo wataruzukiwa mtoto basi wataangaza au kuchinja kwenye makaburi fulani kwa muda wa wiki nzima. Inajuzu kuyaangaza makaburi kwa mishumaa au mataa ya mafuta? Leo imekuwa ni jambo la kawaida kuyaangaza siku za jumatatu au alhamisi usiku wa kuamkia ijumaa. Haya yalithibiti katika zama za Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) au ni Bid´ah?

Jibu: Ni haramu uharibifu kuyaangaza makaburi ya mawalii na ya Mitume. Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amewalaani wenye kufanya hivo. Haijuzu kuyaangaza makaburi haya sawa ikiwa ni usiku wa kuamkia jumatatu au mwengine. Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amemlaani yule mwenye kufanya hivo.

Kujengea juu ya hili ni haramu kuweka nadhiri ya kuliangaza kaburi usiku fulani au mchana fulani. Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Atayeweka nadhiri ya kumtii Allaah na amtii na atakayeweka nadhiri ya kumuasi Allaah na asimuasi.”[1]

Kwa hiyo haijuzu kwake kutimiza nadhiri hii. Lakini, je, ni wajibu kwake kutoa kafara ya yamini kwa ajili ya nadhiri yake hii iliyovunjwa? Wanachuoni wametofautiana juu ya hili. Lililo salama zaidi ni yeye kutoa kafara ya yamini kama ambavyo mtu anatoa kafara kwa ajili ya kiapo kilichovunjwa.

Kuhusu kulenga baadhi ya makaburi ya Mitume, kama kaburi la Mtume Swaalih na Muusa (Swalla Allaahu ´alayhimaa swalaatu wa sallam), si sahihi isipokuwa tu kaburi la Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Makaburi ya Mitume hayajulikani. Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema pindi alipoeleza kwamba Muusa (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alimuomba Allaah amfanye awe karibu na ardhi takasifu:

“Ningekuwa huko ningekuonyesheni kaburi lake karibu na njia kwenye mchanga mwekundu.”[2]

Nafasi hiyo haijulikani leo. Vilevile kaburi la Ibraahiym (Swalla Allaahu ´alayhimaa wa sallam) halijulikani.

[1] al-Bukhaariy (6696).

[2] al-Bukhaariy (1339) na Muslim (2372).

  • Mhusika: Imaam Muhammad bin Swaalih bin ´Uthaymiyn
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Majmuu´-ul-Fataawaa (17/186-188)
  • Imechapishwa: 25/08/2021