Ni ipi hukumu ya kusoma Qur-aan kwa ajili ya roho ya maiti?

Swali: Ni ipi hukumu ya kusoma Qur-aan kwa ajili ya roho ya maiti?

Jibu: Kusoma Qur-aan kwa ajili ya roho ya maiti muislamu kwa lengo thawabu zimwendee. Wanachuoni wametofautiana katika maoni mawili:

1 – Ni jambo halikuwekwa katika Shari´ah na yule maiti hanufaiki kwa Quraan katika hali hii.

2 – Maiti ananufaika na inajuzu kumsomea Qur-aan muislamu yeyote ili anufaike na kile kisomo.

Maoni yaliyo na nguvu ni haya ya pili. Kuna dalili ya kwamba inajuzu kumtumia thawabu za ´ibaadah maiti. Mfano wa hilo ni Sa´d bin ´Ubaadah (Radhiya Allaahu ´anh) alitoa swadaqah bustani yake ili thawabu zimwendee mama yake[1]. Kuna mtu pia alimwambia Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

“Mama yangu amekufa. Nadhani kuwa lau angeliweza kutamka basi angetoa swadaqah. Je, nimtolee swadaqah?” Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akasema: “Ndio.”[2]

Hali hizi maalum zinathibitisha kuwa aina ya ´ibaadah fulani inajuzu kumtumia thawabu zake muislamu. Hata hivyo lililo bora ni wewe kumuombea du´aa maiti na ufanye matendo mema kwa ajili ya nafsi yako mwenyewe. Kwa kuwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Anapofariki mwanaadamu matendo yake yote yanakatika isipokuwa mambo matatu; swadaqah yenye kuendelea, elimu watu wananufaika kwayo au mtoto mwema anayemuombea.”[3]

Hakusema “au mtoto mwema anayemsomea Qur-aan, anayemswalia, anayemfungia au anayemtolea swadaqah.” Alisema:

“… au mtoto mwema anayemuombea.”

Mazingira yanahusiana na matendo na inathibitisha kuwa du´aa ndio kitu bora anachoweza mtu kumfanyia maiti, na si kwamba mtu amfanyie matendo mema yule maiti. Mtu yeye mwenyewe ni muhitaji matendo mema na apate thawabu zake zimehifadhiwa kwa Allaah (´Azza wa Jall).

Kuhusu kukodi mtu asome Qur-aan na thawabu za kisomo zimwendee yule maiti, kitendo hicho ni Bid´ah. Katika hali hii thawabu hazimwendei yule maiti kwa kuwa msomaji huyu amesoma kwa ajili ya maslahi ya kidunia. Mwenye kufanya ´ibaadah kwa ajili ya maslahi ya kidunia hana chochote atachopata siku ya Qiyaamah. Allaah (Ta´ala) amesema:

مَن كَانَ يُرِيدُ الْحَيَاةَ الدُّنْيَا وَزِينَتَهَا نُوَفِّ إِلَيْهِمْ أَعْمَالَهُمْ فِيهَا وَهُمْ فِيهَا لاَ يُبْخَسُونَ أُوْلَئِكَ الَّذِينَ لَيْسَ لَهُمْ فِي الآخِرَةِ إِلاَّ النَّارُ وَحَبِطَ مَا صَنَعُواْ فِيهَا وَبَاطِلٌ مَّا كَانُواْ يَعْمَلُونَ

“Anayetaka uhai wa dunia na mapambo yake Tutawalipa kikamilifu matendo yao humo nao hawatopunjwa chochote humo – hao ndio wale ambao hawatokuwa na chochote Aakhirah isipokuwa Moto na yataharibika yale waliyoyafanya humo na ni yenye kubatilika yale waliyokuwa wakiyatenda.”[4]

Hapa napenda kuwanasihi ndugu zangu ambao wamezowea kufanya kama hivi wahifadhi pesa zao na pesa za warithi wa yule maiti na wajue kuwa kitendo hichi ni Bid´ah kwa dhati yake na maiti hafikiwi na hizo thawabu. Mwenye kupokea malipo kwa kitendo hicho anakula mali za watu kwa dhuluma. Aidha maiti hanufaiki na hilo.

[1][1] al-Bukhaariy (2756).

[2] al-Bukhaariy (2670) na Muslim (1004)

[3] Muslim (1631)

[4] 11:15-16

  • Mhusika: Imaam Muhammad bin Swaalih bin ´Uthaymiyn
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Majmuu´-ul-Fataawaa (17/222-224)
  • Imechapishwa: 02/09/2021