Ni ipi hukumu ya kuwazika maiti misikitini?

Swali: Ni ipi hukumu ya kuwazika maiti misikitini?

Jibu: Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amekataza kuwazika maiti misikitini na amekataza makaburi yasifanywe ni mahala pa kuswalia na amemlaani yule mwenye kufanya hivo wakati alipokuwa katika hali ya kukata roho. Ameeleza (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) ya kwamba ni katika matendo ya mayahudi na manaswara[1]. Aidha kitendo kama hicho kinapelekea katika shirki. Kuyafanya makaburi ni mahala pa kuswalia na kuwazika maiti ndani ya misikiti kunapelekea katika shirki kwa kuwa watu wanaweza kufikiria kuwa hawa waliozikwa wana uwezo wa kunufaisha na kudhuru na wana sifa maalum ambazo zinapelekea kushirikishwa pamoja na Allaah (Subhaanahu wa Ta´ala). Ni wajibu kwa waislamu watahadhari kutokamana na madhihirisho haya ya khatari na wahakikishe misikiti haina kaburi kabisa na ijengwe juu ya Tawhiyd na ´Aqiydah sahihi. Allaah (Ta´ala) amesema:

وَأَنَّ الْمَسَاجِدَ لِلَّهِ فَلَا تَدْعُوا مَعَ اللَّهِ أَحَدًا

“Hakika sehemu zote za kuswalia ni kwa ajili ya Allaah, basi msiombe yeyote pamoja na Allaah.”[2]

Ni wajibu misikiti iwe kwa ajili ya Allaah (Subhaanahu wa Ta´ala) na iwe imetakasika kutokamana na madhihirisho haya ya shirki yanayosababisha kuabudiwa wengine badala ya Allaah. Huu ndio wajibu wa waislamu.

[1] al-Bukhaariy (1330) na Muslim (16).

[2] 72:18

  • Mhusika: Imaam Muhammad bin Swaalih bin ´Uthaymiyn
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Majmuu´-ul-Fataawaa (17/210-211)
  • Imechapishwa: 25/08/2021